2015-02-12 10:44:24

Watawa ni mashuhuda wa furaha!


Kila alipo mtawa kuna furaha ndiyo kauli mbiu ya Mwaka wa watawa nchini Tanzania. Hii ndiyo mada iliyojiri kwenye sherehe za kuzindua rasmi Mwaka wa Watawa Duniani kwenye Jimbo Katoliki Moshi, nchini Tanzania, hivi karibuni, katika Ibada ya Misa Takatifu, iliyoongozwa na Askofu Isaac Amani wa Jimbo Katoliki la Moshi na kuhudhuriwa na watawa zaidi ya elfu moja kutoka mashirika 26 ya watawa wa kike na wa kiume wanaohudumu jimboni humo. Nayo furaha na vigelegele vilijionyesha wazi kwenye nyuso za watawa, kwenye nyimbo na ibada nzima ya kuuzindua Mwaka wa Watawa Jimboni Moshi.

Ibada hiyo ya Misa ilianza na maandamano na mishumaa inayowaka ishara ya Mwanga wa Kristo aliyefufuka kutoka kwenye giza. Askofu Amani alisema kwamba Kristo akiwa kati ya watu, basi mwanga wa imani na amani hutawala mahali hapo.

Askofu aliyataja malengo ya siku hiyo kuwa ni kusherehekea na kuuzindua rasmi mwaka wa watawa jimboni humo. Alimnukuu Baba Mtakatifu Francisko anayewahimiza watawa wote kutafakari juu ya swala zima la utii ndani ya mwaka huu wa kanisa, ili kila mtawa aweze kuimarika na kujipanga upya katika wito na maisha yake.

Aliutaja utii wa Watawa kama ule wa Yesu Kristo uliodhihirika kwa matendo na mtindo wake wa maisha. Askofu Amani alisema kwamba, maisha ya utawa yana maana na thamani kubwa sana katika Kanisa na kwamba kwa nadhiri za usafi kamili, ufukara na utii, watawa hujifunga na Mungu hadharani ili waweze kuishi maisha ya ushuhuda wa injili kwa imani na ujasiri mkuu ndani ya Shirika husika, na ndani ya Mama Kanisa. Aliwaomba watawa wote kuwa na umoja na kushirikiana kikamilifu na wadau wengine wa Injili ili kuyapa maisha thamani na tija. Alisema ni muhimu sana kuwaombea watawa wote neema ya kudumu bila kukata tamaa wanapokumbana na changamoto mbalimbali kwenye maisha na utume wao.

Askofu Amani aliwaomba watawa wote kusoma na kutafakari Injili, huku wakiongozwa na fikra na hadhi ya kitawa huku wakijikana nafsi na kumfuasa Yesu Kristo, kwa unyenyekevu bila ya kiburi au unafiki. Akiinukuu Barua ya Mtakatifu Paulo kwa Wafilipi, aliwaomba watawa kuwa na msimamo ule ule aliokuwa nao Kristo mwenyewe, kwani japo kwa asili alikuwa Mungu, lakini hakuona kule kuwa sawa na Mungu ni kitu cha kunga’angania sana, akajinyenyekesha hadi kufa Msalabani kwa ajili ya ndugu zake. (Phil. 2:3-5).

Uzima wa milele una gharama kubwa. Hivyo ni sharti watawa wote wazingatie Maandiko Matakatifu na Katiba ya shirika ili waweze kuendeleza, ndani ya Kanisa, kile ambacho waanzilishi wao walikitarajia, na kwa maisha na mitindo ya maisha yao, Watawa wafufue ile roho iliyowasukuma waanzilishi kuanzisha Mashirika ya kitawa na kazi za kitume.
Askofu Amani alisema kuwa Roho Mtakatifu huyaangazia mashirika mbalimbali namna ya kuwa mashhuhuda na mashujaa wa injili, hivyo hawana budi kuishikilia Injili ambayo Mama Kanisa anaitangaza kwa ari, bidii na moyo mkuu Aliwasihi watawa wote kuutafuta kwanza ufalme wa Mungu na haki yake kwa furaha kuu ili waweze kuwa mwanga Shirikani, Kanisani na katika jamii.

Wakati wa sherehe hizo, Padri Gabriel Mrina wa Shirika la Kazi za Roho Mtakatifu alitoa hamasa kwa watawa waliohudhuria kwa kumtaja Papa Francisko kama kingozi anayewashangaza wengi kutokana na utu wake na unyenyekevu wa hali ya juu unaompelekea kuwa na mahusiano ya kipekee na watu wa kawaida na hasa kwa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Alionyesha jinsi Baba Mtakatifu Fransisko mara kwa mara ameliacha gari lake na kutembea kwa miguu ili kuweza kuwafikia watu hao.

Padri Mrina alimtaja Papa Francisko kama kiunganisho na kivutio hata kwa watu wa madhehebu mengine. Ni kiongozi anayeonesha wazi furaha ya Injili kama unavyoshauri waraka wake wa kitume Evangelii gaudium, yaani Injili ya Furaha, ambayo kila mtawa anahimizwa kuizingatia ili utume wa kitawa uweze kuenezwa kwa furaha, na kwa kila mtu.

Padri Mrina aliwaomba watawa wote kuwa makini na kuwaendea maskini walio kati yao na kuwahudumia kwa upendo na furaha, huku akiwapa changamoto ya kwenda kila mahali bila ya kujali hali zao. Alitoa mfano wa jinsi Malaika walivyowatembelea wachungaji malishoni na hao wachungaji walionekana kama watu duni. Nao wachungaji wanafurahi na kumwendea Yesu Kristo, na wakawa wa kwanza kuieneza habari njema ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo. Kumbe watawa wote wanaalikwa kuwaendea watu kwa furaha na kuwaletea habari njema ya Kristo. Watawa wakijazwa na furaha ya huduma ndani mwao, itakuwa rahisi kwao kuwaletea wengine furaha hiyo.

Padri Mrina alionya kuhusu kubanwa na vionjo vya dunia ya leo ya utandawazi na hivyo kwa watawa kukosa nafasi kwa ajili ya huduma kwa wengine, na kuwahimiza wakite mizizi kwenye sala za pamoja na za binafsi, kwenye kulitafakari Neno la Mungu na katika kupokea Sakramenti ili waweze kuisikia sauti ya Mungu inayowajaza tamaa ya kutenda mema.

Aliwaomba kutafuta kwanza ufalme wa Mungu kwa kujitoa sadaka ili kukuza maisha ya imani kwani dunia ya utandawazi na utafiti wa kila namna inahitaji pia Wainjilishaji wataalam wenye uhusiano mwema na Mungu; anayewatuma kuendeleza utume wake. Kwa kujenga uhusiano mzuri na Mungu, watawa hupata maarifa ya kutimiza vyema utume wao.

Na Sr. Bridgita S. Mwawasi, SSJ
Moshi, Kilimanjaro. Tanzania.








All the contents on this site are copyrighted ©.