2015-02-11 15:18:09

Unganeni katika kifungo cha upendo!


Baba Mtakatifu Francisko katika mwendelezo wa katekesi yake kuhusu familia baada ya kuzungumzia: Mama na Baba, Jumatano tarehe 11 Februari 2015 amewageukiwa watoto ambao ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu; kwa kutambua umuhimu na dhamana yao katika maisha ya kifamilia. Nabii Isaya anasema inua macho yako, utazame pande zote: wote wanakusanyana, wanakujia wewe. Wanawako watakuja kutoka mbali, na binti zako watabebwa nyongani. Ndipo utakapoona na kutiwa nuru, moyo wako utatetemeka na kukunjuka.

Baba Mtakatifu anasema, watoto ni chamchemi ya furaha na matumaini kwa wazazi wao; matunda ya upendo kati ya Baba na Mama na zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu anayemkiria kila mtu anayezaliwa ulimwenguni hadhi na utu unaopaswa kulindwa na kuheshimiwa.

Amri ya nne ya Mungu, inawataka watoto kuwaheshimu wazazi na ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuona mahusiano yaliyopo kati ya vizazi na kifungo cha Kimungu ambacho kinaathiri mahusiano mengine yote muhimu ndani ya Jamii katika ujumla wake. Kanisa kwa namna ya pekee linapenda kukazia uwajibikaji na ukarimu wa kurithisha zawadi ya uhai katika jamii yenye afya bora; inayoimarishwa na kupyaishwa sanjari na kuboreshwa kwa uwepo wa vijana wa kizazi kipya.

Baba Mtakatifu Francisko anamwomba Yesu, Mwana wa Mungu na familia ya binadamu, awasaidie waamini na jamii katika ujumla wake, kulinda na kuthamini zawadi ya uhai; utu na heshima ya familia sanjari na kutekeleza dhamana ya kuwasaidia vijana wa kizazi kipya kuwa na matumaini, furaha na ujasiri kwa leo na kesho iliyo bora zaidi.

Baba Mtakatifu anaungana na mahujaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaofanya hija ya maisha ya kiroho kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Lourdes, Ufaransa, kutambua umuhimu wa kupokea na kutunza zawadi ya uhai kwa ukarimu na furaha, ili kujenga na kuimarisha umoja na udugu. Ulimwengu unawahitaji Wakristo wanaoshuhudia imani yao kwa Mwenyezi Mungu kwa njia ya ukarimu sanjari na kukumbatia zawadi ya uhai. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, familia zitaendelea kushirikiana kutekeleza mpango wa Mungu katika maisha yao.

Baba Mtakatifu anasema, watoto ni zawadi ambayo inapaswa kulindwa, kutunzwa na kuendelezwa kwa hali na mali na wazazi pamoja na walezi. Watoto kwa upande wao, wanapaswa kuwaheshimu, kuwatunza na kuwasaidia wazazi wao, wote wakiwa wameunganika katika kifungo cha upendo. Baba Mtakatifu anawaombea watoto wema pamoja na kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwaongoa watoto watukutu.

Mara baada ya Katekesi yake, Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, kwa masikitiko makubwa amepokea taarifa za wahamiaji waliofariki dunia kwenye bahari ya Mediterrania kutokana na baridi kali wakati wakiwa njiani kuelekea Italia. Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia wahanga wa tukio hili sala zake pamoja na kuendelea kuhimiza mshikamano, ili asiwepo hata mtu mmoja anayekosa msaada.

Mwishoni, Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya kuwaombea Makardinali watakaokutanika mjini Vatican, ili Roho Mtakatifu awasaidie katika kazi zao na kuwaangazia Makardinali wapya ili waweze kutekeleza barabara huduma yao kwa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.