Hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko alimteua Mheshimiwa Padre Prosper Balthazar
Lyimo, kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo kuu la Arusha, Tanzania. Askofu mteule Lyimo
kabla ya uteuzi huu alikuwa ni Katibu mkuu wa Jimbo na Mkuu wa Mahakama ya Kanisa
Jimbo kuu la Arusha. Askofu mteule anatarajiwa kupokelewa rasmi Jimbo kuu la Arusha,
Jumamosi, tarehe 14 Februari na tarehe 15, Februari 2015 kuwekwa wakfu kuwa Askofu
msaidizi wa Jimbo kuu la Arusha.
Katika mahojiano
maalum na Radio Vatican, Askofu Joseph Mlola wa Jimbo Katoliki Kigoma anamtakia kheri
na mafanikio mema katika maisha na utume wake katika Jimbo kuu la Arusha. Anamwambia
kwamba, asiogope kwani kuna Askofu mkuu Josephat Louis Lebulu atamwongoza na kumwonesha
njia n adira; kuna Maaskofu Katoliki Tanzania wapo ili kujenga na kuimarisha Urika
wao, bila kusahau kwamba, Familia ya Mungu Jimbo kuu la Arusha, inamshindikiza kwa
sala na sadaka yake. Lengo ni kujenga na kudumisha Familia ya Mungu nchini Tanzania.
Askofu mteule Prosper Balthazar Lyimo alizaliwa kunako tarehe 20 Agosti
1964 huko Kyou-Kilema, Jimbo Katoliki la Moshi. Baada ya masomo yake ya shule ya msingi
huko Maua na Arusha, alijiunga na Seminari ndogo ya Jimbo Katoliki Arusha. Alipata
masomo yake ya Falsafa kwenye Seminari kuu ya Kibosho, iliyoko Jimbo Katoliki la Moshi
na masomo ya Taalimungu alipata Seminari kuu ya Kipalapala, iliyoko Jimbo kuu la Tabora.
Baada
ya majiundo yake ya Kikasisi, akapadrishwa Jimbo kuu la Arusha kunako tarehe 4 Julai
1997. Tangu wakati huo amekuwa ni mlezi katika Seminari ndogo ya Jimbo kuu la Arusha
kuanzia mwaka 1997 hadi mwaka 1999. Kuanzia mwaka 2000 hadi mwaka 2004 alikuwa ni
Katibu mkuu wa Jimbo kuu la Arusha. Kunako mwaka 2004 hadi mwaka 2007 alipelekwa na
Jimbo kwa ajili ya masomo ya juu mjini Roma, kwenye Chuo kikuu cha Kipapa cha Urbaniana.
Kunako mwaka 2007 hadi mwaka 2008 alikuwa ni Katibu mkuu wa Jimbo kuu la Arusha.
Kuanzia
mwaka 2008 hadi mwaka 2011 Askofu mteule Prosper Balthazar Lyimo, alitumwa na Jimbo
kuu la Arusha kwa ajili ya masomo ya juu nchini Canada na huko akajipatia shahada
ya uzamivu kutoka katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Paul, kilichoko mjini Ottawa. Na
kunako mwaka 2011 alirejea nchini Tanzania na kupangiwa kazi ya kuwa Katibu mkuu na
Mkuu wa Mahakama ya Jimbo kuu la Arusha.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.