Mpendwa msikilizaji wa kipindi chetu pendevu sana cha Kanisa la nyumbani, Tumsifu
Yesu Kristo.
Tunakukaribisha
tuendelee kuchota hekima kutoka katika hazina ya mafundisho ya mtaguso Mkuu wa II
wa Vatican. Kukukumbusha tu ni kwamba, Mtaguso huu mkuu ulioitishwa na Mtakatifu Yohane
wa XXIII, ulikuwa na lengo la kufungua madirisha ili kuleta hewa mpya ndani Kanisa,
ili kuyapyaisha maisha na utume wa Kanisa. Ndiyo maana tutakuta kwamba, wazee wa Mtaguso
waligusa kila kona ya maisha ya Kanisa kwa undani wake.
Mpendwa msikilizaji
baada ya kulimwilisha tamko lile liliyohusu uzito wa malezi katika kipindi kilichopita,
leo tuitazame hati nyingine ambayo pia ni tamko kuhusu hadhi ya mwanadamu, kwa lugha
ya Kilatini inakijulikana kwa jina la Dignitatis humanae. Maudhui msingi ya Dignitatis
humanae ni juu ya Uhuru wa Dini. Kwa mantiki wazee wetu wa Mtaguso wanatazama Uhuru
katika mambo ya dini kama ni sehemu ya kuheshimu hadhi ya Mwanadamu.
Msingi
wa hadhi ya mwanadamu ni Mungu mwenyewe aliyependa kumwuumba mwanadamu kwa sura na
mfano wake. Hadhi na thamani ya Mwanadamu vipo katika asili yake babisa, siyo kitu
anachopewa na mtu yeyote yule. Ni Mungu amependa kumshirikisha mwanadamu umungu wake
na utakatifu wake. Na ndiyo maana mwanadamu safi, kwa msukumo wa kiu ya ndani ya roho,
daima hujibidisha kutafuta Muungano na Muumba wake.
Ndani ya Dignitates humanae,
wazee wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanatazama kwa kina udhahiri wa mwanadamu
na dini. Wakaaona kuwa dini sio kitu ambacho mtu hupewa, bali hutafuta kwa hekima
ya moyo. Dini siyo kitu ambacho mtu hulazimishwa kufuata, bali kwa hiari ya moyo wake
humtafuta na kumwelekea Muumba wake. Kwa mantiki hiyo, dini ni sehemu ya hadhi kabisa
ya Mwanadamu na hivyo kila moja anapaswa kuheshimiwa katika hadhi yake hiyo. Wanakaza
kusema, uhuru wa dini umejengwa katika maumbile ya mwanadamu mwenyewe. Siyo suala
la kihisia au la kiitikadi. Ni kwa mantiki hiyo linapaswa kutazamwa kwa uzito wa pekee.
Kwa
mawazo, mchanganuo, Dignitatis humanae inakazia juu ya haki ya mtu binafsi na ya
jumuiya pia ya kuwa na uhuru wa kijamii na wa kiserikali katika masuala ya dini. Historia
na nyakati zetu zinashuhudia jinsi ambavyo watu wananyanyaswa hata kudhulumiwa uhai
wao kwa kulazimishwa kufuata itikadi fulani za kidini. Jambo hilo liwe linafanywa
hadharani au kwa siri, au kwa propaganda ya aina yoyote ile linadhalilisha Hadhi ya
mwanadamu. Lakini katika tamko hili, Dignitatis humane, Hadhi ya mwanadamu, Wazee
wa Mtaguso wanaangazia pia suala la uhuru wajibifu. Kwa sababu sisi binadamu ni viumbe
jamii basi, uhuru wetu katika kufikiri, kupanga na kuamua lazima uheshimu mipaka,
uheshimu utu na uwepo wa wengine pia. Migogoro na migongano inakuja pale ambapo baadhi
wanatumia vibaya uhuru wao, huku wakikanyagakanyaga uhuru wa wengine. Kimsingi, hakuna
mtu mwenye uhuru wa kufanya kila kitu anachowaza na kutaka. Uhuru wetu uratibishwe
na heshima yetu kwa Mungu na kwa wanadamu wenzetu. Uhuru wetu utusaidie kutenda mambo
kwa manufaa ya wote.
Ikikazia mafaa ya wote Dignitatis humanae, hadhi ya mwanadamu
inakaza kusema, watu lazima waheshimu kanuni za kimaadili na uwajibikaji wa mtu binafsi
na wa kijamii. Katika kuzitumia haki binafsi ni lazima pia kujali haki za wengine.
Na hayo yote yaongozwe kwa dhamiri safi, hai na wajibifu mbele za Mungu na wanadamu.
Hadhi ya Mwanadamu, Uhuru na uwajibikaji makini wake ndiyo mambo msingi yanayoweza
kuchangia kwa kiasi kikubwa sana usitawi wa jumuiya ya watu, kiroho na kimwili.
Mpendwa
msikilizaji, Dignitatis humanae inakufuata hapohapo unapoishi na kufanya kazi. Inakukumbusha
kuwa wewe ni kiumbe huru wa Mungu, ishi kwa uhuru unaokusaidia kujenga na kulinda
thamani yako kama mwanadamu. Uhuru huo utusaidie kumtafuta Mungu, kumpenda na kumtumikia
kwa umakini zaidi katika nyanja mbalimbali za maisha yetu, tukianzia katika familia
zetu na maisha ya kawaida ya mahusiano jamii. Fundisho msingi hapa ni hili, kabla
hujamtendea lolote mwenzako, kwanza kabisa kumbua kuwa huyo ni binadamu.
Hadhi
ya ubinadamu wake itangulizwe mbele kabisa ili usije ukakosea, ukaunyanyasa utu wake
kwa kigezo cha upendo. Endapo wewe unataka mie nikusikilize na kutii tu vile unavosema
na kutaka, hapo unanishusha hadhi. Mimi ni mtu, na wewe mtu mwenzangu uwe tayari kunisikiliza.
Endapo wewe unataka mimi nikuheshimu tu, na wewe hutaki kuniheshimu, hapo ndugu yangu
unanipunguza thamani. Endapo wewe unajiona ni mwenye haki zaidi kuliko mimi, na haki
zako unazitetea hata kwa njia ya kukanyaga pua za sie wenzio, hapo unatupunguza thamani.
Hii ni moja ya kanuni inayosaidia kulinda hadhi ya mwanadamu, iwe ni katika
familia au popote pale tuishipo watu. Tuonane, tutambuane, tuthaminiane, tusaidiane,
tuelekezane kwa upendo, tuvumiliane, tuinuane, tushikane mikono – twende pamoja. Ni
hapo tu sote tutakuwa na furaha. Tusipunguzane thamani bwana! Thamani na hadhi yangu
sio mali yako ni ya Mungu. Unisaidie kuitunza hadhi yangu na mimi nitakutendea vivyo
hivyo kwa ajili ya heshima ya Mungu!
Yote hayo yajengwe katika uhuru wetu katika
Bwana, uhuru wa watoto wa Mungu. Kwa bahati mbaya kubwa sana, leo hii watu wengi wanafikiri
kuwa huru ni kumkimbia Mwenyezi Mungu, kuenenda katika njia zao peke yao huku wakiongozwa
na dhamiri butu na akili tundu zinazowapelekea katika harufu ya kifo cha mwili na
roho. Ndiyo maana tunajitendea na kutendeana matendo ya ajabu na wakati mwingine tunashetanishana
kabisa, huku tunasahau thamani na maana ya maisha yetu, tunapuuza thamani ya mwanadamu,
mwanadamu anageuzwa kuwa kitu tu cha kuburuzwa, kupuuzwa na kutendewa kikatiri kama
tunavyoshuhudia katika ulimwengu wetu leo.
Na kwa kujiweka mbali na Mungu,
tunaukosa ufunuo wa Kimungu wa kutusaidia kujua Mungu anataka nini kwetu. Badala yake
wapo wengi leo hii ambao wamegeuza dini kuwa ni kitega uchumi chao. Wataanzisha makundi
ya ibada, ili kukusanya pesa. Ikitokea hivyo, hadhi ya mwanadamu na heshima ya Mungu,
vyote huangamizwa. Dini siyo biashara, kubiasharisha dini ni kudhihaki heshima ya
Mungu!
Kwa mwangwi wa Dignitatis humanae, tukazie maarifa kusema kuanzi katika
malezi ya mwanzo kabisa mwanadamu afundishwe namna ya kutenda kwa kujiheshimu mwenyewe
na kuwaheshimu wenzake. Uhuru katika kutenda, uchochee zaidi thamani ya Mwanadamu.
Cheche za tamko hili, Dignitatis humanae, zitusaidie sana kukwepa kishawishi cha watu
wa nyakati zetu, ambao kwao uhuru wa mwanadamu ndiyo kigezo cha kuwa watenda maovu
hodari. Zipo hata taasisi zisizojali utu, ambao kwao matendo yao maovu na mifumo dhambi
wanaoiweka, wanaipa sura ya ‘haki ya binadamu’. Wanaunda na kuhalalisha mifumo-angamizi
kwa kudai kuwa hizo ni haki za binadamu. Kwa nini hivi? Kwa sababu tunatumia vibaya
uhuru wetu wa akili mwili na roho hadi tunasahau utu wetu.
Dignitatis humane
inatualika wewe na mimi, kusimama kidete kueleza, na kulinda thamani ya mwanadamu,
na kuhimiza matumizi ya uhuru wetu kwa manufaa ya wote, ni kwa namna hiyo tutachangia
zaidi katika kuienzi thamani ya mwanadamu.
Kutoka katika studio za Radio vatican,
ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.