Papa Francisko kuhutubia Congress ya Marekani, 24 Septemba!
Familia ya Mungu Jimbo kuu la Washington, nchini Marekani limepokea kwa furaha na
bashasha kubwa taarifa inayosema kwamba, Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake
ya kitume nchini Marekani, mwezi Septemba, 2015, tarehe 24 Septemba, atahutubia Baraza
la Congresi la Marekani. Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro
kuhutubia wajumbe wa Congresi. Taarifa hii imetolewa na Mheshimiwa John Boehner.
Tukio hili la kihistoria utakuwa ni wakati wa furaha na neema na kwamba, Familia ya
Mungu nchini Marekani kwa sasa inasubiri kwa hamu na matumaini makubwa mpango mzima
wa hija ya kitume ya Baba Mtakatifu nchini Marekani, ili waweze kujipanga kikamilifu
kumpokea na kumkarimu mgeni huyu maalum anayeendea kukonga nyoyo za watu wengi kwa
njia ya ushuhuda wa maisha na utume wake. Itakumbukwa kwamba, Jimbo kuu la Washington
lina Wakatoliki zaidi ya 620, 000 wanaoishi katika Parokia 139. Jimbo linamiliki na
kuendesha shule 95 ndani ya Jiji la Washingtown DC na kwenye vitongoji vyake. Na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.