Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema
kuwa uongozi siyo kujisifu na kujisifia tu bali ni kutenda vitendo na kufanya maamuzi
yanayothibitisha na yanayolingana na sifa hizo. Rais Kikwete ameyasema hayo, Jumanne,
Februari 10, 2015, wakati alipofungua jengo la kisasa kabisa la kitega uchumi lenye
thamani ya sh. bilioni 64 kwenye Manispaa ya Moshi katika siku yake ya kwanza ya ziara
ya siku mbili ya kikazi Mkoani Kilimanjaro.
Jengo hilo linalojulikana kama
Kilimanjaro Commercial Complex na lililoko katikati ya Manispaa ya Moshi limejengwa
kwa ubia wa Shirika la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii la NSSF, taasisi ya Girls Guide Tanzania,
taasisi ya Red Cross na Chama cha Uzazi na Malezi Bora Tanzania (UMATI) na ndilo jengo
kubwa kuliko yote katika manispaa hiyo.
Amelisifia uongozi na maono ya maamuzi
ya NSSF akisisitiza kuwa shirika hilo limethibitisha kwa vitendo sifa ambazo shirika
hilo linazo na zimethibishwa. “Uongozi siyo kujisifia na kujisifu tu bali ni kutenda
vitendo na kufanya maamuzi yanayothibisha na kulingana na sifa hizo na katika hilo
NSSF imeonyesha njia.” Jengo hilo ambalo ujenzi wake ulianza Desemba 2011 na kuchukua
miaka mitatu limejengwa kwa pamoja na Kampuni ya Group Six International ya China
na Advent Construction ya hapa nchini na litakuwa na maduka makubwa na madogo, maofisi,
mabenki na kumbi za mikutano.
Akizungumza katika shughuli hiyo iliyohudhuriwa
na mamia ya wananchi na viongozi wa taasisi zilizoko katika ubia wa ujenzi wa Jengo
hilo, Waziri wa Kazi na Ajira, Mheshimiwa Gaudencia Kabaka amesema kuwa ni muhimu
kwa NSSF kuendelea kuwekeza katika miradi ya kimkakati na inayolipa, badala ya fedha
hizo kubakia kwenye mabenki tu ambako zinaweza kukumbwa na athari za mfumuko wa bei.
Mapema,
Rais Kikwete katika shughuli yake ya kwanza baada ya kuwasili Mkoani Kilimanjaro,
alifungua wodi ya upasuaji na kuweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa jengo la wodi
ya akinamama na mtoto katika Hospitali ya Mkoa ya Mawezi katikati ya Manispaa ya Moshi.
Mawenzi ni moja ya hospitali kongwe zaidi nchini ikiwa imeanzishwa mwaka 1920
Akizungumza
kabla ya kufanya shughuli hizo mbili kubwa, Rais Kikwete ameelezea mafanikio makubwa
yaliyopatikana katika utekelezaji wa Sera ya Afrika ya mwaka 2007 iliyochukua nafasi
ya sera ya mwaka 1997, ikiwa ni pamoja na kujenga maabara za kisasa katika kila hospitali
ya Mkoa nchini na kuzifanya hospitali hizo kuwa za rufani ndani ya mikoa.
Rais
Kikwete pia ameelezea jitihada za Serikali kupambana na magonjwa mbali mbali ikiwemo
malaria na ukimwi na juhudi za kupunguza vifo vya watoto na akinamama kwa sababu ambazo
zinazuilika. Aidha, Rais amefafanua hatua zilizochukuliwa na Serikali yake kuongeza
idadi ya madaktari na watumishi wengine wa sekta ya afya ambazo ni pamoja na ujenzi
wa vyuo vya kufundishia madaktari katika hospitali mbili kubwa na mpya za Mlongazila
na ile ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na upanuzi wa Chuo Kikuu cha Tiba cha Muhas
cha Dar es Salaam.
Rais Kikwete pia amezungumzia matatizo ya kudumaa kwa watoto
wadogo nchini akisema kuwa matunzo na lishe ya watoto wadogo katika siku 1,000 za
kwanza za maisha yake ni muhimu sana katika maisha ya baadaye ya watoto. Amesema kuwa
kwa watoto wadogo lishe duni inasababisha kudumaa kwa watoto, watoto kuwa na kimo
kidogo kuliko umri wao, watoto kuwa na uzito mdogo kulinganisha na umri wao, watoto
kuwa na upungufu wa madini joto na upungufu wa vitamin A.