2015-02-07 08:06:25

Mshikamano na wagonjwa!


Askofu mkuu Andrè Gueye wa Jimbo kuu la Dakar, Senegal anasema, Familia ya Mungu Jimboni humo inajiandaa kwa udi na uvumba kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya 35 ya Wagonjwa Jimboni humo kwa njia ya Novena itakayoanza kunako tarehe 7 hadi tarehe 14 Februari na tarehe 15 itakuwa ni siku maalum kwa ajili ya wagonjwa, wazee na walemavu, itakayoadhimishwa kwenye madhabahu ya Bikira Maria wa Popenguine. RealAudioMP3
Maadhimisho haya yanaongozwa na kauli mbiu “Nilikuwa ni jicho kwa kipofu na mguu kwa kiwete”, maneno ambayo ni sehemu ya ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Siku ya Wogonjwa Duniani inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 11 Februari, sanjari na Kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Lourdes.
Madhabahu ya Popenguine ni kielelezo cha upatanisho miongoni mwa watu na chemchemi ya majadiliano ya kidini, kwani katika maadhimisho haya, limekuwa ni jambo la kawaida waamini wa dini mbali mbali kushiriki pia, ili kuomba neema na baraka kutoka kwa Bikira Maria katika shida na mahangaiko yao ya ndani.
Hiki ni kipindi ambacho Jimbo kuu la Dakar, Senegal linapenda kuonesha kwa namna ya pekee mshikamano wa dhati na wazee, wagonjwa na walemavu, kwa kuwaonjesha upendo na huruma inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.
Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya Wagonjwa Duniani anakumbusha kwamba, muda ambao watu wanautumia kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa, wazee na walemavu ni muda wa neema na baraka, chachu ya maisha ya utakatifu, kwa kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani, kwa kuwajalia Yesu Kristo aliyekuja si kwa ajili ya kuhudumiwa bali kuhudumia na kuyamimina maisha yake kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.
Baba Mtakatifu Francisko anakemea tabia ya baadhi ya watu kutaka kupata ubora wa maisha kwa gharama zote, kiasi hata cha kuwabeza wazee, wagonjwa na walemavu kwamba, hawana sababu ya kuishi. Haya ni mawazo yanayokumbatia utamaduni wa kifo, kwa kutema Injili ya Uhai, ambayo Mama Kanisa anapenda kuwatangazia walimwengu kwa ari na moyo mkuu.
Wagonjwa na watu wote wanaopambana na magumu katika maisha yao, wanaweza kupokea na kuikumbatia zawadi ya imani na kuendelea kuwa kweli ni mashuhuda hai wa imani, kwani akili ya binadamu haiwezi kutambua fika kuhusu Fumbo la mateso na mahangaiko ya binadamu. Hapa kunahitajika imani na kumwachia Mungu ili mapenzi yake yaweze kufanyika, jambo ambalo si rahisi kwa mtu asiyekuwa na imani.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.