2015-02-09 14:50:46

Mikakati ya kuwalinda watoto!


Tume ya Kipapa kwa ajili ya ulinzi kwa watoto iliyokutana kwa mara ya kwanza tangu kuundwa kwake na Baba Mtakatifu Francisko, kuanzia tarehe 6 hadi tarehe 8 Februari, 2015, imemaliza mkutano wake kwa wajumbe kushirikishana uzoefu, ujuzi na mang'amuzi, ili kuweza kumsaidia Baba Mtakatifu katika kubainisha mikakati na kanuni za kuwalinda watoto wadogo ndani ya Kanisa.

Wajumbe kutoka katika makundi mbali mbali wameshirikisha taarifa ya taaluma waliyoifanyia kazi kwa miaka kadhaa iliyopita. Wajumbe wamekamilisha muundo wa tume na kutoa mapendekezo yatakayowasilishwa kwa Baba Mtakatifu kwa ajili ya uamuzi na utekelezaji zaidi. Wajumbe wataendelea kufanya tafiti na miradi mbali mbali mintarafu utume na dhamana waliyokabidhiwa na Kanisa, ili kweli watoto waweze kupata mazingira bora na salama.

Mkakati huu unapania pamoja na mambo mengine kutoa huduma za kichungaji kwa wahanga wa nyanyaso za kijinsia pamoja na familia zao; elimu, miongozo, majiundo makini kwa Wakleri na Watawa; sheria za Kanisa na kiraia kuhusu nyanyaso za kijinsia pamoja na wajibu wa viongozi wa Kanisa katika kukabiliana na tuhuma za nyanyaso za kijinsia. Uwajibikaji wa viongozi wa Kanisa ni muhimu sana, lakini wajibu huu unapaswa pia kutekelezwa Wakleri, Watawa na Walei wanaowahudumia watoto kadiri ya shughuli zao.

Kwa kuzingatia unyeti wa tatizo lenyewe, kuna haja kwa Kanisa katika ngazi mbali mbali kuwa na uelewa mpana zaidi, jambo ambalo linahitaji semina kama sehemu ya mchakato unaopania kuwajengea viongozi wa Kanisa kanuni na uelewa zaidi ili kuwalinda watoto wadogo. Tume inaandaa pia siku maalum ya kusali kwa ajili ya kuwaombea wahanga wa nyanyaso za kijinsia, ili watu watambue kwamba, kweli Kanisa linapania kuwalinda watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.