Kanisa Katoliki nchini Nigeria limejiandaa kikamilifu ili kushiriki katika mchakato
wa uchaguzi mkuu, kwa kuwatuma waangalizi wa uchaguzi wapatao 4889 katika majimbo
23 ya uchaguzi, wakati wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika nchini Nigeria hapo
tarehe 14 Februari 2015. Wasimamizi kutoka Kanisa Katoliki wanaratibiwa na Padre Evaristus
Bassey, Mkurugenzi wa Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki nchini Nigeria, Caritas
sanjari na Tume ya haki, amani na maendeleo endelevu.
Viongozi wakuu wa dini
nchini Nigeria wanahamasishwa kusaidia kudumisha misingi ya haki, amani na utulivu
wakati na baada ya uchaguzi mkuu nchini humo. Vijana wajiheshimu na kutunza amani
na utulivu na kamwe wasikubali kutumiwa na baadhi ya wanasiasa uchwara ili kuchochea
fujo na vurugu kwa masilahi yao binafsi. Wanasiasa wawe makini katika kampeni na kamwe
wasiwe ni vyanzo vya fujo na machafuko wakati wa mchakato wa uchaguzi mkuu.
Wananchi
wa Nigeria wanakumbushwa kwamba, ulinzi na usalama viko mikononi mwao, hata kama Serikali
imeahidi kuhakikisha kwamba, kuna ulinzi na usalama wa kutosha wakati wa kupiga kura,
lakini wananchi wenyewe wawe pia macho kwani vikosi vya ulinzi na usalama vinaweza
kuzidiwa nguvu na matokeo yake yakawa ni majanga kwa watu na mali zao.
Viongozi
wa kidini wanapaswa pia kujiandaa kwa kutenga fungu linaloweza kutumika kwa ajili
ya kukabiliana na majanga, ikiwa kama yatatokea wakati wa uchaguzi mkuu, kwani hadi
sasa hali ya usalama ni tete sana nchini Nigeria. Kwa miaka mitano sasa, kikundi cha
Kigaidi cha Boko Haram kimekuwa ni tishio kwa maisha na usalama wa wananchi wa Nigeria.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.