2015-02-14 11:58:10

Utamaduni wa mshikamano!


Patriaki Bartolomeo wa kwanza katika hotuba yake wakati wa kutunukiwa Shahada ya heshima ya uzamivu katika masuala ya kijamii kutoka katika Chuo kikuu cha Uchumi cha Smirne, kilichoko nchini Uturuki, hivi karibuni anabainisha kwamba, kuna haja ya kujenga madaraja katika mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kulinda mazingira na kuimarisha utamaduni wa mshikamano wa upendo.

Patriaki Bartolomeo wa kwanza anasema kwamba, vijana wa kizazi kipya wana haki ya kupata ulimwengu usiokuwa na misimamo mikali ya kidini, kinzani na vita inayoendeshwa kwa misingi ya kidini. Watu wanataka kuishi katika mazingira bora zaidi pasi na uchafuzi mkubwa wa mazingira, mambo ambayo yanahatarisha afya, ustawi na maendeleo ya wengi kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Jamii haina budi kuhakikisha kwamba, inawafunda watu wake katika misingi ya maadili na utu wema, ili kupambana kufa na kupona na saratani ya rushwa na ufisadi, inayokwamisha mafao ya wengi kwa kuwatajirisha watu wachache katika jamii. Kimsingi watu wangependa kujenga jamii inayojikita katika mshikamano wa upendo na udugu.

Wachunguzi wa mambo wanasema, katika kipindi cha karne mbili zilizopita, wananchi wengi wamejikuta wakipambana kufa na kupona ili kutafuta haki na usawa; sasa kinapaswa kuwa ni kipindi cha udugu na mshikamano; jambo ambalo kimsingi haliwezekani pasipokuwa na mchango wa dini mbali mbali, hii ndiyo hatari kubwa iliyoko mbele ya Jumuiya ya Kimataifa kwa watu wanaokana umuhimu wa dini katika maisha na vipaumbele vya watu.

Dini zina mchango mkubwa katika mchakato unaowafunda watu kulinda na kutetea mazingira ambayo ni kazi ya uumbaji, kwa kuwataka kujikita katika kulinda, kutetea na kudumisha misingi ya haki na amani. Lakini Patriaki Bartolomeo wa kwanza anasikitika kusema kwamba, wakati mwingine dini imetumiwa vibaya na hivyo kuwa ni chanzo cha vita na kinzani za kijamii, tatizo linalokuzwa na kudumishwa na watu wenye misimamo mikali ya kidini, hatari kubwa ndani ya jamii.

Majadiliano ya kidini katika ukweli na uwazi; katika heshima na kuthaminiana ni nyenzo msingi katika mapambano dhidi ya misimamo mikali ya kiimani, inayoendelea kuhatarisha amani na mfungamano wa kitaifa, sehemu mbali mbali za dunia. Ikumbukwe kwamba, leo hii kuna watu wa dini na tamaduni mbali mbali wanaopaswa kuheshimiana na kuthaminiana, ili kujenga madaraja ya amani, matumaini na udugu, bila ya kujifungia katika masuala ya udini, chanzo kikuu cha misimamo mikali ya kidini.

Changamoto kubwa inayozikabili dini mbali mbali duniani ni kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu, kwa kuzimwilisha mintarafu sheria na kanuni za dini husika; katika ukweli na uwazi. Historia ya madai ya haki msingi za binadamu inafumbatwa katika utu na heshima ya binadamu. Vijana wa kizazi kipya na wasomi hawana budi kuangaliana machoni kwa ujasiri, ili kujenga imani na matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi.

Ni wajibu wa Majaalimu kuhakikisha kwamba, wanawasaidia wanafunzi wao kuwa na uelewa mpana wa maisha na changamoto zake; kwa kukazia tunu msingi za maisha ya kijamii na kiutu, kwani wao ndio wenye dhamana ya kukuza na kuendeleza tunu hizi kwa siku za usoni. Vijana wajishughulishe na masuala ya maisha ya kiroho na kitamaduni kwa kujikita katika kanuni maadili na utu wema; katika uhuru na haki; heshima na mshikamano; kwa kulinda na kutunza mazingira. Elimu inaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa mchakato wa ujenzi wa utamaduni shirikishi unaojikita katika mshikamano, kwa kusaidiana na kuhudumiana.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.