Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani linaadhimisha Juma la Sita Kitaifa kuhusu Ndoa,
nafasi ya pekee kwa ajili ya kusherehekea tunu msingi za maisha ya ndoa na familia
na baraka inayobubujika katika maisha ya ndoa. Ni fursa kwa Mama Kanisa kuendelea
kuwasindikiza wanandoa katika maisha na utume wao, ili kuweza kukabiliana na changamoto
mbali mbali zinazojitokeza katika maisha yao.
Ni kilele cha upendo wa dhati
kati ya bwana na bibi wanaoshikamana hadi kifo kwa njia ya Sakramenti ya Ndoa Takatifu.
Kilele cha Juma hili ni hapo tarehe 14 Februari, maarufu kama Siku ya Wapendanao duniani!
Maadhimisho ya mwaka huu yana umuhimu wa pekee kwani hii ni sehemu ya maandalizi ya
maadhimisho ya Siku ya Familia Kimataifa itakayoadhimishwa Jimbo kuu la Philadelphia,
Marekani sanjari na Sinodi ya Maaskofu kuhusu Familia, itakayofanyika mjini Vatican,
mwezi Oktoba, 2015, kwa kuongozwa na mada "Wito na utume wa Familia ndani ya Kanisa
na Ulimwengu mamboleo".
Waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanaadhimisha
Juma hili kwa njia ya sala kwa kuwaombea wanandoa, siku ambayo imeadhimishwa nchini
Marekani Jumapili tarehe 8 Februari 2015. Maaskofu wamechapisha vitini vinavyoonesha
umuhimu wa maisha ya ndoa na familia katika maisha na utume wa Kanisa, changamoto
kwa waamini kujikita katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, ili kuwatangazia
walimwengu Injili ya Familia, kwa njia ya ushuhuda wa maisha.
Baraza la Maaskofu
Katoliki Marekani, limechagua tarehe 13 Februari 2015 kuwa ni Siku maalum ya kuombea
heshima na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia, kadiri ya mpango wa Mungu. Ni Siku
ya kufunga na kusali, ili kuomba toba na huruma ya Mungu kwa wanandoa, ili waweze
kudumu katika fadhila ya uaminifu hata pale wanapokabiliana na changamoto mbali mbali
za maisha. Wanandoa wasikate wala kukatishwa tamaa, bali waendelee kumtumainia Mungu
katika maisha yao ya kila siku. Kuna watu wamekwisha adhimisha Jubilee ya Miaka 50
ya Ndoa, kumbe, hili ni jambo linalowezekana kwa msaada na neema ya Mungu.
Na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.