Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya 23 ya Wagonjwa Duniani inayoadhimishwa
na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 11 Februari, anawaalika waamini na watu wenye
mapenzi mema kuongozwa na hekima ya kiroho wanapowahudumia wagonjwa, kwa kujitoa bila
ya kujibakiza.
Kauli mbiu
ya maadhimisho haya ni “Nalikuwa macho kwa kipofu, nalikuwa mguu kwa aliyechechemea”.
Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kujisadaka kwa ajili ya wagonjwa, kwa
kutambua kwamba, wao pia wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Itakumbukwa kwamba,
Siku ya Wagonjwa Duniani ilianzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II yapata miaka ishirini
na mitatu iliyopita, ili kuwasaidia watu wanaojitolea maisha yao kwa ajili ya kuwahudumia
wagonjwa, waweze kutekeleza dhamana hii kwa unyofu.
Kwa namna ya pekee, Baba
Mtakatifu anawaalika waamini kufanya tafakari ya kina kutoka katika Kitabu cha Nabii
Ayubu, sura ya 29: 15, yaani “Nalikuwa macho kwa kipofu, nalikuwa mguu kwa aliyechechemea”
Muda ambao mtu anautumia kwa ajili ya huduma kwa mgonjwa ni muda mtakatifu, ni kielelezo
cha sifa kwa Mungu kwa ajili ya faraja kwa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano
wa Mungu pamoja na kukumbuka kwamba, Yesu alikuja hapa duniani si kwa ajili ya kutumikiwa
bali kutumikia na kutoa uhai wake ili uweze kuwa ni fidia ya wengi.
Ujumbe
wa Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya 23 ya Wagonjwa Duniani
anakazia kwa namna ya pekee hekima ya moyoni kwa ajili ya kuwasindikiza wagonjwa katika
shida, mateso na mahangaiko yao, wakati mwingine katika hali ya ukimya na kutokana
na uwepo huu wa karibu wanapata faraja na kujisikia kwamba, kweli wanapendwa na kuthaminiwa.
Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwa uchungu mkubwa aibu inayojificha kati ya watu
wanaotaka na kutafuta maisha bora kwa ud ina uvumba, kiasi hata cha kukumbatia utamaduni
wa kifo kwa kudhani kwamba, wagonjwa katika mateso na mahangaiko yao ya ndani hawana
sababu ya kuendelea kuishi.
Baba Mtakatifu anawataka waamini na watu wote wenye
mapenzi mema kujisadaka kwa ajili ya kuwasaidia wagonjwa, kwa kutenga muda maalum
wa kuwatembelea na kuwasaidia bila ya kuwa na haraka ya maisha na visingizio vya kazi
nyingi. Kwa kufanya hivi watu wanasahau umuhimu wa mtu kujisadaka kwa ajili ya jirani
zake, kama kielelezo makini cha imani tendaji, kwani Yesu anawakumbusha wafuasi wake
kwamba, yale yote waliyomtendea mmoja kati ya wadogo hao amemtendea yeye!
Baba
Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutoka katika ubinafsi
na undani wao, tayari kuwaendea jirani zao kama sehemu ya utekelezaji wa amri ya upendo
kwa Mungu na jirani, kanuni maadili na alama makini katika mang’amuzi ya maisha ya
kiroho, kwa kujisadaka kwa ajili ya wengine.
Baba Mtakatifu Francisko anaendelea
kusema kwamba, upendo hauna mipaka ya muda, hakuna mipaka ya kuwahudumia na kuwatembelea
wagonjwa. Lakini anaonya kwamba, watu wasifanye kama wale rafiki zake Ayubu waliokuwa
wanamtembelea, huku wakiwa na mwelekeo hasi juu ya maisha yake. Wao walidhani kwamba,
ugonjwa wake ilikuwa ni adhabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu kutokana na dhambi alizotenda.
Upendo wa kweli unajikita katika umoja na mshikamano bila kuhukumu wala kutaka
kumwongoa jirani, bali ni sehemu ya mchakato unaomkomboa mtu kutoka katika unafiki
wa kutaka kuonesha kwamba, anampenda jirani yake kwa matendo yake mema, kumbe ni kinyume
chake kabisa.
Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, mateso na mahangaiko
ya binadamu yanapata majibu kamili kutoka katika Fumbo la Msalaba wa Yesu, kielelezo
cha hali ya juu kabisa cha mshikamano kati ya Mungu na binadamu; sadaka ya hali juu
kabisa inayoonesha huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Hili ni jibu makini katika
shida na mahangaiko ya binadamu na hasa zaidi kwa watu wasiokuwa na hatia, chapa ya
kudumu katika Mwili wa Yesu Kristo Mfufuka; madonda yake matakatifu ni kashfa na ukweli
wa imani.
Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kusema kwamba, hata watu ambao
wanaishi katika Fumbo la Mateso na Mahangaiko, wakiyapokea mateso na mahangaiko haya
kwa imani na matumaini, wanaweza kuwa kweli ni mashuhuda hai wa imani inayofumbatwa
katika mateso na mahangaiko hayo, jambo ambalo haliwezi kueleweka kwa urahisi na akili
ya binadamu.
Baba Mtakatifu anawakumbuka Wakristo wengi wanaoendelea kushuhudia
imani yao si kwa maneno matupu, bali kwa njia ya maisha yao yanayofumbatwa katika
imani makini, ili kuwa kweli ni jicho kwa kipofu na miguu kwa mtu anayechechemea!
Hawa ndio wale watu wanaokaa pembeni mwa wagonjwa wanaohitaji msaada wa daima: ili
kuoga, kuvaa na kula chakula. Huduma hii hasa pale inapochukua muda mrefu inachosha
na kugeuka kuwa ngumu.
Baba Mtakatifu anasema ni rahisi sana kuweza kumhudumia
mgonjwa kwa siku chache, lakini kutoa huduma kwa mgonjwa kwa miezi au miaka na hasa
pale ambapo mgonjwa hawezi tena kutoa shukrani kwa huduma, yataka moyo na imani thabiti!
Baba Mtakatifu anasema, hii ndiyo hija ya utakatifu wa maisha!
Na Padre Richard
A. Mjigwa, C.PP.S Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.