2015-02-10 15:31:00

Mitandao ya kijamii!


Watumiaji wa teknolojia ya interneti nchini wametakiwa kutumia teknolojia hii kutafuta taarifa mbalimbali za maarifa na zenye mwelekeo wa kuleta maendeleo badala ya kutumia teknolojia hii kutafuta taarifa zisizo na faida na zenye mwelekeo wa kupotosha kizazi cha sasa kimaadili.

Wito huu umetolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na uhusiano wa Vodacom Tanzania, Rosalynn Mworia, katika siku ya matumizi ya interneti duniani iliyoadhimishwa leo duniani kote ambako alisema kuwa Vodacom kama kampuni ya mawasiliano siku zote itakuwa mstari wa mbele kuwaelimisha wananchi juu ya matumizi bora na sahihi ya mtandao wa interneti.

“Tukiwa kampuni inayoongoza kutoa huduma za mawasiliano nchini siku zote tutashirikiana na serikali na wadau wengine wa masuala ya mawasiliano kuhimiza matumizi bora na sahihi yamtandao wa internet.Matumizi ya intaneti yamekuwa siyo anasa tena kama ilivyokuwa ikichukuliwa na wengi hapo awali ambapo watu hujiunga kwa ajili ya kuwasiliana na watu walio nje ya nchi au kwa burudani nyinginezo. Hivi sasa utumiaji wa intaneti umekuwa kutoka watu kuwasiliaina mpaka kwa matumizi ya biashara ambapo watu wa mataifa mbali mbali hukutana mtandaoni kuuza ama kununua bidhaa na huduma,”.Alisema.

Mbali na biashara alisema kuwa interneti imejaa maarifa ya kielimu ya taaluma mbalimbali ambazo zinafanya dunia kuwa kijiji kimoja hivyo matumizi mazuri ya interneti yanaweza kumfanya mtu popote alipo kupata taarifa na maarifa ya fani anayohitaji au taarifa anazotaka kujua kwa haraka na kwenda na wakati na kuna vyuo vingi duniani vinatoa elimu kwa njia ya mtandao. “Inashangaza kuona baadhi ya watu hususani katika nchi zetu zinazoendelea wanatumia muda wao mwingi kuangalia taarifa zisizo na manufaa kwenye mitandao ya interneti”.Alisema.

Aliwaasa vijana wanaojiita wa kizazi cha Dot.Com hususani wanafunzi ambao wako mashuleni na vyuoni kuachana na kutumia muda wao kutafuta taarifa za kuwapotosha na zisizoendana na utamaduni wa kitanzania badala yake watumie teknolojia hii kupata maarifa na taarifa zenye manufaa kwao na kwa maisha yao ya baadaye.

Alimalizia kwa kuwahimiza watanzania kujiunga na mtandao wa Vodacom ambao hivi sasa unatoa huduma ya interneti yenye kasi kubwa na viwango vya gharama nafuu lengo kubwa likiwa ni kuhakikisha idadi ya watumiaji wa interneti nchini inaongezeka ili kwenda na nchi zilizopo katika ukanda wa Afrika Mashariki.

“Katika kuhakikisha lengo hii linatimia hivi karibuni tuliingiza kwenye soko simu za smartphone za gharama nafuu ambazo zimewalenga watu wenye vipato vya chini hususani wanaoishi maeneo ya vijijini na tuna imani watazipenda na kuzifurahia kwa kuwa mbali na kuwapatia interneti kwa gharama nafuu wakizinunua wanakuwa wameunganishwa na mitandao maarufu duniani kama vile Facebook, Whatsap, Twitter, Viber, Instagram na mingineyo”.Alisema.








All the contents on this site are copyrighted ©.