Maadhimisho ya Siku za Wagonjwa Duniani ni mwaliko na changamoto kwa waamini kuhakikisha
kwamba, wanawasaidia na kuwaonjesha wagonjwa imani, matumaini na mapendo katika hija
ya maisha yao, kwa kutambua kwamba, hata katika magonjwa yao, bado utu na heshima
yao kama binadamu inapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa na wote!
Baba Mtakatifu
Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuendelea kujisadaka
kwa njia ya huduma makini kwa wagonjwa, wazee, walemavu na watu pweke, ili waweze
kuonja tena thamani na utu wao kama binadamu, walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.
Kadiri ya taratibu zilizowekwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI kwamba,
maadhimisho makuu ya Siku za Wagonjwa, Familia na Vijana yatafanyika katika ngazi
ya kimataifa kila baada ya miaka mitatu. Kutokana na mantiki hii, Maadhimisho ya Siku
ya 24 ya Wagonjwa Duniani kwa Mwaka 2016 yatafanyika mjini Nazareth, Nchi Takatifu,
kwa kuongoza na kauli mbiu "Kujiaminisha kwa Yesu kama Bikira Maria: Lolote
atakalowaambia fanyeni" (Yoh. 2:5).
Hapa Bikira Maria anakuwa ni kielelezo
muhimu cha imani tendaji na faraja kwa wote wanaoteseka kiroho na kimwili pamoja na
mshikamano wa upendo na udugu kutoka kwa wahudumu wa sekta ya afya, ndugu na majirani.
Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa wafanyakazi katika Sekta ya Afya mwaka
2015 linaadhimisha kumbu kumbu ya miaka thelathini tangu lilipoanzishwa na Mtakatifu
Yohane Paulo II. Katika miaka yote hii, limekuwa ni kituo rejea cha imani, matumaini,
mapendo na mshikamano katika sekta ya afya, kwa kusimama kidete kulinda na kutetea
utu na heshima ya binadamu.
Padre Augusto Chendi, Katibu mkuu msaidizi wa Baraza
la Kipapa la huduma za kichungaji kwa wafanyakazi katika sekta ya afya anabainisha
kwamba, Mwaka 2015, Kanisa linaadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 20 tangu Mtakatifu Yohane
Paulo II alipochapisha Waraka wa Injili ya Uhai, ili kulisaidia Kanisa kusimama kidete
kulinda, kutetea, kuhudumia na kutangaza Injili ya Uhai.
Tarehe 25 Machi 2015,
Baraza hili la Kipapa litapembua kwa kina na mapana: matatizo na changamoto zinazojitokeza
katika Injili ya Uhai, ili kuwasaidia waamini na watu wenye mapenzi mema, kukataa
katu katu utamaduni wa kifo. Tarehe 15 na 16 Mei, 2015 kutafanyika kongamano la kimataifa
kuhusu magonjwa nadra katika maisha ya mwanadamu, lengo ni kujenga na kukuza mshikamano
wa upendo. Tarehe 18 Mei 2015 wajumbe kutoka Mabaraza ya Maaskofu Katoliki duniani
watapanga na kuibua mbinu mkakati wa kupambana na changamoto pamoja na vizingiti dhidi
ya Injili ya Uhai.
Baraza linajiandaa pia kuchapisha Mwongozo kwa ajili ya
wafanyakazi katika Sekta ya Afya, ili kupyaisha Mwongozo uliokuwa umechapishwa kunako
mwaka 1994, ili kutetea Injili ya Uhai kwa kuzingatia kanuni maadili, utu wema na
Mafundisho ya Kanisa.