2015-02-09 08:39:03

Ada ya shule isiwe ni kikwazo cha elimu!


Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linaonesha wasi wasi wake kutokana na kuongezeka kwa gharama ya elimu nchini humo, hali ambayo inatishia mchakato wa wananchi wengi kupata elimu bora kwa kiwango cha gharama wanachoweza kumudu, hata maskini na watu wenye kipato cha kawaida.

Ongezeko la ada kwa shule za Serikali kuna hatarisha kukwamisha juhudi za kuwapatia elimu watoto wote wa Kenya na kwamba, ni wajibu na jukumu la Serikali ya Kenya kuhakikisha kwamba, watoto wote wanapata elimu. Si haki watoto wa maskini kunyimwa haki ya kujipatia elimu kwa kukosa ada ya kulipia gharama za elimu nchini Kenya, wanasema Maaskofu.

Serikali iangalie namna ya kuwasaidia watoto wa maskini hata wao kupata elimu, kwa kuwashirikisha wadau mbali mbali ili kuangalia uwezekano wa kugharimia elimu kadiri ya gharama ya maisha ya wananchi wengi wa Kenya. Elimu ni wajibu wa wananchi wote wa Kenya, jambo ambalo pia linahitaji sheria makini, uwajibikaji, ukweli na uwazi, kwani ongezeko la gharama za elimu kutakwamisha utoaji wa elimu, kwani gharama ya maisha kwa sasa iko juu sana, wakati hali ya maisha ya wananchi wengi wa Kenya inaendelea kudidimia anasema Askofu Maurice Crwowley, Makamu mwenyekiti, Tume ya elimu na elimu ya dini, Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.