2015-02-10 08:43:07

Binadamu si bidhaa!


Baraza la Maaskofu Katoliki Australia linawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kushikamana kwa dhati katika mapambano dhidi ya utumwa mamboleo na biashara haramu ya binadamu; mambo ambayo ni uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Itakumbukwa kwamba, kwa mara ya kwanza, Kanisa hapo tarehe 8 Februari 2015, katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya Mtakatifu Josefina Bhakita, mtawa wa Mabinti wa Canossa kutoka Sudan, aliyekombolewa kutoka utumwani na hatimaye kutangazwa na Papa Yohane Paulo II kunako mwaka 2000, limeadhimisha Siku ya kwanza ya kimataifa ya kupambana na biashara haramu ya binadamu.

Hii imekuwa ni fursa kwa ajili ya kusali, kutafakari na kuibua mbinu mkakati wa kupambana na biashara haramu ya binadamu. Baraza la Maaskofu Katoliki katika ujumbe wao kwa siku hii, wanasema, kamwe binadamu si bidhaa ya kuuzwa sokoni!

Biashara haramu ya binadamu inaendelea kushamiri sehemu mbali mbali za dunia kwa sababu watu wenyewe wameamua iendelee, lakini wakiamua kwa kauli moja, biashara haramu ya binadamu inaweza kukomeshwa na hivyo kuponya madonda makuu yanayowaandama watu zaidi ya millioni 27 kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Hawa ni wanawake, wasichana na watoto wanaonyimwa uhuru na utu wao unawekwa rehani, kiasi cha kugeuzwa kuwa kama bidhaa sokoni. Kutokana na watu hawa kudhalilishwa utu na heshima yao, kuna haja ya watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kupinga na hatimaye, kukomesha biashara haramu ya binadamu.

Baraza la Maaskofu Katoliki Australia, linaialika Jumuiya ya Kimataifa kushikamana kwa dhati, ili kuhakikisha kwamba, biashara haramu ya binadamu inapewa ufumbuzi wa kudumu. Bado kuna makundi makubwa ya wanawake, wasichana na watoto yanatumbukizwa katika utumwa mamboleo; baadhi ya watoto wanafanyishwa kazi za suluba kwenye mashamba makubwa na kwenye migodi; ni wazalishaji wakubwa viwandani na katika sekta ya uvuvi, lakini wanaishi na kufanya kazi katika mazingira duni na magumu. Hadi leo hii kuna wasichana 200 kutoka Nigeria walitekwa nyara na kikundi cha kigaidi cha Boko Haram hadi leo hii hawajulikani mahali walipofichwa.

Kumbe, kuna haja ya kuzuia uhalifu huu dhidi ya ubinadamu; kuwalinda wahanga, kuwashughulikia wahusika kadiri ya sheria na kushirikiana kwa ajili ya kufanya mabadiliko makubwa katika jamii. Hii ni changamoto kubwa inayowashirikisha watu wote kila mtu kadiri ya nafasi na dhamana yake katika jamii.

Tarehe 8 Februari 2015 ni siku ambayo ilichaguliwa na Baraza la Kipapa la haki na amani kwa kushirikiana na Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa wahamiaji, wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi maalum pamoja na Shirikisho la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, wameamua kwamba, kuanzia tarehe 8 Februari 2015, siku hii itakuwa inaadhimishwa na Kanisa lote ulimwenguni
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.