Ujumbe wa Kwaresima kutoka katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwa mwaka 2015
unaongozwa na kauli mbiu "Zingatieni haki na kutenda mema, (Isa 56:1)
UTANGULIZI:
Wapendwa Taifa la Mungu, “Neema na iwe kwenu, na amani zitokazo kwa Mungu,
Baba yetu” (Kol 1:2). Tunapoanza kipindi cha Kwaresima, kipindi cha toba na uongofu
wa nafsi zetu, “tujiandae kuruhusu nafsi zetu zitajirishwe kwa neema ya Ufufuko”.1
Maisha yote ya imani yetu yanatuelekeza katika tumaini la ufufuko. Katika kipindicha
Kwaresima, imani inaimarishwa, matumaini ya kweli yanafufuliwa, upendo ulioanza kuchakaa
unasafishwa na Pasaka ya milele inaandaliwa. Hiki ni kipindi ambacho Kanisa,kupitia
Neno la Mungu na mazoezi ya kiroho, linatukumbusha na kutuelekeza kurudi na kulielekea
lengo la juu kabisa la maisha yetu katika uhusiano mkamilifu na Mungu. Ukamilifu wa
uhusiano na Mungu, ambao kwao uhusiano wote wa binadamu unaratibiwa, unajengwa juu
ya msingi wa wemana haki. Ndio maana, katika maadhimisho ya Kwaresima ya mwaka huu,
sisi Maaskofu wenu, tunapenda kuungana nanabii Isaya tukiwahimiza na kusema: “Zingatieni
haki na kutenda mema” (Isa 56:1).
Kama jamii ya waamini, tumesimama mbele
ya wajibu wa maisha ambao unadai ukomavu na ujasiri wa kiimani. Wajibu huu ni wa kutenda
haki kwa nafsi zetu wenyewe, yaani;kuutafuta wokovu wetu, na kuwa wema kwa kuwatendea
jirani zetu wote haki kila tunaposaidiana na kuelekezana katika mambo yote yampendezayo
Mungu na kuijenga jamii.
Tafakari hii ya Kwaresima tunaileta kwenu ili
pamoja tuzipime njia na mienendo yetu ili kuona ni kwa kiasi gani tunazingatia haki
na kutenda mema mbele ya Mungu na mbele ya jamii. Ni kwa njia hiyo tu ndipo tunapoweza
kutambua ni kwa kiasi gani tumefanikiwa “kuidhihirisha harufu ya kumjua yeye kila
mahali kwa kazi yetu!” (2Kor 2:14). Kama bado hatujaanzakuzingatia misingi ya haki
na wema, hii ni fursa ya kuanza mara moja. Na Mungu atatuimarisha na kutuokoa kwani
yeyemwenyewe anatamka: “Ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jinalangu, watajinyenyekesha,
na kuomba, na kunitafuta uso, nakuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia kutoka mbinguni,
nakuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao” (2Nya 7:14).
SURA YA KWANZA
HAKI
1 Zingatieni haki na kutenda mema ninyi ambao mlioitwa
na Mungu na kukombolewa na Bwana Wetu Yesu Kristo mpate kufanywa wenye haki na kustahili
kupokea memayote ambayo Mungu amewaandalia watu wake. Ujumbehuu ulikuwa ni onyo kwa
viongozi wa Waisraeli wa kizazi kilichofuatia kile kilichotoka utumwani Babeli, kizazi
kilichokuwa na matumaini makubwa ya kuishi maisha huru na ya mafanikio ambayo kwa
bahati mbaya hawakuyapata kutokana na umaskini uliokithiri, manyanyaso na kusetwa
mikononi mwa wachache. Maneno haya ambayo Mwenyezi Mungu anayatamka kupitia kinywa
cha nabii Isaya ndio mwaliko ambao sisi Maaskofu wenu tunautoa kwenu Wanafamilia ya
Mungu ili kila mwamini ajichunguze na kupima mwenendowake katika kuzingatia haki na
kutenda mema. Msingi wa maisha yetu ni kumuonea Mungu kiu na kuishi katika njaa isiyokoma
ya kutenda mema kwa ajili ya Mungu.
2 Mungu ni haki. Na kila inapotokea mwanadamu
akatenda mema anakuwa ametenda haki. Haki ni “utashi wa kudumu wa kumpa Mungu na jirani
iliyo haki yao”.2 Mungu na jirani ni sehemu ya lazima katika safari ya maisha yetu.
Kuumbwa kwetu kwa sura na mfano waMungu (Mwa 1:26) kumetuweka chini ya wajibu wa kuwakielelezo
cha haki na wema wa Mungu katika maisha yetu. Tunapoutimiza wajibu huu adhimu Mungu
anaishibisha njaa yetu na kuponya kiu yetu (Mt 5:6). Kwa upendomkubwa Mungu aliiumba
dunia na vyote vilivyomo nakwa haki yake anatawala dunia na kuiongoza.
Ni
kwa wema na upendo mkubwa alimwumba mwanadamu na kumpa hadhi na heshima kubwa kati
ya viumbe vyake vyote. Hata pale mwanadamu alipomkosea muumbawake, Mungu alimwadhibu
kwa haki na kwa wema wake akaanzisha mpango mkubwa wa ukombozi. Mwenyezi Mungu aliendelea
kuonesha upendo, wema na haki yake kwa taifa teule kipindi chote cha mahangaiko utumwani
Misri na baadaye jangwani alipowaongoza wana waIsraeli kwa miaka 40.
Ni kwa
wema, upendo na haki yake aliwainua waamuzi na baadaye manabii wapate kuwaelekeza
watu wakena kwa mkono wa watawala aliwateua, aliwaongoza nakuwafanya taifa kubwa ingawa
mara nyingi walimwachana kumwasi. Utimilifu wa upendo na wema wa Mungukwa wanadamu
unaonekana katika nafsi ya Bwana wetu Yesu Kristo aliyesulubiwa ili wanadamu wapate
kuhesabiwa haki: “Kwa maana jinsi hii Mungualiupenda Ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe
pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee bali awe na uzima wa milele!” (Yn 3:16).
3. Kumjua Mungu ni kutenda haki (Yer 22:16). Ni katika huruma kuu na wema wake
Mungu, Neno alifanyika mwili na kukaa kwetu nasi tukauona utukufu wake, amejaa neema
na kweli. Katika maisha na utume wake Bwana Wetu Yesu Kristo alipita huko na huko
akitangaza habari njema kwa maneno na matendo yake. Kwa hotuba ya mlimani anatoa ufupisho
wa mafundisho yake; “heri walio maskini wa roho, maana ufalme wa mbinguni ni wao”
(Mt 5:3-11) na kwa maneno ya nabii Isaya anadhihirisha na kutoa dira ya utume wake;
“roho ya Bwana i juu yangu, kwa sababu Bwana amenitia mafuta,niwahubiri wanyenyekevu
Habari Njema. Amenituma ili kuwaganga waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka uhuru
wao, na na hao waliofungwa habari za kufunguliwa kwao” (Is 61:1). Kwa wema mkubwa
anaponya wagonjwa, anafufua wafu, analisha wenye njaa na kwa huruma kuu anasamehe
wenye dhambi. Ni katika mwanga wa haki ya kimungu Kristo anatetea wanyonge na kuwashutumumafarisayo
na walimu wa sheria.
4. Kanisa lililo chombo cha wokovu wa wanadamu linabidishwa
kupokea mwaliko wa kuzingatia haki nakutenda mema kama msingi wa utume wake kwa karne
zote. Kanisa linao wajibu wa msingi kabisa wa kulindana kutetea haki na kujibidisha
kwa huruma na ukarimu kuwatetea watu wote hasa wanyonge na waliosahaulika. Pamoja
na jukumu hili, Kanisa linatambua kuwa linapaswa kuongozwa na kutekeleza utume wake
kwa haki, upendo na ukarimu kwa wote. Ni katika mwanga huu jamii ya waamini katika
ujumla wake na hatamwamini mmoja mmoja anaalikwa kuzingatia haki na kutenda mema kwanza
kabla ya kutafuta haki na kudai kutendewa mema kama anavyofundisha Mt. Fransiskowa
Asizi katika sala yake: “Ee Bwana unifanye chombo cha amani yako, nieneze mapendo
palipo na chuki, walipokoseana nilete msamaha, nilete mwanga palipo na giza, nilete
furaha palipo na huzuni… Ee Bwana unijalienitamani zaidi kufariji kuliko kufarijiwa,
kufahamukuliko kufahamiwa, kupenda kuliko kupendwa”.
SURA YA PILI UKUU
WA HAKI NA TUNU ZAKE
1 Haki ni fadhila-tunu imwelekezayo mwanadamu na
jamii kumtendea Mungu muumba wa vitu vyoteitakiwavyo kwa Umungu wake na wanadamu wenyewekutendeana
ilivyo halali kwa hali zao. Katika haki zakijamii kunatakiwa pawepo taratibu na kanuni
za kujenga mahusiano mema ya kumstawisha kila mtu ndani ya jamii. Lakini, mara nyingi
haki inahatarishwa kwa mwelekeo wa kuweka mbele ubinafsi au upendeleo kwamakundi kwa
malengo ya kujinufaisha na kuwatengambali wengine na mafao yaliyo halali yao. Haki
ni zaidi yamikataba au misururu ya sheria na kanuni walizojiwekea wanadamu kukidhi
vionjo vyao. Haki sharti itokane na utu wa mwanadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano
wa Mungu. Haki ikiwemo na ikizingatiwa kwa dhatikatika jamii wanajamii huendesha mambo
yao kwa mshikamano, upendo na amani, maana bila haki hakuna amani.
2 Upendo
ni tunu ya kwanza ya haki. Palipo na upendolazima haki itawale na palipo na haki pia
upendo upo.Upendo ni wema unaovuka mipaka ya haki kwa ajili ya usitawi na furaha ya
wote. Ni tunu itupayo kipimocha kuthaminisha maadili mengine yote katika jamii. Wanajamii
wapendanao huwa huru na wa kweli wakitendeana kwa haki. Upendo hudhihirishwa kwamatendo
mema.
Uhuru ni tunda jingine la haki. Uhuru ni ishara ya heshima kuu ya utu
wa kila binadamu aliye sura na mfano wa Mugu akiwa na akili na utashi wa kulinda himaya
aliyodhaminiwa na Mungu. Binadamu kuwa huru hakumaanishi kujitenga na asili yake bali
ni kuishi katikamfungamano wa kujaliana kwa kila hali akiongozwa na ukweli na haki.
Kilele cha uhuru wa mtu ni uwezo wake wa kujiamulia kutenda mema yatukuzayo utu wake
na kumpa Mungu tukufu au kutenda maovu yadhalilishayo utu wake na kuiumiza jamii.
Matendo Mema kama ushuhuda wa imani.
7. Nyakati zetu, pengine
kuliko nyakati nyingine zote za maisha na utume wake, Kanisa linashuhudia hitaji kubwa
la maisha ya ushuhuda wa kiimani katika kutafuta haki na kutenda mema. Injili ya Kristo
imehubiriwa nakupokelewa na watu wengi katika maeneo mengi, lakini hatuoni uwiano
wa ongezeko la wanaomwamini Kristo na ongezeko la matendo mema, matendo ya huruma
na kukua kwa upatikanaji na utoaji wa haki. Ni dhahiri kuwakumwamini Kristo ni kushika
amri na maagizo yake; na agizo kuu analotupatia ni kupendana na kutendeana wema. Bwana
anatuonya na kutufundisha kwa manenona mifano mbalimbali kama mfano wa tajiri na maskiniLazaro
(Lk 16:19-31) na kama ilivyo pia kwa mfano wa hukumu ya mwisho -nalikua na njaa, ukanilisha,
nalikuwa uchi ukanivika, nalikuwa na kiu ukaninywesha,nalikuwa mgonjwa ukaja kunitazama,
nalikuwa mgeniukanikaribisha, nalikuwa kifungoni ukanijia (Mt 25:31¬46). Yakobo Mtume
anasisitiza na kutuasa kwa maneno mazito: “Ndugu zangu kuna faida gani mtu kusema
ana imani, lakini haoneshi kwa vitendo? Tuseme kaka au dada hana nguo na chakula,
yafaa kitu gani kuwaambia hao: ‘Nendeni salama mkaote moto na kushiba,’ bila kuwapa
mahitaji yao ya maisha? Vivyo hivyo imani bila matendo imekufa” (Yak 2:14-17). Tunawasihi
na kuwaalika wanafamilia ya Mungu, kujali na kuwasaidia wahitaji na kuzingatia haki
katika nyanja zote kuanzia katika familiazetu zilizo Kanisa dogo.
8. Pamoja
na ukweli kwamba leo hii tunashuhudia ongezekola watu, makundi ya watu na taasisi
zinazojishughulishana kuwasaidia wahitaji, lakini pia tunashuhudia wengiwa watu hao
na taasisi hizo zikiwatumia wahitajiili kujinufaisha wao zaidi ya walengwa. Upendo
kwa masikini haupatani na ubinafsi unaopelekeakujilimbikizia mali au matumizi yake
ya choyo: “Haya basi, enyi matajiri! Lieni, mkapige yowe kwa sababuya mashaka yenu
yanayowajia. Mali zenu zimeoza, namavazi yenu yameliwa na nondo. Dhahabu yenu na mali
yenu zimeingia kutu, na kutu yake imewashuhudia, nayo itaila miili yenu kama moto”
(Yak 5:1-3).
9. Ubinafsi na uchoyo uliokithiri unaathiri sana jamii yetu ya
kitanzania kiasi cha kubadili hata mifumo ya kiutendaji ili kuwalinda wachache wenye
mali na nguvu ya madaraka. Mwelekeo huu umeshusha thamani ya utuna kupumbaza fikra
za wengi kiasi cha kuelekea kuamini kuwa bila mali na madaraka thamani ya mtu hushuka
nakudidimia. Dhana hii imezaa hatari kubwa kwani utajiri, mali na madaraka vyaelekea
kumeza malengo makuu yamaisha ya mwanadamu wa leo.
10. Kwa kujibidisha kutenda
kazi za huruma, mwamini anakuwa ameonesha kwa matendo kile anachokiishi na kukiamini
na kutoa ushuhuda wa imani yake. Kwa kazi na matendo ya huruma tunamsaidia jirani
katika shida zake kiroho na kimwili. Matendo hayo ni pamoja na kufundisha, kushauri,
kutuliza, kufariji, kusamehe nakusikiliza kwa utulivu (matendo ya huruma ya kiroho
). Pamoja na hayo, yapo pia matendo ya huruma ya kimwili ambayo ni pamoja na kuwalisha
wenye njaa, kuwasitiriwasio na nyumba, kuwavika walio uchi, kuwatembeleawagonjwa na
wafungwa na kuwazika wafu. Roho yenye kuzingatia haki na kutenda matendo mema ni kama
taa iliyojaa mafuta ambayo hung’aa na kuangaza tayari kumlaki Bwana siku ya mwisho,
bali roho isiyopambwa na matendo mema ni kama taa isiyo na mafuta ambayoimefifia na
haiangazi (Mt 25:1-13).
11. Tunapoalikwa kuzingatia haki na kutenda mema,
wakati huohuo, tunaalikwa kutafuta upatanisho kati yetu naMuumba na kati yetu sisi
wenyewe kwa kuwa tayarikusamehe na kuomba msamaha pale tulipokosea. Nidhahiri kuwa
Mungu ndiye asili na chimbuko la msamaha na kwamba ni vigumu kwa hulka yake, binadamu
kuwezakusamehe kirahisi. Familia nyingi zinasambaratika kutokana na wanandoa kushindwa
kutoa au kupokea msamaha. Kusamehe ni kutenda wema na kuzingatiahaki. Tusipokuwa tayari
kuwasamehe walio tukosea, tunajifungia milango ya kupokea msamaha wa dhambizetu kutoka
kwa Mungu mwenyezi. Mioyo yetu imekuwa migumu ikijitwika chuki, kinyongo na roho ya
kisasi kwa waliotukosea japo kuwa hata sisi wenyewe si wenye haki mbele ya Mungu.
SURA YA TATU MATUKIO YA KIKANISA
Sinodi ya Familia
12. Tukiwa bado tunakumbukumbu hai ya Sinodi ya Familia iliyofanyika
mwishoni mwa mwaka jana huko Roma,tunapata nafasi ya kuendelea kutafakari na kujifunza
juu ya chimbuko, asili na malengo ya familia kadiri ya mpango wa Mungu. Tunatambua
kuwa familia hupata utambulisho na dhima yake katika mpango wa Mungu wauumbaji na
ukombozi ikielekezwa juu ya kile inachowezakufanya na inachopaswa kutenda.3 Kila familia
inapaswakutambua ndani mwake wito wake ambao hauwezi kupuuzwa, na ambao ni heshima
na haki yake na wajibu wake mkuu. Tunapaswa kukumbuka daima kuwa, “mustakabali wa
Kanisa na ubinadamu unazaliwa na kukua katika familia”.4 Kwa uelewa huo tunazialika
familia kurudi daima kwenye lengo la mwanzo na la asili ya familia kama lilivyoratibiwa
na Mungu. Hii ni fursa yakujifahamu na ya kuufahamu wito na utume wa familiaambao
unapaswa kuwa dira ya kuongoza safari ya familia za kikristo zilizo msingi wa Kanisa
lililo Familia hasa yaMungu.
13. Katika mpango wa Mungu familia ni jumuiya
mwandani ya uhai na upendo ikiwa na dhima ya kudumisha uhai na upendo hadi kuufikia
ukamilifu wake kama wote walioumbwa na kukombolewa wanavyotakiwakujitahidi. Familia
ndiyo “hekalu la uhai wa binadamu” na chembe hai ya jamii, Kanisa na nchi yetu. Katika
familia, baba, mama na watoto hujifunza mambo yote ya msingi kama kuheshimiana, kupendana,
kusaidiana nakuwajibikiana.
Humo wote hubaini pia sura ya Mungu na iwapo mafunzo
yote hayo yanakosekana, jamii nzimahuteseka kwa ukatili huo na huwa chimbuko la ziada
yaukatili. Kila mfumo wa jamii unawajibu wa kuhakikisha familia zinawezeshwa kuendelea
kuwa muhimili wa maisha bora na endelevu kiuchumi na kimaadili. Hata hivyo, jamii
inawajibu wa kutambua kuwa familia ina haki zake ambazo hakuna anayeweza kuinyang’anya
kwani zimetoka kwa Mungu mwenyewe. Ni katikafamilia mtoto anaweza kupata haki zake
zote za mwilina roho na uhai wake kulindwa. Familia kama taasisi ya msingi kabisa
inapaswa kulindwa ikianzia kulinda uhai wa wanafamilia toka kutungwa mimba mpaka kifo
cha kawaida. Pasipo familia taifa halitakuwepo! Hata hivyo, familia zinapita katika
kipindi kigumusana. Katika familia, ndiko tunakokuta manyanyaso na dhuluma kubwa wanazofanyiana
wanafamilia pasipo udhibiti wowote.
Utamaduni wa uonevu haswakwa watoto na
wanawake unajenga tabia za ukatili nauhalifu sugu katika familia kama taasisi asilia.
Katika mazingira haya ni lazima tusimame na kuitetea taasisi ya familia kama ilivyoratibiwa
katika mpango wa Mungu.Familia hujenga jumuiya ya watu, huhudumia uhai wawanajumuia
na kupokea uhai mpya; ni mshirika mkuu wa kwanza wa maendeleo na ustawi wa jamii na
mhusika mkuu katika dhima za Serikali na Kanisa. Kwa hiyo ni wajibu wa kila mmoja
kuilinda familia. Mwaka huu pia, Kanisa litaendelea kutafakari nafasi na dhima ya
familia katika Sinodi ya Kawaida ya Maaskofu itakayofanyikaRoma mwezi Oktoba 2015.
Huu ni mwaliko wa kuzidi kujizamisha katika tafakari na mikakati ya kujenga na kulinda
familia zetu ili nazo ziilinde na kuijenga jamii.
Mwaka wa Watawa
14. Baba Mtakatifu Fransisko ameutangaza mwaka huu Novemba 2014 – Februari
2016 kuwa Mwaka wa Watawa. Sisi Kanisa la Tanzania tumeupokea mwaliko huu kwa moyo
wa shukrani tukitambua mchango mkubwa wa watawa katika utume wa Kanisa. Wapendwa watawa
“twamshukuru Mungu sikuzote kwa ajili yenu nyote… Wala hatuachi kuikumbuka kazi yenu
ya imani, na taabu yenu ya upendo, na saburi yenu ya tumaini lililo katika Bwana wetu
Yesu Kristo” (1 Thes 1: 1-5). Katika mwaka huu tungependa kuwahimiza watawa kurudi
katika roho ya karama ya mashirika yenu. Litakuwa jambo la hatarikubwa kama shirika
la kitawa litapoteza njia na kuiacharoho ya karama ya shirika. Mwaka huu uwe wa tafakari
kwenu na kipindi cha kurudi daima kwenye chemchemi za maisha ya kikristo na za roho
ya mwanzoni ya mashirika yenu.Tunapenda pia kuwahimiza mfanye bidii katika utume wenu
ili mlipambe Kanisa, nalo limdhihirishe Kristo,“kwa waamini na wasioamini”,6 huku
mkimpeleka na kumfikisha Kristo kwa watu.
15. Watawa kimsingi wanafanya kazi
katika Kanisa mahalia. Uhusiano wa mashirika na uongozi wa majimbo naounapaswa uzidi
kuboreshwa, ili huduma na utume wa Kanisa uzidi kuimarika.7 Utambuzi na umuhimu wa
mashirika ya kitawa kutenda shughuli ndani ya jimboyakiwa yameunganika na uongozi
wa Kanisa mahali ni wa kuzingatia sana.
16. Mwaka huu pia unapaswa kuwa fursa
ya kutathiminina kuona ni kwa jinsi gani miito ya utawa inavyokua. Ni vema kuendelea
kuhimiza miito. Namna ya kwanzaya kuhimiza miito iwe ni kwa mfano wa maisha yetu.Maisha
ya kielelezo na ya kujitoa ni ya muhimu na hiindio namna bora ya kuufanya wito wa
utawa uchanue nakupendwa. Vijana wakivutiwa kuingia utawa kwa sababu nyingine yoyote
zaidi ya kumfanya Kristo apendwe naKanisa liendelee kutimiza wito wake, basi lengo
lote la maisha ya utawa litapotea.
SURA YA NNE WAJIBU WA KIJAMII
WA KANISA
17. “Wito wa binadamu ni kudhihirisha sura ya Mungu”.8 Kanisa
linazingatia wazo hili katika roho ya utume wake. Ni kwa sababu hii, Kanisa haliwezi
kufumbia macho wajibu wake katika kuchangia makuzi ya jamii na kuhimiza “unyofu wa
mwenendo”.9 Himizo la kuzingatia haki na kutenda mema, ni himizo linalolitaka Kanisa
lijihusishe na jamii. “Mimi ni mwanadamu, hakuna suala linalomuhusu mwanadamu yeyote
ambalo halinihusu”.10 Kila mara Kanisa linapotimiza wajibu huu linashutumiwa kuingilia
siasa. Tafsiri hiyo ni potofu. Swali la kujiuliza ni hili kwamba, “siasa ni nini?”.
Kama siasa ni mfumo wa maisha unaowahusu watu, Kanisa haliwezi kukaa pembeni. Kanisa
likikaa pembeni litatenda dhambi ya kutotimiza wajibu kwa jamii. Kwani, “furaha na
matumaini, uchungu na fadhaa ya wanadamu wa nyakati zetu, hasa ya maskini na wale
wote wanaoteswa yote ni furaha na matumaini, uchungu na fadhaa ya wafuasiwa Kristo
pia. Wala hakuna jambo lililo na hali halisi ya kibinadamu lisiloigusa mioyo yao”.11
Ni vema tuzidi kuwakumbusha wanakanisa kuwa wajibu wa kutetea nakulinda haki ni sehemu
ya uinjilishaji na umisionari wa Kanisa. Hivyo basi, tusiruhusu kupokonywa furaha
ya uinjilishaji na ari ya umisionari huu.
18. Dhana ya kudai kwamba Kanisa
linaingilia siasa palelinapokosoa mifumo mibovu ya jamii ni upotoshajiwa makusudi.
Hata hivyo, Kanisa Katoliki lingependa kutamka wazi kuwa wakati waamini wake wana
vyama vyao vya siasa, Kanisa Katoliki halina wala halifungamanina chama chochote cha
siasa. Kanisa linafungamana nabinadamu katika hali zake zote, njema na ngumu na lina
wajibu wa kinabii wa kuwa “sauti ya wasiokuwa na sauti”. Baba wa Taifa, Mwalimu Julius
Nyerere aliwahi kuliasa Kanisa akisema: “Hutokea wakati mwingine kwambawahanga wa
umasikini na kusetwa waamuapo kuanza kutenda kama watu wenye akili timamu na utashi
na kudhubutu kukabiliana na vikwazo vya umasikini na manyanyaso, wawakilishi wa Kanisa
hujiengua na kujifanya waangalizi tu. Kanisa sharti likubali kwamba maendeleo ya watu
humaanisha maasi dhidi ya udhalimu. Iwapo Kanisa halitashiriki kwa vitendo katika
maasi dhidi ya mifumo dhalimu ya kiuchumi inayosababisha watu kutoswa katika fedheha
ya umaskini na kudhalilishwa, Kanisa halitakuwa na maana yoyote kwa watu na dini ya
kikristo itapoteza mvuto na kuwa kamaushirikina ikikubaliwa kwa uoga tu. Iwapo Kanisa,
waamini wake na asasi zake, halitadhihirisha upendo wa Mungu kwa watu kwa kushirikiana
na watu na kwa kuwaongoza katika kupinga kiungwana maovu wanayotendewa na wadhalimu,
basi litahusishwa na utesaji wa watu wote na kutokuwa na haki kwao. Jambo hili likitokea,
Kanisa litakufa, na kwa kufikiri kibinadamu linastahili kufa”.13
19. Safari
ya Taifa letu katika wakati wetu sasa ni safari inayopitia katika mkanganyiko mkubwa
wa kutokujitambua na inayokosa utashi wa dhati wa kuijenga jamii inayokua katika misingi
ya haki. Hii ni kwa sababu zipo dalili lukuki za kukosekana kwa uadilifu na dhamiri
safi. “Hadhi ya binadamu yadokeza na kudai unyofu wa dhamiri adilifu. Dhamiri adilifu
ni pamoja na kutambua misingi ya uadilifu”.14 Na kimsingi, “kadiri dhamiri inavyozidi
kuwa nyofu, ndivyo watu na vikundivinavyozidi kujitenga na uamuzi kipofu na kujaribu
(kuishi) kulingana na sheria halisi za uadilifu”.15
20. Kuinjilisha ni kuufanya
uwepo wa Mungu ujidhihirishekatika ulimwengu wetu.16 Mungu, katika Kristo hamkomboi
mtu mmoja mmoja tu, bali pia mahusiano ya kijamii baina ya watu.17 Ndio maana, katika
moyo wa Injili tunaona uhusiano wa kina kati ya uinjilishaji na maendeleo ya mwanadamu.18
Tusiruhusu kupokonywa furaha ya uinjilishaji na umisionari huu.
Mchakato
wa Katiba mpya
21. Taifa letu linapita katika kipindi cha mchakato
wa Katiba mpya. Tunarudia kusisitiza kuwa hiki ni kipindi adhimu kwa Taifa letu. Tunapenda
kulikumbusha Taifa letu kwamba hili ni zoezi linalodai uadilifu mkubwa na utashi wa
kisiasa wenye lengo la kujenga Taifa kwa muda mrefu. Kejeli, vitisho, migomo, vijembe
na kukosa ustahimilivu katika mijadala yenye kulenga kuunda misingi ya mustakabali
mwema wa Taifa letu vinaonesha kukosekana kwa uzalendo na ukomavu wa kisiasa. Mchakato
wa marekebisho ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania usiwe chimbuko na chanzo
cha kubomoa mema mengi yaliyokwisha kufikiwa kwa amani, uhuru, udugu na haki. Ikumbukwe
kwamba Katiba ni Mwongozo Mkuu na kiunganishi cha msingi chajamii yetu ya Tanzania.
Katiba mpya inapaswa kutujenga katika utamaduni na maisha mapya yatakayotokana
na mila na desturi za makabila zaidi ya 130 kwa kujengamisingi mipya iliyosheheni
dira mpya, miiko ya uongozi, haki, wajibu na uwajibikaji chini yake au kwa mujibu
washeria, kanuni, mila, desturi na mapokeo ya jamii. Kwa nguvu ya katiba bora sisi
sote Watanzania wa Bara na Visiwani tutaweza kuheshimiana kiadilifu, siyo kinafiki;
na jumuiya ya kisiasa na wengine wote walio na mamlaka na nyadhifa za kiutawala na
kiuongozi kuwajibikakidemokrasi.
Uchaguzi mkuu 2015
22.
Mwaka huu wa 2015 ni mwaka wa Uchaguzi Mkuunchini Tanzania. Tutakuwa tunakabiliwa
na uamuzi wa kisiasa kwa kuchagua viongozi watakaotumia rasilimaliza taifa letu kwa
ama ustawi na maendeleo ya wengiwalio katika lindi la umaskini au kwa matumizi ya
faharizao binafsi na wabia wao katika kujitajirisha. Tunashauri zoezi hili liendeshwe
kwa uadilifu na lisifanywe kuwatendo la ulanguzi wa kura. Huku ni kudhalilisha utu
wawatu na kuvuna madaraka kupitia umasikini wa watu.Tunapenda wale wanaoomba dhamana
ya uongoziwa Taifa hili katika nyanja zote na sisi sote tunaotumia haki ya kura zetu
tuitumie fursa hii kama dhamana na tendo la heshima ya utu wetu. Matukio haya ya makuzi
ya jamii yetu yasidhoofishe amani yetu. Katika yote tunawahimiza; zingatieni haki
na kutenda mema, mkitenda yote kwa moyo huru unaoongozwa na dhamiri safi.
Hitimisho
23. Wapendwa Taifa la Mungu, sisi Maaskofu wenu tunawatakieni kila baraka
katika safari hii ya imani.Tumwombe Mungu aithibitishe Imani yetu nayoijidhihirishe
katika maisha na matendo yetu ya kila siku katika kuzingatia haki na kutenda mema.
Ni sisi Maaskofu wenu, 1. Mhashamu Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa Rais wa
Balaza la Maaskofu Tanzania, Iringa 2. Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo - Dar
es Salaam 3. Mhashamu Askofu Mkuu Josaphat Lebulu - Arusha 4. Mhashamu Askofu
Mkuu Paul Ruzoka - Tabora 5. Mhashamu Askofu Mkuu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi OfmCap
– Mwanza 6. Mhashamu Askofu Mkuu Damian Dallu - Songea 7. Mhashamu Askofu
Mkuu Beatus Kinyaiya - Ofm Cap - Dodoma 8. Mhashamu Askofu Mkuu Jude Thaddaeus
Ruwa’ichi OfmCap – Ap. Adm Shinyanga 9. Mhashamu Askofu Telesphor Mkude - Morogoro
10. Mhashamu Askofu Gabriel Mmole - Mtwara 11. Mhashamu Askofu Bruno Ngonyani
- Lindi 12. Mhashamu Askofu Anthony Banzi - Tanga 13. Mhashamu Askofu Agapiti
Ndorobo - Mahenge 14. Mhashamu Askofu Evaristo Chengula, IMC - Mbeya 15. Mhashamu
Askofu Augustino Shao, CSSp - Zanzibar 16. Mhashamu Askofu Damian Kyaruzi - Sumbawanga
17. Mhashamu Askofu Severine NiweMugizi - Rulenge-Ngara 18. Mhashamu Askofu
Desiderius Rwoma - Bukoba 19. Mhashamu Askofu Desiderius Rwoma – Ap. Adm Singida
20. Mhashamu Askofu Method Kilaini, Askofu Msaidizi - Bukoba 21. Mhashamu
Askofu Ludovick Minde, ALCP/OSS -Kahama 22. Mhashamu Askofu Alfred Leonard Maluma
- Njombe 23. Mhashamu Askofu Castor Paul Msemwa - Tunduru-Masasi 24. Mhashamu
Askofu Michael Msonganzila - Musoma 25. Mhashamu Askofu Issack Amani - Moshi 26.
Mhashamu Askofu Almachius Rweyongeza - Kayanga 27. Mhashamu Askofu Rogath Kimaryo
CSSp - Same 28. Mhashamu Askofu Salutaris Libena - Ifakara 29. Mhashamu Askofu
Eusebius Nzigilwa, Askofu Msaidizi -Dar es Salaam 30. Mhashamu Askofu Renatus
Nkwande - Bunda 31. Mhashamu Askofu Gervas Nyaisonga - Mpanda 32. Mhashamu
Askofu Bernadin Mfumbusa – Kondoa 33. Mhashamu Askofu John Ndimbo – Mbinga 34.
Mhashamu Askofu Titus Mdoe, Askofu Msaidizi – Dar es Salaam 35. Mhashamu Askofu
Renatus Nkwande – Ap. Adm Geita 36. Mhashamu Askofu Joseph Mlola ALCP/OSS - Kigoma
37. Mhashamu Askofu Prosper Lyimo, Askofu Msaidizi -Arusha.