2015-02-14 14:44:41

Ni huduma ya utii na unyenyekevu; hata ikibidi kumwaga damu!


Kardinali Dominique Mamberti, Mwenyekiti wa Mahakama Kuu ya Kitume ya Kanisa Katoliki ndiye aliyepewa heshima ya kutoa shukrani kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa niaba ya Makardinali Wapya 19 waliokuwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican huku wakiungana na Kardinali Josè de Jesus Pimiento Rodriguez ambaye atapokea kofia yake ya Ukardinali nchini Colombia kwa kushindwa kuhudhuria tukio hili muhimu katika maisha na utume wa Kanisa kutokana na uzee.

Itakumbukwa kwamba, Kardinali Pimiento alizaliwa kunako mwaka 1919 na huyu ndiye Kardinali mzee kuliko wote waliotangazwa na kusimikwa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 14 Februari 2015. Makardinali wapya wanatambua kwamba, wameteuliwa kwa ajili ya kutekeleza utume mpya ndani ya Kanisa kama ambavyo Baba Mtakatifu mwenyewe alivyokuwa amefafanua katika barua aliyowaandikia Makardinali wapya, kwa kuwa karibu naye na kwa ajili ya mafao ya Kanisa. Makardinali hawa kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanashiriki katika utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa njia ya huduma kwa Kanisa.

Makardinali wanasema wanapenda kuungana na kushirikishana tone la upendo na utii uliooneshwa na Yesu Kristo kiasi hata cha kuyamimina maisha yake pale juu Msalabani na kwamba, hata wao wanataka kuungana na Yesu, huku wakiendelea kuwajibika kwa njia ya huduma inayojikita katika unyenyekevu, ukarimu, kiasi hata cha kuweza kumwaga damu yao kwa ajili ya wokovu wa roho za waamini na kwa mafao ya Watu wa Mungu.

Makardinali kwa sasa wamekuwa ni sehemu ya maisha na utume wa Kanisa la Roma, kielelezo cha utimilifu wa upendo, tayari kutoka kifua mbele ili kushiriki katika mchakato wa Uinjilishaji, huku wakijenga na kuimarisha mshikamano wa Kanisa la Kiulimwengu. Mshikamano huu unaendelea kuboreshwa kwa njia ya upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo anayewataka kuishi kwa ajili yake Yeye aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu.

Damu ya Mashuhuda wa imani, iwatie nguvu na ujasiri wa kuwa kweli Mashuhuda wa Kristo Mfufuka hadi miisho ya dunia; tayari kupiga magoti ili kuganga madonda ya binadamu wa leo na kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu. Hii ni huduma ya mshikamano na upendo inayotekelezwa kwa njia ya unyenyekevu na uaminifu kadiri ya nguvu na uwezo wao.

Makardinali wanapenda kumhakikishia Baba Mtakatifu Francisko ushirikiano na mshikamano wa kidugu katika utekelezaji wa dhamana na utume wake, katika kuliongoza Kanisa na kuwaimarisha ndugu zake katika imani. Wanaahidi kuendelea kumkumbuka katika utume wake kwa njia ya sala na sadaka ya maisha yao; huku wakitumainia ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mtakatifu Yosefu mlinzi wa Kanisa na watakatifu Petro na Paulo wasimamizi wa Kanisa la Roma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.