Baraza la Maaskofu Katoliki New Zealand, linawataka waamini kutolea ushuhuda wenye
mvuto na mashiko katika maisha ya ndoa na familia katika maeneno wanamoishi na kufanya
kazi, ili Watu wa Mataifa waguswe na ujumbe wa Injili ya Familia, inayotangazwa kwa
njia ya ushuhuda makini! Changamoto hii ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya
Sinodi ya Maaskofu kuhusu Familia, itakayoadhimishwa mjini Vatican, mwezi Oktoba 2015.
Baraza
la Maaskofu Katoliki New Zealand linasema kwamba, maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu
kuhusu familia ni matunda ya tafakari ya kina, sala, tafiti na mang'amuzi katika maisha
na utume wa Kanisa, ili kubainisha sera na mikakati ya shughuli za kichungaji zitakazowasaidia
wanandoa kutangaza Injili ya Familia kwa ari na moyo mkuu zaidi, licha ya changamoto
na magumu wanayokabiliana nayo kila siku ya maisha yao.
Maaskofu wanakumbushwa
kwamba, Sinodi maalum ya Maaskofu iliyofanyika mjini Vatican mwaka 2014, ilijielekeza
zaidi katika kupambanua mikakati, sera, dira na maelekeo ya shughuli za kichungaji
kwa ajili ya familia katika ulimwengu mamboleo. Kuna haja kwa waamini kuendelea kujikita
katika maboresho ya maisha ya ndoa na familia, kwa njia ya sala, tafakari, Sakramenti
za Kanisa; upendo na msamaha; mambo msingi katika udumifu kwenye ndoa. Kwa sasa waamini
wanaendelea kuhamasishwa ili kuchangia mawazo, tafakari na mang'amuzi yao, tayari
kupelekwa kwenye Sekretarieti kuu ya Sinodi, ili "Hati ya Kutendea Kazi" iweze kuandaliwa.
Baraza
la Maaskofu Katoliki New Zealand linawamasisha wanandoa kushiriki kikamilifu katika
maisha na utume wa Kanisa. Mwaliko huu unawaendea hata wale wanaodhani kwamba, Mama
Kanisa amewasahau katika maisha na utume wake kutokana na kasoro za maisha ya ndoa
na familia. Maaskofu wanawaalika wote hawa kushirikisha mawazo yao, kwani Mchungaji
mwema, anapenda kutembea na watoto wake wote, akitambua kwamba, kati yao kuna wale
wanaohitaji msaada zaidi.
Maaskofu wanawahimiza waamini kujibu maswali dodoso
kadiri ya hali na maisha yao ya ndoa na familia na wala si lazima kujibu maswali yote
yaliyoulizwa, kwani Mama Kanisa anapenda kusikiliza sauti ya mwamini mmoja mmoja,
ili hatimaye, kufahamu sauti ya Familia ya Mungu nchini New Zealand, kadiri ya mwanga
wa Roho Mtakatifu. Majibu yote ya maswali dodoso yanapaswa kuwa yamekwisha kusanywa
ifaikapo tarehe 14 Aprili 2015, tayari kwa maandalizi ya Hati ya kutendea kazi.
Na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.