2015-02-09 09:16:43

Fumbo la mateso na mahangaiko ya mwanadamu!


Yesu Kristo alikuwa anatangaza uwepo wa Ufalme wa Mungu kati ya watu wake kwa njia ya mahubiri na uponyaji wa watu waliokuwa wanaelemewa na magonjwa ya kimwili na kuwaondolea dhambi zao. Alionesha upendeleo wa pekee kwa maskini, wadhambi, watu waliokuwa wameshikwa na pepo wachafu; wagonjwa na wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Yesu alijidhihirisha kuwa ni mganga wa roho na mwili; anayeokoa, anayetibu na kuponya.

Hii ni tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 8 Februari 2015. Baba Mtakatifu anasema, huu ndio mwelekeo wa maadhimisho ya Siku ya Wagonjwa Duniani, itakayoadhimishwa na Mama Kanisa hapo tarehe 11 Februari 2015 sanjari na Kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Lourdes. Jimbo kuu la Roma litafanya mkesha wa Siku hii hapo tarehe 10 Februari 2015 na Baba Mtakatifu anawapatia baraka zake za kitume, wale wote watakaoshiriki katika tukio hili la mshikamano wa upendo na wagonjwa.

Wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Baba Mtakatifu amewaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumwombea na kumsindikiza kwa njia ya sala Askofu mkuu Zygmund Zimowski, Rais wa Baraza la Kipapa la huduma kwa wafanyakazi katika sekta ya afya ambaye kwa sasa anaumwa sana na amelazwa nchini Poland. Yeye ndiye aliyekuwa ameandaa tukio la maadhimisho ya Siku ya Wagonjwa Duniani.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, utume wa uponyaji ulioanzishwa na Yesu Kristo unaendelezwa na Mama Kanisa, kama Sakramenti ya upendo na huruma ya Mungu. Wakristo wanatumwa kutangaza Injili na kuwaponya wagonjwa. Kanisa bado linaendelea kuwa aminifu kwa utume huu kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa wagonjwa kama njia ya kukutana na Yesu, kwani kwa njia ya tiba, ukarimu na huduma, Kanisa linamhudumia Yesu mwenyewe, kwani wagonjwa ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo.

Baba Mtakatifu anasema, licha ya maendeleo ya sayansi na teknolojia, lakini magonjwa ni mambo ambayo yanaacha maswali magumu yasiyokuwa na majibu. Kwanini kuna magonjwa, mateso na kifo? Baba Mtakatifu anasema, Kanisa linatoa majibu ya maswali haya magumu kwa mwanga wa imani, likiwa na picha ya Yesu Kristo mbele yake. Kristo anaonesha Fumbo la Ukombozi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ambaye aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanaye wa pekee; mwaliko kwa Wakristo kuwapelekea wagonjwa mwanga wa Neno la Mungu, bila kuwasahau wale wanaowahudumia na kuwatibu wagonjwa; ili huduma ya tiba kwa wagonjwa itekelezwe katika msingi wa ubinadamu, kwa njia ya ukarimu, upendo na huruma ya Kiinjili.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, alimkumbuka Mtakatifu Josefina Bakhita, Mtawa kutoka Sudan, aliyeonja suluba na nyanyaso za utumwa. Baba Mtakatifu anaungana na viongozi mbali mbali wa Kanisa katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Sala na Tafakari dhidi ya biashara haramu ya binadamu.

Baba Mtakatifu anapenda kuwatia shime wale wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya kuwasaidia, kuwahudumia na kuwalinda wahanga wa biashara haramu ya binadamu, ambayo kamwe haistahili kuonekana katika jamii iliyostaaribika, kwani huu ni uhalifu dhidi ya binadamu. Baba Mtakatifu anawaalika viongozi wa Serikali na wadau mbali mbali kujifunga kibwebwe ili kuhakikisha kwamba, utumwa mamboleo unaokomeshwa kutoka katika uso wa dunia.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.