Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, tarehe 9 Februari 2015 imeadhimisha kumbu kumbu ya miaka
47 tangu ilipoanzishwa kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa na Kardinali Jaime
Lucas Ortega Alamino, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Havana, Cuba, kwenye Kanisa kuu
la Mtakatifu Yohane wa Laterano, Jimbo kuu la Roma.
Ibada hii imehudhuriwa
na waamini pamoja na viongozi mbali mbali wa Serikali na taasisi za kimataifa. Sala,
maskini na amani ni mambo makuu matatu yanayounda dira, mwelekeo na mikakati ya shughuli
za kitume zinazotekelezwa na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, sehemu mbali mbali za dunia.
Jumuiya hii ina jumla ya wanachama 60, 000 wanaotekeleza utume wao katika nchi 73
duniani, wote hawa ni watu wa kujitolea.
Jumuiya ya Mtakatifu Egidio imeendelea
kujielekeza zaidi na zaidi katika mchakato wa kutafuta suluhu ya amani katika maeneo
ambayo kwa sasa yanazidi kuwaka moto kutokana na vita na kinzani za kijamii na kisiasa.
Jumuiya hii pia ni shuhuda wa huduma ya upendo kwa maskini na wote wanaosukumizwa
pembezoni mwa jamii.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili
ya Radio Vatican.