Ndugu mpendwa, tukumbuke kuwa katika sehemu hii ya maandiko, yaani sehemu hii ya Neno
la Mungu toka injili ya Marko, swali kubwa toka kwa watu waliokuwa wanamsikiliza ni
kuwa Yesu ni nani? Domenika iliyopita tumeona wasiwasi huo toka kwa Wayahudi. Leo
swali elekezi ni kuwa Yesu alikuja kufanya nini?
Katika neno la Mungu siku
ya leo, twaona mambo mengi yakifanywa na Bwana. Tumeweza kuona pia jinsi siku ya Yesu
ilivyo, yaani mpango kazi wake kwa siku na utekelezaji wake. Alipotoka katika Sinagogi
– alienda nyumbani kwa mkwewe Petro, anaponya, watu wanamletea wagonjwa, anawaponya,
anajitenga kwa ajili ya sala na baadaye anafundisha kuhusu ufalme wa Mungu. Huu ndiyo
mpango kazi wa Yesu kwa siku.
Jambo kuu na la msingi ni kuwa Yesu alikuja
kutangaza kwanza habari njema za ufalme wa mbinguni. Ni vizuri nasi pia leo tukatafari
kuhusu hilo. Amekuja kutangaza habari njema kwa maskini – Lk. 4:18-19 –Roho wa Bwana
yu juu yangu, kwa maana amenipaka mafuta niwahubirie maskini habari njema. Amenituma
kuwatangazia wafunga kufunguliwa, vipofu kuona tena, kuwaletea wafungwa uhuru, na
kutangaza mwaka uliokubalika kwa Bwana.
Hapa twapata jibu kwa nini Yesu asubuhi
ile, katika somo la injili – hata baada ya kuambiwa kuna umati mkubwa, aliwaagiza
wanafunzi wake waondoke, waende miji jirani, kuhubiri habari njema pia huko. Katika
Barua Evangelii Nuntiandi, Papa Paulo VI – anasema wazi – uinjilishaji kwa hakika
ni neema na wito kabisa wa kanisa, ndiyo utambulisho wa kanisa. Somo la pili la leo
latupatia msingi wa somo letu la Injili la leo – kuinjilisha ni sawa na kupumua. Uinjilishaji
ndiyo pumzi ya kanisa.
Namna hii ya ufahamu unatuchanganya wengi wetu. Yaani
ni upi hasa utume wa Yesu? Hapo juu tunapata jibu. Kwamba kwanza Yesu amekuja kutangaza
ufalme wa Mungu. Mengine yote hutokana na hilo. Hebui tuongeze majibu zaidi ili kusaidia
ufahamu huu. Katika Mt. 6:33 – tunaendelea kupata majibu – Basi tafuteni kwanza ufalme
wa Mungu na uadilifu wake, na hayo yote mtaongezewa.
Lengo la Yesu kuutangaza
ufalme wa Mungu ni kutoa nafasi kwa wanaoamini, watawaliwe na roho ya Mungu kwanza.
Mahangaiko yetu katika sura ya dhambi, utengano, magonjwa, mateso n.k yanaingia katika
hali yetu ya udhaifu. Tukielewa vizuri mapenzi yake Mungu, haya yote yataponywa na
tutajikuta katika hali ya kupokea neema na baraka yake Mungu. Tatizo ni kuwa tunataka
kutatua matatizo yetu kadiri tunavyofikiria sisi. Sisi tunataka kumweka punda nyuma
ya mkokoteni. Wakati kazi ya punda ni kuvuta mkokoteni.
Lile kundi lililokuja
asubuhi ile ni aina ya watu tuliona nao sasa. Walimtafuta Yesu kwa ajili ya shida
zao tu. Na ndivyo tunavyoishi imani yetu. Angalia kwa mfano mahudhurio yetu katika
ibada na shughuli mbalimbali za kanisa na zinazomhusu Mungu. Pengine tunapotaka kutatua
au tukiwa na maombi fulani tu ndiyo tunaonekana kanisani. Mfano tukiomba misa kwa
ajili ya marehemu wetu. Familia nzima hufika kusali siku hiyo.
Lakini siku
nyingine za wiki, za jumapili ambapo tunajiona hatuna shida, basi na Mungu hapewi
nafasi yake. Tunaishi na Mungu au tunafanya mambo ya Mungu kimatukio tu. Tukio fulani
na hasa linalotutisha likishapita, basi na Mungu hatumhitaji tena kwa wakati huo.
Kwa kweli haya ni mahusiano hatarishi na Mungu. Hatari ya kumtumia Mungu kama mganga
wa kienyeji.
Tumsifu Yesu Kristo, Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.