2015-02-11 10:33:40

Ukraine kunawaka moto!


Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican anabainisha kwamba, Vatican inaendelea kufuatilia kwa umaskini mkubwa machafuko na vita inayoendelea sehemu mbali mbali za dunia na kati yake ni vita huko Ukraine, ambayo inaendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Mara kadhaa, Baba Mtakatifu Francisko amewasihi wadau mbali mbali kusitisha vita na kuanza kujikita katika majadiliano ya kisiasa ili amani iweze kupatikana, lakini hadi sasa juhudi hizi zote zimegonga mwamba.

Baba Mtakatifu anaendelea kuwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya kuwaombea watu waliofariki dunia kutokana na vita huko Ukraine pamoja na wale ambao wamepata majeraha ili waweze kupona haraka. Jambo la msingi ni majadiliano, ili kweli amani iweze kupatikana badala ya kuendelea na mtindo wa sasa wa kulaumiana na kushambuliana. Majadiliano ya kisiasa pamoja na kuzingatia sheria za kimataifa ni mambo msingi yanayoweza kusaidia mchakato wa amani ya kudumu nchini Ukraine.

Hapa kama alivyowahi kusema Mtakatifu Yohane Paulo II kuna haja kwa binadamu kuwa na ujasiri wa kutumia hoja ya nguvu kwa kujikita katika hoja ya sheria. Baba Mtakatifu anasubiri kwa hamu na matumaini makubwa kukutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Ukraine wakati wa hija yao ya kitume inayofanyika walau kila baada ya miaka mitano mjini Vatican.

Maaskofu hawa watakuwa mjini Vatican kuanzia tarehe 16 hadi 21 Februari 2015. Hapa itakuwa ni fursa kwa Baba Mtakatifu kupata habari za moja kwa moja kwa kile kinachoendelea nchini Ukraine, tayari kuanza mchakato wa haki, amani na upatanisho.

Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kukutana na kuzungumza na Chancellor, Angela Merkel mjini Vatican tarehe 21 Februari 2015. Mgogoro wa Ukraine ni kati ya ajenda ambazo, bila shaka Baba Mtakatifu atapenda kuzungumza na mgeni wake, ili kuonesha wasi wasi wake kuhusiana na hali halisi huko Ukraine.







All the contents on this site are copyrighted ©.