Padre Indunil Kodithuwakku, Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa la Majadiliano
ya kidini anaongoza ujumbe wa viongozi wa Baraza hili katika mikutano ya majadiliano
ya kidini iliyoanza nchini India, kuanzia tarehe 12 na itahitimishwa hapo tarehe 17
Februari 2015. Askofu mkuu Salvatore Pennacchio, Balozi wa Vatican nchini India anashiriki
pia katika matukio haya. Washiriki wa mikutano hii ni kutoka katika nchi mbali mbali
za Bara la Asia.
Wabudha na Wakristo katika mchakato wa kudumisha udugu, ndiyo
kauli mbiu inayoongoza majadiliano haya kwa kutambua kwamba, binadamu wote kwa pamoja
wanaunda familia ya Mungu. Itakumbukwa kwamba, kuna mwingiliano wa tamaduni, lakini
kama waamini wanahimizwa kujenga utamaduni wa udugu na mshikamano, ili kwa pamoja
waweze kupambana na maovu yanayoendelea kujitokeza ndani ya jamii, kwani mshikamano
wa udugu, unafuta machozi na huu ndio mwelekeo mpya.
Haya kimsingi ni mambo
makuu ambayo yanaendelea kujadiliwa na wajumbe katika mikutano iliyoandaliwa na Baraza
la Kipapa la majadiliano ya kidini huko India kwa kushirikiana na Baraza la Maaskofu
Katoliki India. Baraza la Kipapa linaadhimisha Jubilee ya miaka 50 tangu Mababa wa
Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipochapisha Waraka kuhusu majadiliano ya kidini,
chombo ambacho kimekuwa mstari wa mbele katika mchakato wa kukuza na kudumisha misingi
ya haki, amani na uhuru wa kidini.