Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM, ni matunda
ya Mtaguso mkuu wa Piliwa Vatican kama sehemu ya mchakato wa Mama Kanisa kukabiliana
na changamoto mbali mbali zinazojitokeza katika maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika,
kwa kuwa na sauti moja sanjari na kuendelea kuwa chombo cha wokovu, amani, majadiliano
na upatanisho.
Ili kutekeleza dhamana na wajibu huu, SECAM haina budi kuwa
aminifu kwa utambulisho wake kama kielelezo hai cha umoja na huduma hasa miongoni
mwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hapa viongozi wa Kanisa hawana
budi kuwa makini katika maisha na utume wao, na kamwe wasimezwe na malimwengu, bali
kwa kuendelea kushirikiana na kwa karibu zaidi na Balozi za Vatican zilizoko Barani
Afrika pamoja na kudumisha umoja na mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro, ili
kushirikishana uzoefu na mang'amuzi ya kikanisa na shughuli za kichungaji, daima Kanisa
likijitahidi kuwa karibu na watu!
Ni changamoto na wosia unaotolewa na Baba
Mtakatifu Francisko kwa Viongozi wakuu wa SECAM, alipokutana na kuzungumza nao, Jumamosi,
tarehe 7 Februari 2015 mjini Vatican, baada ya kuhitimisha mkutano wa SECAM uliokuwa
unafanyika mjini Vatican. Vijana wa kizazi kipya anasema Baba Mtakatifu wanahitaji
ushuhuda, changamoto ya kutoshikamana sana na mambo ya utajiri, mali, madaraka, mafanikio
na misimamo mikali ya kidini.
Ili kuwasaidia vijana Barani Afrika kuwa na
matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi kuna haja ya kuwekeza katika sekta ya elimu,
ili kuwajengea watu nidhamu, haki, amani na utulivu; kwa kutoa kipaumbele cha kwanza
kwa tunu msingi za maisha na utu wema. Mchakato wa maboresho katika sekta ya elimu,
hauna budi kwenda sanjari na mikakati makini ya shughuli za kichungaji kwa vijana,
ili waweze kuwa ni mashuhuda amini wa Injili ya Kristo.
Baba Mtakatifu Francisko
anasema kwamba, kuna mambo mengi yanayochangia kuporomoka kwa tunu msingi za maisha
ya ndoa na familia, lakini inapaswa kukumbukwa kwamba, Familia ni chemchemi ya udugu
na msingi wa amani; changamoto kwa Kanisa Barani Afrika kuendelea kuwekeza katika
Injili ya Uhai, kwa kuwasaidia wagonjwa, walemavu, wazee pamoja na kuzijengea uwezo
familia ili ziweze kukabiliana na dhamana yake barabara.
Kanisa Barani Afrika
limeendelea kuwa kweli ni shuhuda wa upendo unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha,
kwa Wakristo kujisadaka kwa ajili ya jirani zao katika medani mbali mbali za maisha.
Baba Mtakatifu anaipongeza na kuishukuru Familia ya Mungu Barani Afrika kwa kuonesha
mshikamano wa upendo na udugu wakati wa kukabiliana na janga la Ebola, ambalo limekuwa
kweli ni tishio kwa maisha na maendeleo ya watu wengi Barani Afrika. Kanisa liendelee
kuwekeza kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii pamoja na kuamsha
dhamiri za viongozi wa kisiasa na kijamii, ili waweze nao kuchangia katika maboresho
ya maisha ya watu wao.
Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza Wamissionari
wa Mashirika mbali mbali ya kitawa na kazi za kitume yanayotekeleza utume wake Barani
Afrika. SECAM ni chombo cha sheria, ili kusaidia kuponya madonda ya rushwa na ufisadi,
ili kukoleza mchakato wa kutafuta na kukumbatia mafao ya wengi. Ikumbukwe kwamba,
Uinjilishaji ni dhamana na wajibu wa kila Mkristo, ili iweze kuenea na kuwafikia watu
wengi zaidi. Uinjilishaji unajikita katika toba na wongofu wa ndani, tayari kuiamini
Injili; dhamana inayopaswa kutekelezwa na Jumuiya nzima ya waamini, ili kuimarisha
imani na mapendo.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili
ya Radio Vatican.