Tamaduni za wanawake: usawa na utofauti ndiyo kauli mbiu iliyokuwa inaongoza mkutano
mkuu wa Baraza la Kipapa la Utamaduni, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa wanawake
ili kushiriki kikamilifu katika kuchangia tafakari hii, ili kuwajengea uwezo wanawake
ili kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa na wala wasijisikie kuwa
ni "watu wa kuja tu". Hii ni changamoto kubwa kwa wanawake wenyewe, waamini walei
na viongozi wa Kanisa katika ngazi mbali mbali za maisha na utume wa Kanisa.
Baba
Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwa wajumbe wa Baraza la Kipapa la Utamaduni,
alipokutana nao Jumamosi, tarehe 7 Februari 2015 amekazia mambo makuu manne yanayopaswa
kufanyiwa kazi na Kanisa katika tamaduni mbali mbali, ili kukuza majadiliano na waamini
wa dini mbali mbali kuhusu nafasi na dhamana ya wanawake katika jamii: Uwiano mzuri,
uwezo wa kuzaa; mwili wa mwanamke kati ya tamaduni na bayolojia; wanawake na dini;
Je, wanashiriki katika maisha na utume wa Kanisa?
Kwanza kabisa, Baba Mtakatifu
Francisko anasema kuna haja ya kutambua kwamba, kuna usawa na utofauti, kama kielelezo
makini kinachotafuta uwiano mzuri unaojikita katika mahusiano dhidi ya utamaduni wa
mfumo dume unaoendelea kumkandamiza mwanamke. Kuna haja ya kuvuka kishawishi cha kudhani
kwamba, wote ni sawa sawa, kwa kushindwa kutambua tofauti, katika utambulisho wa mtu
na asili kwani mwanamke na mwanaume wanakamilishana.
Pili, Baba Mtakatifu anasema,
uwezo wa mwanamke kuzaa ni kanuni na utambulisho maalum kwa wanawake ambao wamejaliwa
uwezo wa kuendeleza zawadi ya maisha, kwa kuilinda na kuidumisha. Kanisa linapenda
kuwapongeza wanawake kwa mchango wao katika medani mbali mbali za maisha ya mwandamu;
kwani wamekuwa mstari wa mbele katika masuala ya elimu na majiundo; shughuli na mikakati
mbali mbali ya kichungaji na kwamba, wanawake wanaonesha sura ya huruma ya Mungu kwa
binadamu. Ni watu wanaojisadaka kwa njia ya huduma, kwa kuonesha ukarimu, kimsingi,
wanawake ni sawa na tumbo la Kanisa linalopokea na kuzaa maisha.
Tatu, Baba
Mtakatifu anajaribu kuangalia mwili wa mwanamke kati ya tamaduni na bayolojia, kwa
kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu amemkirimia mwanamke mwili unaopendeza, lakini pia
umesheheni madonda ambayo wakati mwingine yamesababishwa na dhuluma pamoja na nyanyaso.
Mwili wa mwanamke ni kielelezo cha maisha, lakini kwa bahati mbaya, unaharibiwa hata
na wale ambao walipaswa kuwalinda na kuwasindikiza katika maisha!
Kuna mifumo
mbali mbali ya utumwa mamboleo, biashara ya ngono na vitendo vya ukeketaji; mambo
ambayo Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuyavalia njuga, ili kusitisha vitendo vinavyodhalilisha
utu na heshima ya wanawake duniani, kiasi cha kuwageuza kuwa kama bidhaa inayouzwa
sokoni, bila kusahau umaskini unaosababisha wanawake wengi kuishi katika mazingira
magumu na hatarishi; kiasi hata cha kunyanyaswa, kielelezo cha utamaduni usiojali
wala kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya wengine.
Nne, Baba Mtakatifu
anapopembua kuhusu wanawake na dini: mwelekeo wa kutafuta ushiriki katika maisha na
utume wa Kanisa anakiri kwamba, kuna haja kwa Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, anatoa
fursa zaidi kwa wanawake kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kutambua
kwamba, wanawake wanashiriki kwa ukamilifu zaidi katika utekelezaji wa dira na mikakati
ya shughuli za kichungaji ndani na nje ya Kanisa.
Wanawake ni wadau wakuu
katika kukoleza na kudumisha tunu msingi za maisha ya kifamilia, ni watu wenye utajiri
mkubwa, wanaoweza kusaidia upatikanaji wa amani na utulivu; wito na utume maalum kwa
wanawake. Ziwepo juhudi za makusudi ili kuwahamasisha wanawake kushiriki katika maisha
ya hadhara, katika medani mbali mbali za maisha: mahali panapotolewa maamuzi na utekelezaji
wa mikakati na sera mbali mbali; kwa kutoa kipaumbele cha pekee katika maisha ya kifamilia.
Wanawake wasaidiwe kufanya maamuzi machungu katika maisha, kwa kuwajibika barabara
katika jamii na katika maisha na utume wa Kanisa.
Na Padre Richard A. Mjigwa,
C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.