Askofu mkuu Ignatius Ayau Kaigama, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria anasema
kwamba, wananchi wengi hawakufurahia na uamuzi uliofanywa na Tume Huru ya Uchaguzi
nchini Nigeria wa kuamua kuhairisha uchaguzi mkuu hadi tarehe 28 Machi 2015 kutokana
na sababu za kiusalama.
Uchaguzi mkuu nchini Nigeria ulikuwa umepangwa kufanyika
tarehe 14 Februari 2015. Wachunguzi wa mambo wanasema, kama Serikali imeshindwa kudhibiti
vitendo vya kigaidi vinavyofanywa na Kikundi cha Boko Haram, siku hizi chache, itakuwa
imepata wapi jeuri ya kulinda raia na mali zao?
Askofu mkuu Kaigama anatumaini
kwamba, uamuzi huu umefikiwa kwa ajili ya mafao ya wengi nchini Nigeria na kwamba,
Kanisa Katoliki nchini humo linaendelea kuwahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu
katika mchakato wa uchaguzi mkuu, kama sehemu ya utekelezaji wa haki yao msingi kikatiba.
Maaskofu wanawataka wananchi wote wa Nigeria kuzingatia: haki, amani, usalama
na utulivu ili kufanikisha zoezi la upigaji kura. Juhudi hizi zinakwenda sanjari na
majadiliano ya kidini kama sehemu ya mchakato wa kujenga na kukuza: haki, amani, umoja
na mshikamano wa kitaifa, lengo ni kuhakikisha kwamba, uchaguzi unakuwa huru na wa
haki; mambo msingi yatakayosaidia kuchochea maendeleo endelevu nchini Nigeria.
Na
Padre Richard A. Mjigwa. C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.