Simameni kidete dhidi ya biashara haramu ya binadamu!
Washa mwanga dhidi ya biashara haramu ya binadamu ndiyo kauli mbiu ambayo imeongoza
maadhimisho ya Siku ya Kwanza Kimataifa ya kupambana na biashara haramu ya binadamu,
iliyofanyika, Jumapili tarehe 8 Februari 2015. Ni siku ambayo imeanzishwa na Baraza
la Kipapa la haki na amani, Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa ajili ya
wahamiaji, wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi maalum kwa kushirikiana na Shirikisho
la Kimataifa la Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume.
Kardinali Antonio
Maria Vegliò, Rais wa Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa ajili ya wahamiaji,
wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi anasema, Baba Mtakatifu Francisko anaendeleza
mapambano yaliyoanzishwa na watangulizi wake, ili kulinda na kutetea utu na heshima
ya binadamu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu dhidi ya uhalifu wa ubinadamu.
Biashara haramu ya binadamu ni janga la kimataifa, linalowahusisha watu zaidi ya millioni
21 kadiri ya takwimu zilizotolewa na Shirika la Kazi Duniani, ILO.
Hili ni
kundi la watu wanaofanyishwa kazi za suluba; wasichana, wanawake na watoto wanaotumbukizwa
katika biashara ya utumwa mamboleo; watu wanaonyofolewa viungo vyao kwa ajili ya kukidhi
soko la biashara ya viungo vya binadamu; baadhi yao ni watu wanaofanyishwa kazi za
majumbani kwa mishahara kiduchu na wakati mwingine wanajikuta wakilazimika kuingia
katika ndoa za shuruti.
Vitendo vyote hivi ni uhalifu dhidi ya ubinadamu kama
anavyosema Baba Mtakatifu Francisko na vinapaswa kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa,
kwa kuhakikisha kwamba, kila mtu anatekeleza dhamana na wajibu wake kikamilifu, ili
kweli biashara haramu ya binadamu iweze kukomeshwa na mwanadamu kuwa kweli huru. Ni
biashara ambayo inaendelea kupata faida kubwa sana duniani, ndiyo maana watu wasiokuwa
na dhamiri nyofu, kwa kuelemewa na uchu wa mali na madaraka, wamekuwa wakifumbia
macho janga hili katika maeneo yao ya kazi, kwa kukumbatia rushwa.
Kardinali
Vegliò anasema, biashara haramu ya binadamu ina uhusiano mkubwa na tatizo la wakimbizi
na wahamiaji, ambao wakati mwingine wanajikuta wakitumbukizwa katika mchezo huu mchafu,
kiasi hata cha kuhatarisha maisha yao. Haya ni maabara ya utengenezaji wa madanguro
ya biashara na utumwa wa ngono duniani. Watoto wasiokuwa na wazazi au walezi wao ni
rahisi sana kutumbukizwa katika majanga haya.
Ni wajibu wa vyombo vya ulinzi
na usalama kutambua makundi haya ya kijasusi na kuadhibiti kwa njia ya ushirikiano
wa kimataifa kwani hili ni tatizo sugu na kwamba, watu waambiwe kuhusu athari wanazoweza
kukutana nazo katika maisha yao. Kanisa litaendelea kuwahamasisha watu kutambua madhara
na athari za utumwa mamboleo pamoja na kuwasaidia waathirika kuanza tena ukurasa
mpya wa maisha yao, kwa imani na matumaini zaidi.
Viongozi wa Kanisa waendelee
kushirikisha na vyombo vya ulinzi na usalama katika kuwatambua wahalifu dhidi ya ubinadamu,
ili sheria iweze kushika mkondo wake. Mashirika mbali mbali ya Kanisa Katoliki yataendelea
kuhamasisha Jumuiya ya Kimataifa, ili kulivalia njuga tatizo la biashara haramu ya
binadamu, ili kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu.
Na Padre Richard
A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.