Tarehe 8 Februari, 2015 imewekwa kuwa siku ya sala na uhamasishaji kimataifa kuhusu
swala la biashara haramu ya watumwa. Baraza la Kipapa la haki na amani kwa kushirikiana
na umoja wa Wakuu wa mashirika ya kitawa ulimwenguni, wanawaalika Wanakanisa ulimwenguni
kote kusali na kuhamasisha jamii juu ya tatizo sugu la utumiaji wa watu kama vyombo
vya kujipatia mapato.
Tarehe 8
Februari kila mwaka ni sikukuu ya Mtakatifu Josephine Bakhita, huyu alikuwa mtumwa
kutoka Darfur, Sudan ambaye alipowekwa huru akawa mtawa wa Masista wa Kanosa, na
alitangazwa kuwa mtakatifu mwaka 2000 Papa Yohane Paulo II.
Lengo la siku
hii ni kuhamasisha jamii na kusali ili haki za watu wanaotumiwa kama vyombo vya kujipatia
mapato ziweze kutambuliwa na bihashara hii haramu iweze kukomeshwa. Papa Francisko
katika Barua yake ya Kipapa Evangelii Gaudium anakumbusha kwamba bihashara ya binadamu
inaathiri jamii zote ulimwenguni. “Ni kwa jinsi gani ningetamani watu wote tusikie
sauti ya Mungu inayotuuliza: “Ndugu yako yuko wapi?” (Mw. 4:9).
Huyo ndugu
yako anayefanywa mtumwa yuko wapi? Huyo kaka au dada yako anayeuzwa kwenye ukahaba
yuko wapi? Huyo kaka au dada yako anayetumiwa na baadaye kuachwa afe kwenye maghala
ya viwanda au kwenye mashamba, yuko wapi? Watoto wanaolazimishwa kuwa ombomba kwa
ajili mapato ya watu wasio na dhamiri si tunawaona? Sasa kwanini tunajifanya hatuoni?
Swala hili linatuhusu sisi wote.”
Watu wote, hasa wakatoliki popote waliko,
katika majimbo yote ulimwenguni tukusanyike na kusali, tujitahidi kutoa mchago wetu
ili watu hawa ambao hakuna anayetetea haki zao waweze kuona mwanga wa matumaini. Sisi
wote hatuna budi kujitahidi kuchukua hatua madhubuti ili kukomesha kila sababisho
la aina hii ya utumwa. Takwimu kuhusu tatizo hili zatuonyesha kuwa biashara hii inawahusisha
watu takriban milioni 21, wengi wao wakiwa watu maskini wa kila rika na jinsia, wakimbizi,
yatima wasio na ulinzi wowote.
Kadiri ya utafiti uliofanya na David Pegg mwaka
jana (4 Juni, 2014) unaonyesha mambo ishirini na tano yanayosababisha kubaki mdomo
wazi mbele ya hali hii ya biashara haramu ya watu:
Mwaka 2013, bei ya mtumwa
mmoja ilikuwa wastani wa Dola za Marekani kati ya 90-100. Katika sehemu nyingi ulimwenguni
80% ya biashara ya binadamu ilihusisha ngono na 20% zilizobaki zilihusisha kutumikishwa
katika kazi viwandani na mashambani. Mwaka 2013 idadi ya watumwa ulimwenguni ilikuwa
kati ya milioni 20-30. Kati ya hao, takriban watu milioni moja walisafirishwa kuvuka
mipaka toka nchi moja kwenda nyingine kimagendo. Asilimia 5. 70% ya hao walikuwa ni
watumwa wa kike. 6. 50% ya hao walikuwa ni watoto.
Biashara ya watu ni ya tatu
kwa ukubwa wa mapato ikifuatia mdawa ya kulevywa na biashara ya silaha. Biashara ya
watu inazalisha takriban bilioni 33 kila mwaka na nusu ya mapato hayo hutoka kwenye
nchi zilizoendelea kiviwanda. Hata katika biashara ya nguvu kazi, wanawake bado ni
nusu ya idadi ya watu wanaouzwa utumwani.
Biashara ya viungo vya binadamu ni
moja shughuli zinazoongezeka siku hadi siku hata kama hutajwa kwa nadra sana katika
vyombo vya habari. Takriban watu 30,000 ya waathirika katika biashara ya ukahaba hupoteza
maisha kila mwaka kwa ajili ya majeraha, magonjwa ya kuambukizwa na kwa kutelelezwa.
Asilimia 80% ya watu wanaouzwa katika utumwa wa kingono wana umri wa chini ya miaka
24 na baadhi yao ni watoto ambao hawajafikia umrti wa miaka sita.
Mtuhumiwa
katika biashara ya watu Ludwig “Tarzan” Fainberg aliyehukumiwa hivi katibuni anabaini
kuwa: “Unaweza kumnunua mwanamke kwa Dola 10,000 za kimarekani na kurudisha mtaji
wako ndani ya muda wa wiki moja; na baada ya hapo kila upatacho ni faida tu ikiwa
mwanamke mwenyewe ni mrembo na bado kijana.” Kadiri ya utafiti uliofanywa nchini Uholanzi
mwaka 2003, mtumwa wa ngono humletea mmiliki wake pato la kiasi cha Dola za kimarekani
250,000 kila mwaka. Mfanya biashara wa watumwa wa ngono aweza kupata faida mara ishirini
kwa kila msichana aliyemnunua, ili mradi hakusababishiwa majeraha yanayoharibu urembo
wake.
Kati ya matokeo ya kumalizika kwa vita baridi kati ya magharibi na mashariki
ni kuongezeka kwa makundi ya waasi katika sehemu mbalimbali za dunia na makundi hayo
kutumia watoto katika mapambano kati yao. Kadiri ya utafiti uliofanywa na mwandishi
wa habari wa gazeti la Times uliofanyika mwaka 2009, kundi la Taliban limekuwa likiwatumia
watoto wadogo walio na umri wa chini ya miaka saba katika mashambulio ya kujitolea
mhanga.
Bei ya mtoto wa kujilipua inafikia kati ya Dola za kimarekani 7,000-14,000.
Shirika la UNICEF linakadiria kwamba kiasi cha watoto 300,000 walio chini ya umri
wa miaka kumi na nane wanatumika katika mapigano katika sehemu mbalimbali za dunia.
Watoto wadogo wanauzwa katika soko la kimagendo na mapato ya biashara hiyo hugawiwa
kati ya wafanya biashara, madaktari, wanasheria, maafisa wa uhamiaji na wengineo.
Watafiti
mbalimbali wamebaini kuwa kadiri hali mbaya ya uchumi inavyozidisha makali yake ulimwenguni,
bishara haramu ya watu inazidi kuongezeka. Biashara haramu ya watu ni kati ya shughuli
za kijangili zinazoongezeka kwa kasi kuliko zote ulimwenguni. Makundi ya wafanya biashara
haramu wanavutwa kufanya biashara ya watu kwa sababu mtu anaweza kuuzwa mara nyingi
kuliko bidhaa nyingine yoyote.
Kuna idadi kubwa ya watumwa ulimwenguni leo
hii kuliko wakati mwingine wowote wa historia ya binadamu. Mnamo mwaka 2013 wafanya
biashara ya watu walipata kipato cha Dola za Marekani bilioni 32 na kuwapiku makampuni
ya Nike, Google, Starbucks kwa pamoja.
Kama vile Masista Wakanosa walivyofaulu
kumfanya Mtakatifu Josephine Bakhita aweze kubadili mtazamo na maana ya neno “Bwana”,
kutoka katika hali ya kuwaelewa mabwana wa utumwa na kuona upendo usio mipaka wa Bwana
wa mabwana; hata sisi katika siku hii ya sala hatuna budi kujitahidi kwa kila tuwezalo
kubadili hali za mamilioni ya watu wanaoishi katika hali ya utumwa na kuwasaidia waweze
kuona wanapendwa na kujali utu wao.
Katika ujumbe wake wa siku ya kuombea Amani
Duniani mwaka huu 2015, Papa Fracisko amependa uwe na kichwa cha habari kifuatacho:
“Toka sasa Utumwa uwe mwiko: sisi wote ni ndugu.” – “No longer Slaves but brothers
and sisters”. Basi sisi wote tuunganishe nguvu na kuhakikisha kuwa hali hii ya utumwa
inakoma na siku hadi siku jamii itambue kuwa ni mwiko kumfanya binadamu mwenzetu kuwa
mtu na bidhaa ya kujipatia mapato.
“Ee Mungu, tunaposikia habari za watoto
na watu wazima wakidanganywa na kupelekwa kwenye maeneo yasiyojulikana kwa madhumuni
ya unyanyasaji wa kingono, wakilazimishwa kufanya kazi na viungo vyao vya mwili kutumiwa
kama vyombo vya kujipatia mapato,mioyo yetu inajaa huzuni na roho zetu kuwa na hasira
kwani utu wao na haki zao zapuuzwa kwa njia za ulag’ai, vitisho na nguvu. Twainua
sauti zetu tukilaani tabia hii na biashara hii ya utumwa wa kisasa. Kwa maombezi ya
Mt. Josefina Bakhita kizazi chetu kiweze kuona mwisho wa biashara hii haramu. Tupe
hekima na ujasiri wa kusimama pamoja na wale ambao miili, mioyo na roho zao zimejeruhiwa,
ili kwa pamoja tuweze kufanya kweli ahadi yako kwa kuwajaza hao ndugu zetu upendo
utokao kwako. Hao maharamia wakashindwe na kurudi mikono mitupu wakatubu kutoka katika
njia zao ovu. Tusaidie nasi tuweze kuwa vyombo vya uhuru ambao ni zawadi itokayo kwako
kwa ajili ya wana wako. Amina.”
Na Padre Felix Mushobozi, C.PP.S. Afisa
kutoka Shirikisho la Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, Italia.