2015-02-12 12:14:59

Mheshimiwa Padre Francois Gnonhossou ateuliwa kuwa Askofu wa Jimbo la Dassa-Zoume, Benin


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Mheshimiwa Padre Francois Gnonhossou kutoka Shirika la Wamissionari wa Afrika, kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Dassa-Zoumè, lililoko nchini Benin. Tangu mwaka 2010, Jimbo hili limekuwa wazi, baada ya Askofu Antoine Ganyè kuteuliwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Cotonou, Benin.

Askofu mteule Francois Gnonhossou, S.M.A. alizaliwa tarehe 3 Desemba 1961 huko Dassa-Zoumè. Baada ya masomo na maisha uraiani, akajiunga na mchakato wa masomo na majiundo ya kikasisi nchini Benin na Nigeria na kuweka nadhiri zake za daima kwenye Shirika la Wamissionari wa Afrika kunako tarehe 6 Desemba 1996 na hapo tarehe 26 Julai 1997 akapewa Daraja Takatifu la Upadre.

Katika maisha na utume wake kama Padre amewahi kuwa Paroko msaidizi na hatimaye Paroko; Mlezi wa vijana wanaoishi katika mazingira hatarishi; Msaidizi mkuu wa Shirika katika malezi, Kanda ya Afrika, Mkuu wa Malezi Kanda ya Afrika, Paroko msaidizi na mhamasishaji wa shughuli za kimissionari nchini Canada. Kuanzia mwaka 2013 amekuwa mjini Roma kama Mshauri mkuu wa Shirika la Wamissionari wa Afrika.

Wakati huo huo, Baba Mtakatifu Francisko, amekubali ombi lililowasilishwa kwake na Askofu mkuu Ildefonso Obama Obono wa Jimbo kuu la Malabo, nchini Guinea Ekwatorio kadiri ya Sheria za Kanisa namba 401 § Ibara ya 1. Wakati huo huo, Baba Mtakatifu amemteua Askofu Juan Nsue Mayè kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Malabo. Kabla ya uteuzi huu, alikuwa ni Askofu wa Jimbo Katoliki Ebebiyin.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.