2015-02-13 15:06:48

Washirikisheni watu tabasamu la nguvu!


Katika Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani, Baraza la Maaskofu Katoliki Australia kwa namna ya pekee kabisa, linawaalika Watawa mbali mbali nchini humo, kuhakikisha kwamba, wanaishirikisha Familia ya Mungu nchini Australia upendo na tabasamu kutoka kwa Mwenyezi Mungu. RealAudioMP3
Maadhimisho haya yanakwenda sanjari na Jubilee ya miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipotangaza Waraka wa Upendo Mkamilifu, Perfectae caritatis, ili watawa waweze kupyaisha maisha yao ndani ya Kanisa, tayari kutoka kifua mbele kuwatangazia Watu wa Mataifa, Injili ya Furaha na Matumaini kwa wale waliokata tamaa.
Hii ni changamoto kwa watawa kuhakikisha kwamba, wanakuwa ni mashuhuda wenye mvuto na mashiko kutokana na maisha na utume wao unaomwilishwa katika huduma makini kwa Familia ya Mungu inayowazunguka. Watawa waendelee kuwa ni sauti ya kinabii inayowaamsha walimwengu, daima, wakiwa ni watu wenye furaha, kwa kutambua kwamba, wanapendwa na kuthaminiwa na Mwenyezi Mungu.
Baraza la Maaskofu Katoliki Australia linaendelea kuwahimiza watawa kuhakikisha kwamba, wanasimika maisha yao katika sala na tafakari ya Neno la Mungu, ili waweze kujifunza kutoka kwa Yesu Kristo, ambaye ni Mwalimu na Bwana. Hata pale wanapokuwa wanatekeleza wajibu na dhamana yao, watawa waoneshe umuhimu wa sala na tafakari ya Neno la Mungu.
Walimwengu wanapenda kuwaona watawa wakishuhudia kwa njia ya maisha yao, huruma na upendo wa Mungu, unaoleta mvuto kwa watu kutaka kuchuchumilia yaliyo: kweli, mema na matakatifu. Watawa wawe ni cheche za matumaini kwa wale waliokata tamaa ya maisha; wawe tayari kujisadaka pale wanaohitajika kutoa huduma kwa watu; watawa wawe ni faraja kwa wale waliopondeka moyo; wawe tayari kuwaonjesha waamini wanaokimbilia huruma ya Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho, ili hatimaye, waweze kuonja furaha ya kweli inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.
Kimsingi, watawa wote wanahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanawaonjesha wengine furaha, upendo na huruma ya Mungu. Watambue mapungufu yao ya kibinadamu na waendelee kujitakatifuza, ili kujenga na kudumisha umoja unaojionesha katika maisha ya kijumuiya, ili kuwaamsha walimwengu wanaojikita katika ubinafsi na migawanyiko. Watawa wawe ni chachu inayokoleza maisha ya watu ili kutafuta mafao ya wengi.
Baraza la Maaskofu Katoliki Australia linawaalika Watawa katika maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani, kuhakikisha kwamba, kweli wanaendelea kuwa ni chemchemi ya furaha na matumaini.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.