Wakurugenzi wakuu wa Mashirika ya Kipapa ya Kazi za Kimissionari kutoka Afrika ya
Kati, kuanzia tarehe 9 hadi tarehe 15 Februari 2015 watafanya mkutano wao utakaoongozwa
na kauli mbiu "Utume na familia: changamoto za kichungaji". Mkutano huu hufanyika
kila baada ya miaka miwili, ili kuweka mbinu na mikakati ya shughuli za kichungaji
kwa ajili ya Mashirika ya Kipapa ya Kazi za Kimissionari.
Hii itakuwa ni fursa
kwa wajumbe kuweza kubadilishana mawazo, changamoto na matarajio yao katika maisha
na utume wa Kanisa mintarafu tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Tafakari hizi
ni mwendelezo wa maadhimisho ya awamu ya kwanza ya Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili
ya Familia sanjari na maandalizi ya mwendelezo wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu
kuhusu familia, itakayofanyika mjini Vatican, mwezi Oktoba 2015, kwa kuongozwa na
kauli mbiu "Wito na utume wa Familia ndani ya Kanisa na Ulimwengu mamboleo".
Padre
Gaspard Mengata, Mkurugenzi mkuu wa Mashirika ya Kipapa ya Kazi za Kimissionari kutoka
Baraza la Maaskofu Katoliki Cameroon anasema kwamba, kuna haja kwa Kanisa mahalia
kupembua na kupyaisha mikakati na shughuli za kimissionari kwa Makanisa mahalia.
Ratiba
inaonesha kwamba, wajumbe pamoja na mambo mengine, watajadili kuhusu utume kwa Mashirika
ya Kitawa; Familia kadiri ya Mpango wa Mungu na uelewa wake mintarafu mila na desturi
njema za Kiafrika; mchakato wa Uinjilishaji wa Familia, ili familia ziweze Kuinjilisha
walimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha. Mkutano huu utahudhuriwa pia na Padre Ryszard
Szmydki, Katibu mkuu wa Mashirika ya Uinjilishaji wa Watu.
Kuna Wamissionari
wengi wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika
na kati yao, kuna wale wanaomimina maisha yao katika huduma. Itakumbukwa kwamba, kwa
mwaka 2014 kuna Wamissionari na Watawa 7 waliopoteza maisha yao Barani Afrika: Watawa
3 wameuwawa kikatili nchini Burundi, kuna Mapadre wawili ambao wamepotea na hadi sasa
hawajulikani mahali walipo huko Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati; Mtawa mmoja alitekwa
nyara na hatimaye kuuwawa kikatili Afrika ya Kusini na mwishoni, kuna Mtawa mmoja
aliyeuwawa kikatili katika tukio la ujambazi Dar Es Salaam, nchini Tanzania.
Na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.