Bado wahamiaji wanaendelea kupoteza maisha yao katika Bahari ya Mediterrania hata
baada ya kunyanyaswa na kudhulumiwa na wafanyabiashara haramu ya binadamu. Taarifa
kutoka Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba, wahamiaji 232 wengi wao wakiwa ni wanawake
na watoto, wamekufa maji na kwamba, kuna mashua moja imepotea ambayo pia inasadikiwa
kuwa na idadi kubwa ya wahamiaji, ambao pia wanahofiwa kwamba, wamefariki dunia.
Ikiwa
kama takwimu za awali na ambazo zimekwisha kutolewa hadi sasa zitaweza kuthibitishwa,
basi kuna wahamiaji zaidi ya 400 watakuwa wamekufa maji katika siku za hivi karibuni.
Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano, tarehe 11 Februari wakati wa Katekesi yake, amesema
kwamba, anaendelea kufuatilia taarifa za maafa yanayoendelea kujitokeza kwenye Bahari
ya Mediterrania kwa masikitiko makubwa, kwani kuna watu bado wanaendelea kupoteza
maisha yao na kwamba, anapenda kuwahakikishia wote sala na uwepo wake kiroho!
Mashuhuda
wanasema kwamba, hali ya hewa ilikuwa mbaya, lakini wafanyabiashara haramu wa binadamu
wakawalazimisha kupanda kwenye mashua na kuanza safari, vinginevyo, wangekiona cha
mtema kuni. Mashua nne zilizokuwa zimebeba wahamiaji 460, wakati wakiwa njiani, mashua
moja ikazama maji na abiria wote wakapoteza maisha.
Hii ni safari iliyoanza
huko Tripoli, Libya, Mwishoni mwa Juma. Baadhi ya wahamiaji waliweza kuokolewa na
Kikosi cha Wanamaji wa Italia, lakini wengi wao walikuwa na hali mbaya sana kiasi
cha kuhitaji huduma ya haraka. Jumuiya ya Kimataifa inaendelea kujadili kuhusu hatima
ya wahamiaji kwenye Bahari ya Meditterania, lakini watu wanaendelea kupoteza maisha!