Baba Mtakatifu Francisko kwa kusoma alama za nyakati amefanya marekebisho makubwa
katika mfumo wa fedha na uchumi mjini Vatican kwa kukazia: ukweli, uwazi, uaminifu
na uwajibikaji kwa fedha za Kanisa zinazopania kuliwezesha Kanisa kutekeleza utume
wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili sanjari
na kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.
Mtakatifu
Yohane Paulo II katika maisha na utume wake, alifanya mageuzi makubwa katika maisha
na utume wa Kanisa kwa kuandika Waraka wa shughuli za kichungaji, maarufu kama "Pastor
bonus". Papa akafuta Baraza la Kipapa la majadiliano na wasioamini kwa kuliunganisha
na Baraza la Kipapa la Utamaduni. Papa Yohane Paulo II akaunda Tume ya kutunza mambo
ya kale, ambayo hapo awali ilikuwa imeunganishwa na Baraza la Kipapa kwa ajili ya
Wakleri na hapa ikaanza kujulikana kama Tume ya Kipapa kwa ajili ya mambo ya kale
ya Kanisa, inayoendelea kushirikiana kwa karibu zaidi na Baraza la Kipapa la Utamaduni.
Baba
Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI kunako mwaka 2010 akaunda Baraza la Kipapa la Uhamasishaji
wa Uinjilishaji Mpya. Mwaka 2011, akaondoa mamlaka ya kutengua uhalali wa Sakramenti
ya Daraja Takatifu kutoka kwenye Baraza la Kipapa la Ibada, Nidhamu na Sakramenti
za Kanisa na kuanzisha Ofisi ambayo kwa sasa iko katika Mahakama kuu ya Kanisa yaani,
Rota Romana. Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI aliunganisha pia Tume ya Kipapa
ya mambo ya kale ya Kanisa kwenye Baraza la Kipapa la Utamaduni.
Ilikuwa ni
mwaka 2013, Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI alipoamua kuondoa madaraka yanayohusu
Seminari kutoka kwenye Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki na kuyaweka mamlaka haya
chini ya Baraza la Kipapa la Wakleri. Masuala ya Katekesi yalihamishwa kutoka kwenye
Baraza la Kipapa la Wakleri kwenda kwenye Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji
mpya. Kwa ufupi haya ndiyo mabadiliko makubwa ambayo yamefanywa katika kipindi cha
miaka ya hivi karibuni, kwa kusoma alama za nyakati ili kuliwezesha Kanisa kutekeleza
utume wake kwa ufanisi mkubwa zaidi.
Na Padre Ricahrd A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.