Baba Mtakatifu Francisko amepokea taarifa ya msiba wa Kardinali Karl Joseph Becker
kutoka Shirika la Wayesuit, aliyefariki dunia, tarehe 10 Februari 2015 kwa majonzi
makubwa na amemtumia salam za rambi rambi Mheshimiwa Padre Adolfo NIcolàs Pachon,
Mkuu wa Shirika la Wayesuit, kwa kumkumbuka Kardinali Becker kwa sadaka na majitoleo
yake katika maisha na utume wa Kanisa.
Ni kiongozi alijipambanua kwa kuwafunda
vijana wa kizazi kipya, hususan mapadre katika tafiti za kitaalimungu pamoja na huduma
kwa Kanisa la Kiulimwengu. Baba Mtakatifu anamwomba Bikira Maria na kwa maombezi ya
Mtakatifu Inyasi wa Loyola, waweze kumwombea Marehemu Kardinali Becker, ili aweze
kupokelewa katika maisha ya uzima wa milele.
Kardinali Becker alizaliwa kunako
mwaka 1928, nchini Ujerumani, akajiunga na Shirika la Wayesuit akiwa na umri wa miaka
ishirini. Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi, akadrishwa kunako mwaka 1958.
Kwa miaka mingi amekuwa ni jaalim la Mafundisho tanzu ya Kanisa, huko Frankfurt na
katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian, kilichoko mjini Roma. Alikuwa ni mjumbe
wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa. Kunako tarehe 18 Februari 2012
aliteuliwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI kuwa Kardinali, amefariki dunia
akiwa na umri wa miaka 86.
Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican
anaungana na wote wanaoomboleza kifo cha kardinali Becker, aliyependwa na kuheshimiwa
sana na vijana wa kizazi kipya, kutokana na hekima na umahiri wake katika kufundisha;
anamwombea maisha ya uzima wa milele.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.