Baba Mtakatifu Francisko katika Ibada ya Liturujia ya Neno la Mungu, Jumamosi, tarehe
14 Februari 2015 amewatangaza Makardinali wapya 20 na kuwapatia kofia nyekundu alama
ya ushuhuda wao, pete ya ukardinali pamoja na kuwapangia Makanisa ya huduma mjini
Roma. Makardinali wapya wamekiri Kanuni ya Imani na kula kiapo cha utii kwa Khalifa
wa Mtakatifu Petro pamoja na waandamizi wake. Ibada hii imehudhuriwa pia na Baba Mtakatifu
mstaafu Benedikto XVI.
Itakumbukwa kwamba, Kanisa Barani Afrika limebahatika
kuwapata Makardinali wapya watatu nao ni: Kardinali Berhaneyesus Demerew Souraphiel,
Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Addis Ababa, Ethiopia na Mwenyekiti wa Shirikisho la Mabaraza
ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA. Wa pili ni Kardinali Arlindo
Gomes Furtado, Askofu wa Santiago de Cape Verde, kutoka katika Visiwa vya Cape Verde.
Tatu ni Kardinali Julio Duarte Langa, Askofu mstaafu wa Jimbo la Xai-Xai, Msumbiji.
Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake amewakumbusha Makardinali kwamba,
hiki si cheo cha kujivunia, bali ni nguzo thabiti katika maisha na utume wa Kanisa;
ni kielelezo cha upendo na umoja wa Kanisa kwani Kanisa la Roma linatekeleza wajibu
msingi katika huduma ya upendo, inayopaswa kujionesha kwa njia ya Khalifa wa Mtakatifu
Petro, wakifuatia Makardinali. Mtakatifu Paulo katika Waraka wake wa kwanza kwa Wakorinto
sura ya 12: 31 hadi sura ya 13: 13 anafafanua sifa ya upendo isiyosikilizwa kwa umakini
mkubwa na kumwilishwa na Bikira Maria.
Baba Mtakatifu anasema kwamba, Yesu
Kristo ni upendo kamili uliomwilishwa, awasaidie kuweza kupokea Neno hili na kutembea
katika njia hii, kwa kuwa wanyenyekevu na wapendelevu kama ilivyo kwa mama kwani upendo
ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayokuwa na kukomaa mahali palipo na unyenyekevu
na upole. Upendo ni ukuu unaojionesha katika fadhila ya huduma ndani ya Kanisa mintarafu
Moyo wa Kristo; sawa na Ukatoliki, unaomtaka mtu kupenda bila mipaka akizingatia uaminifu;
mambo yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha. Upendo unawakumbatia wote: wakubwa
kwa wadogo; kwa kuwatikia mema.
Baba Mtakatifu anasema, muujiza wa upendo ni
kwamba: upendo hauhusudu; upendo hautakabari, haujivuni kwani ni tabia ya binadamu
wa nyakati mbali mbali kujikuta anatambukia katika wivu na majivuno, kielelezo cha
ubinadamu uliojeruhiwa kutokana na dhambi ya asili; hali ambayo inaweza kuwagusa hata
viongozi wa Kanisa; lakini upendo wa Kimungu ndani mwao, ulete mabadiliko na kumwonesha
Kristo anayeishi ndani mwao, kwani Yesu ni kielelezo cha upendo mkalimifu.
Baba
Mtakatifu anafafanua kwamba, upendo haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake, kwani
upendo unaheshimu utu wa mtu; unatambua hali na mahitaji yake, lakini kwa mtu mwenye
ubinafsi atajikuta anatafuta mafao yake binafsi badala ya kutoa kipaumbele cha kwanza
kwa Kristo; kwa kuwaheshimu na kuwatakia mema wengine. Upendo hauhesabu mabaya na
unamwokoa mtu kutoka katika hasira na chuki ya kutaka kulipiza kisasi; mambo ambayo
kamwe hayawezi kuvumiliwa kwa kiongozi wa Kanisa.
Baba Mtakatifu anasema, upendo
haufurahii udhalimu bali hufurahi pamoja na kweli, changamoto kwa viongozi wa Kanisa
kujikita katika kutenda haki na kufurahia ukweli unaopata utimilifu wake katika mwili
wa Yesu Kristo, chemchemi hai ya furaha kwa waja wake. Kiongozi wa Kanisa awe ni kielelezo
cha haki na huduma ya furaha katika ukweli.
Upendo huvumilia yote, huamini
yote, hutumaini yote, hustahimili yote; haya ni maneno makuu anasema Baba Mtakatifu
yanayoweza kuwa ni dira na mwongozo wa maisha ya kiroho na shughuli za kichungaji,
ili kuuwezesha upendo wa Kristo uliomiminwa mioyoni mwa waamini kwa njia ya Roho Mtakatifu
kumwilishwa, ili kutoa msamaha, kuwa na imani thabiti kwa Mwenyezi Mungu pamoja na
kuendeleza mchakato wa kuwamegea wengine matumaini, ili kuvumilia hali mbali mbali
za maisha, huku wakiwa wameungana na Yesu, aliyeshikamana na binadamu kwa njia ya
upendo hata akajitwika dhambi zao zote.
Baba Mtakatifu anasema, Mungu ni upendo,
changamoto kwa viongozi wa Kanisa kuwa wanyenyekevu kwa Roho Mtakatifu, ili kweli
waweze kuwa ni nguzo za unyenyekevu kwa dhamana na wajibu wanaokabidhiwa na Mama Kanisa
kwa ajili ya Kanisa la Kiulimwengu. Makardinali watambue kwamba, wao ni kielelezo
cha upendo unaojionesha kwa njia ya unyenyekevu kwa Roho Mtakatifu anayewamiminia
upendo wa Mungu mioyoni mwao!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.