2015-02-13 08:20:43

Askari watoto na athari zake!


Umoja wa Mataifa unabainisha kwamba, kuna zaidi ya watoto 250, 000 ambao wamepelekwa mstari wa mbele kama wapiganaji, hasa katika nchi maskini zaidi duniani. Hawa ni watoto ambao wamepokwa matumaini ya kupata fursa ya elimu, ili kuwa na matumaini ya kesho iliyo bora zaidi. Ni kundi la watoto ambalo linafanyishwa kazi za kijeshi au wakati mwingine wanapigana bega kwa bega na wanajeshi wengine.

Takwimu hizi zimetolewa na Umoja wa Mataifa, Alhamis, tarehe 12 Februari 2015, Siku ya Kimataifa dhidi ya ajira ya watoto wadogo jeshini. Shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF, linaonesha wasi wasi mkubwa kutokana na taarifa zinazoendelea kuwasili kutoka Sudan ya Kusini na Jamhuri ya watu wa Afrika ya Kati, zikionesha kwamba, kuna idadi kubwa ya watoto wanaoandikishwa jeshini, tayari kupelekwa mstari wa mbele kupigana kama chambo!

Tukio hili limeadhimishwa wakati ambapo Jumuiya ya Kimataifa inafanya kumbu kumbu ya Protokali ya hiyari kuhusu haki za watoto wadogo na vijana iliyopitishwa na Umoja wa Mataifa kunako mwaka 2002. Hiki ni chombo cha kisheria ambacho kimetiwa mkwaju na Nchi 153 ili kuzuia uandikishaji wa watoto wadogo kwenye majeshi au kwa kuajiriwa kwenye makundi ya wanajeshi waasi.







All the contents on this site are copyrighted ©.