2015-02-11 15:41:12

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya VI ya Kipindi cha B wa Kanisa


Mpendwa mwana wa Mungu, tupo katika jahazi tukielekea ng’ambo ya pili ya ziwa, tukitaka kuchota furaha na matumaini yaletwayo na Neno la Mungu. Ni meza ya neno la Mungu dominika ya sita ya mwaka B. Unaalikwa kumtumaini Bwana aliyekuja kutuondoa katika utengano katika maisha yetu unaowakilishwa kwa alama ya ukoma. RealAudioMP3

Tunasikia kutoka kitabu cha Walawi sura ya 13 jinsi ambavyo wagonjwa wa ukoma na magonjwa mengine katika jamii ya Waisraeli walivyotengwa toka jumuiya yao. Utengano ulijionesha katika sura mbalimbali: walikuwa na maziko tofauti na ndiyo maana hakuna aliyetaka kukaa na wakoma katika maisha na hata kifoni. Wakoma walidharauliwa na hata kuamriwa kutangaza daima wanapokaribiwa na watu kwa maneno haya “Niko najisi, niko najisi”. Suala hili kwa Waisraeli lilijitokeza kwa maana waliwaza kuwa daima jumuiya ni watu walio safi tu! Hii itakuwa ajabu kidogo kama hata sisi tutaweza kufikiri namna hii! Lakini fikiria madhulumu dhidi ya maalbino!

Mpendwa msikilizaji, katika Dominika iliyopita Bwana aliwaponya wenye pepo, homa, na wenye maradhi mbalimbali, likiwa ni ashilio kwamba ujio wa Masiha ni ahueni, ni ukombozi kwa wakoma hawa waliokuwa wametengwa katika jumuiya yao. Kumbe hata leo Bwana ni kwa ajili ya watu kama hawa ambao hutengwa na jumuiya, tuweni makini!

Mtume Paulo katika barua yake ya I sura ya 10 anaendelea kuwafundisha Wakorinto kuwa yote wayafanyayo yawe kwa sifa na utukufu wa Mungu. Daima waweni watu wa furaha na matumaini kiasi kwamba wawe ni kichocheo cha imani kwa wengine wasio na matumaini. Wajitahidi kukwepa makwazo kwa wengine. Wawe kinyume na utengano kama huo tuliousikia hapo mwanzo. Mawaidha haya ni kwa ajili yetu na vizazi vijavyo katika harakati za kutunza imani, matumaini, amani na mshikamano unaoondoa ubaguzi katika jumuiya ya kimataifa.

Sehemu ya Injili ya Marko sura ya I katika Dominika hii yatufundisha kuwa Yesu ni Masiha anayeleta ukombozi kwa watu na hasa wale walio maskini. Somo la kwanza latuambia jinsi wakoma walivyotengwa katika familia ya Waisraeli na hivi hata kutokuwa na thamani yoyote. Leo hii Bwana kwa furaha anamponya mwenye ukoma na kumrudisha katika jumuiya. Katika hili, Bwana anikumbusha maneno yake katika Injili ya Luka 4:18-19 akisema nimekuja kuwahubiria maskini habari njema na kuwarudishia uhuru waliotengwa.

Waisraeli waliwaogopa wakoma lakini Bwana anamgusa mkoma na anapona na hivi Bwana akigusa roho zetu twapona haraka pasipo kuchelewa, cha msingi tumwendee kama mkoma alivyomwendea kwa imani na unyenyekevu. Ndiyo kusema wajibu wetu leo ni kutafuta zaidi kukutana na Mungu kwa njia ya waliotengwa, wanaohangaika na taabu mbalimbali katika maisha yao. Tunapaswa kuguswa na utu wa ndani na kisha tutoke nje na kutazama kwa macho yaliyojaa upendo.

Bwana hataki watu wafahamu nani amemponya mkoma yule maana wataweza kuchanganya mambo na kuanza kumwona Masiha wa miujiza badala ya Masiha wa upendo. Pole pole Masiha atafunuliwa na itakuwa wazi pale msalabani akida asemapo “ Hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu” hii ni siri ya kimasiha. Yesu anataka Manabii na Makuhani wafahamu kuwa Mungu amewatembelea watu wake, Nabii mkuu yuko katikati yao.

Huyu mkoma anatangaza kwa furaha kile alichokatazwa, ndiyo kusema tayari anaonesha furaha ya kukombolewa. Kumbe hata sisi leo kwa ukombozi tulioupata hatutaweza kuficha furaha yetu katika kutangaza matendo makuu ya Bwana. Kwa namna hiyo kuimarisha maisha ya kujitoa kutangaza habari njema kwa mataifa.
Nakutakieni heri na baraka za Mungu katika Dominika hii, tukutane tena siku kama ya leo kwa chakula zaidi cha roho zetu.

Tumsifu Yesu Kristo. Ni Pd Richard Tiganya C.PP.S








All the contents on this site are copyrighted ©.