2015-02-11 08:50:55

Mwongozo wa mahubiri!


Baraza la Kipapa la Ibada, nidhamu na Sakramenti za Kanisa limezindua rasmi Mwongozo wa Mahubiri, ili kuwasaidia Wakleri kupata sanaa itakayowawezesha kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa umakini zaidi, kwani mahubiri si mahali pa kuwakaripia watu, wala jukwaa la michezo ya kuigiza. Tayari Mwongozo huu umekwisha chapishwa na Idara ya Uchapaji ya Vatican, katika lugha ya Kiingereza na Kiitalia, ili kuyasaidia Mabaraza ya Maaskofu kufanya tafsiri kwa lugha mbali mbali.

Akizindua Mwongozo huu, Kardinali Robert Sarah, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Ibada, nidhamu na Sakramenti za Kanisa, anasema, hiki ni chombo ambacho kimekuwa kikisubiriwa kwa hamu kubwa kutokana na mahitaji yake msingi, yanayopania kuleta maboresho katika maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa, ili kumtukuza Mwenyezi Mungu na mwanadamu kutakatifuzwa.

Ni changamoto ambayo ilianza kujitokeza wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu iliyofanyika kunako mwaka 2005 na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI akakazia umuhimu wa mahubiri katika Waraka wake wa kitume, Neno la Bwana, "Verbum Domini", kwa kusema kwamba, mahubiri ni sanaa ambayo Wakleri wanapaswa kujifunza. Papa Francisko katika Waraka wake wa kitume, Injili ya Furaha, "Evangelii gaudium" anasema, Kanisa halina budi kufanya maboresho makubwa ili kuwasaidia Wakleri waweze kuhubiri vyema, kwa kutambua kwamba, wao ni Wahudumu wakuu wa Neno la Mungu.

Hapa anasema Kardinali Sarah, kuna haja ya kujifunza kuhubiri, ili kuweza kuwasilisha vyema ujumbe unaokusudiwa na Mama Kanisa kwa ajili ya Familia ya Mungu, kwani mahubiri yanapaswa kuwa ni kielelezo cha maisha na utume wa Mhubiri, kwani anapaswa kuhubiri kile anachoishi na kutenda. Mkleri lazima ajitahidi kumhubiri, Mungu aliye hai, jambo ambalo linapata chimbuko lake katika majadiliano kati ya Mwenyezi Mungu na Padre katika sala na tafakari.

Umuhimu wa mahubiri, umefafanuliwa kwa kina na mapana na Askofu mkuu Arthur Roche, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Ibada, nidhamu na Sakramenti za Kanisa kwa kusema kwamba, Wakleri hawana budi kujiandaa kikamilifu kabla ya kuanza kuhubiri, kwani hii ni sehemu muhimu sana ya utume wao kama Mapadre, changamoto na mwaliko kwa Wakleri kujisadaka kutafuta muda wa kutosha kwa ajili ya kusali, kutafakari na kuandaa mahubiri mazuri yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha yao mintarafu changamoto za shughuli za kichungaji.

Magwiji wa mahubiri kama akina Mtakatifu Ambrose na Papa Leo mkuu wanabainisha kwamba, mahubiri mazuri ni yale yanayogusa watu kutoka katika undani wa mioyo yao katika matukio husika na kwa wakati muafaka. Wakleri wasihubiri kiasi cha kuwachosha watu na kuanza kusinzia na wala wasitoe mahubiri mafupi kana kwamba, wanaharaka ya kufa mtu! Wakleri wawe makini kusoma alama za nyakati na mazingira.

Kardinali Sarah anasema, kwa maeneo ambayo waamini wanafika mara moja kwa ajili ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, hapa kuna haja ya kuhakikisha kwamba, wanapatiwa Neno litakalowasaidia katika hija ya maisha yao; Watu wa Mungu wafundishwe kikamilifu bila kuwachosha au kuwatesa kwa mahubiri marefu!

Akichangia mada katika uzinduzi wa Mwongozo wa mahubiri, Padre Filipo Riva, afisa wa Baraza hili la Kipapa anasema, watu wanachoka kusikiliza mahubiri yasiyokuwa na mashiko na matokeo yake, wanaanza kusinzia na kukosa hamu ya kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu. Pale inapofaa kuna haja ya kusikiliza shuhuda kutoka kwa waamini wenyewe, kama sehemu ya mchakato wa sanaa ya majadiliano katika maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa.

Mwongozo huu umegawanyika katika sehemu kuu mbili: Sehemu ya kwanza ni: Mahubiri na Mazingira ya Kiliturujia, hapa Kanisa linatoa maana ya mahubiri katika maisha na utume wa Kanisa. Sehemu ya Pili inahusu: mbinu, mikakati na mahudhui ya sanaa ya mahubiri. Mahubiri yazingatie Liturujia ya Kanisa. Mwongozo wa mahubiri ni chombo kinachopania kuwasaidia Wakleri kuandaa mahubiri kadiri ya Liturujia ya Kanisa. Maaskofu wa majimbo wanahamasishwa kuhakikisha kwamba, wanasaidia mchakato wa maboresho ya mahubiri majimboni mwao. Majandokasisi wafundwe barabara sanaa ya mahubiri, tangu mwanzo wanapokuwa Seminarini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican







All the contents on this site are copyrighted ©.