2015-02-05 08:43:26

Siku ya Sheria Tanzania


Ifuatayo ni hotuba ya Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania wakati wa sherehe ya kuadhimisha Siku ya Sheria nchini Tanzania, iliyofanyika Jijini Dar es Salaam hapo tarehe 4 Februari 2015. Katika hotuba yake, Rais Kikwete amegusia fursa ya kupata haki nchini Tanzania; huduma ya msaada wa kisheria; wajibu wa Mahakama; mchakato wa kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi na uhusiano uliopo kati ya Mabaraza ya ardhi na Mahakama kuu ya Tanzania. Zaidi unaweza kuendelea kujitarisha mwenyewe!

Nakushukuru sana Mheshimiwa Jaji Mkuu kwa kunialika kwa mara nyingine tena kushirikiana nanyi katika maadhimisho ya Siku ya Sheria Tanzania. Hii ni mara yangu ya nane na ya mwisho kuhudhuria sherehe hizi nikiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Sherehe za mwakani zitahudhuriwa na Rais mpya. Natumai mtaendelea kumualika.

Napenda kuwashukuru wale wote tulioshirikiana nao katika utekelezaji wa jukumu zito la kuimarisha mhimili wa Mahakama katika kipindi changu cha uongozi. Napenda kukutambua, wewe mwenyewe Mheshimiwa Mohamed Chande Othman na Majaji Wakuu waliokutangulia, Mheshimiwa Barnabas Samata niliyemkuta na Mheshimiwa Augustino Ramadhani aliyemfuatia. Nawashukuru kwa ushirikiano wenu, umakini, weledi na umadhubuti wa hali ya juu kwa kuwaongoza wenzenu vizuri katika kutoa haki nchini. Nyote mlikuwa kielelezo kizuri cha utoaji haki hapa nchini na kioo cha uongozi bora wa Mahakama yetu. Pamoja nanyi nawashukuru Majaji wote wa Mahakama ya Rufani na wa Mahakama Kuu, Wasajili, Mahakimu Wakazi, Mahakamu wa Mahakama ya Mwanzo ambao wote mmejitoa kusimamia utoaji wa haki katika nchi yetu. Vile vile, namtambua Mtendaji Mkuu wa Mahakama na Watendaji wa ngazi zote pamoja na watumishi wote wa Mahakama kwa kazi yao nzuri waifanyayo.

Mheshimiwa Jaji Mkuu;
Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu yaani, “Fursa ya Kupata Haki: Wajibu wa Serikali, Mahakama na Wadau” ni muafaka kabisa kwa wakati uliopo. Inatoa fursa kwa mihimili yetu miwili ya dola na wadau wengine kupima jinsi tunavyotimiza wajibu wetu. Naomba tutumie fursa hii tuangalie yale tuliyofanya katika kipindi cha miaka tisa (9) ya uongozi wangu kuhusu kuimarisha utoaji wa fursa ya kupata haki nchini.

Kuboresha utoaji wa haki na utawala wa sheria nchini ilikuwa miongoni mwa mambo tuliyoyapa umuhimu wa juu katika majukumu ya Serikali yetu. Kwa ajili hiyo tumejitahidi kutambua mahitaji na changamoto zilizokuwa zinaikabili Mahakama nchini na kujaribu kutafuta majawabu. Tumechukua hatua na kufanya mambo mbalimbali kwa madhumuni ya kuiwezesha Mahakama kutekeleza wajibu wake wa kutoa haki.

Fursa ya Kupata Haki

Mheshimiwa Jaji Mkuu,
Kama ulivyosema, wewe mwenyewe fursa ya kupata haki imegawanyika katika sehemu mbili. Kwanza, ni fursa ya kuifikia Mahakama, na pili, ni fursa ya kunufaika na huduma za Mahakama yaani kupata haki. Dhana hii inazilazimu Serikali na Mahakama kufanya kazi kwa pamoja, kwani mhimili mmoja pekee hauwezi kufanikisha haya yote mawili. Kimsingi, Serikali inao wajibu wa kuweka mazingira mazuri kwa Mahakama kuweza kutimiza wajibu wake huo wa kutoa haki kwa wakati.

Mheshimiwa Jaji Mkuu;
Ninapoiangalia Mahakama ya leo ninafarijika kuona kwamba hatua zilizochukuliwa na Mahakama yenyewe na nyingine zilizochukuliwa kwa kushirikiana na Serikali zimesaidia kuleta mabadiliko kwenye mifumo na kuboresha utoaji wa haki. Changamoto za kimfumo zilizokuwapo ziliathiri ufanisi katika utoaji haki nchini hususan zilisababisha ucheleweshaji wa mashauri na hukumu.

Hali hii imefanya utatuzi wa migogoro ya mikataba, biashara, ardhi, mahusiano kazini kuchelewa sana (labor matters). Kwa ujumla, jitihada zetu za kukuza uchumi zilipambana na vikwazo vya mifumo yetu ya sheria. Hali kadhalika, kwa upande wa mifumo ya haki jinai, taratibu za kuendesha mashauri hazikuakisi mahitaji ya kutoa haki kwa kuadhibu wakosaji kwa wakati na kutoa fidia na ahueni nyingine inayofaa kwa wahanga wa uhalifu.

Mambo mengi yamefanyika kuboresha Mahakama. Tumetunga Sheria namba 4 ya mwaka 2011 ya uendeshaji Mahakama ambayo pamoja na mambo mengine ilianzisha Mfuko wa Mahakama na kuwezesha Mahakama kuwa na bajeti inayotabirika na ya uhakika. Fedha za Mfuko huu zimekuwa zikiongezeka kutoka bilioni 57.8mwaka 2012/2013 hadi bilioni 89.6 mwaka 2014/15 sawa na ongezeko la asilimia 54.8. Katika mfumo huu mpya tumeanza sasa kutenga bajeti ya maendeleo inayowezesha uwekezaji katika upatikanaji wa miundombinu ya utoaji haki. Nimesikia mwaka huu bajeti ya maendeleo haijaingia, naomba niwahakikishie kuwa mtaipata. Jana nilizungumza na Waziri wa Fedha aliyenihakikishia kuwa katika nusu ya pili ya mwaka huu wa fedha wataanza kutoa fedha.

Jambo lingine muhimu tulilofanya lilikuwa ni kuongeza rasilimali watu. Tumepunguza uhaba mkubwa uliokuwepo na kuwezesha Mahakama kuboresha kazi yake ya kutoa haki. Hivi sasa kuna Majaji wa Rufani 16 kutoka 9 waliokuwepo mwaka 2005 na kuna Majaji wa Mahakama Kuu 81 kutoka Majaji 35 waliokuwapo 2005. Ninafurahi kuwa kati ya Majaji wote wa Mahakama ya Rufaa na Mahakama Kuu waliopo, Majaji 38 sawa na asilimia 39.2ni wanawake. Haya ni mageuzi makubwa. Natambua kuwa mahitaji halisi ni kuwa na Majaji120.

Napenda kukuhakikishia Mheshimiwa Jaji Mkuu kuwa mtakapokuwa tayari nileteeni mapendekezo yenu nifanye uteuzi. Kwa upande wa Mahakimu Wakazi, hadi mwaka huu idadi yao ilifikia 677 nchi nzima ukilinganisha na Mahakimu Wakazi 151 mwaka 2005. Mwaka wa jana pekee tulitoa kibali cha kuajiri Mahakimu wapya 300.

Katika kipindi hiki pia tulifanya mambo mawili mengine muhimu kwa utekelezaji mzuri wa majukumu ya Mahakama. Kwanza ni lile la kukamilisha mchakato wa kutenganisha shughuli za upelelezi na uendeshaji wa mashtaka. Imesaidia kupunguza ucheleweshaji wa mashauri na kuimarisha utoaji wa haki.

Jambo la pili ni kuanzishwa kwa nafasi ya Watendaji wa Mahakama iliyo waondolea Majaji majukumu ya utawala na fedha na kuwaaacha washughulike na utoaji wa haki. Jambo hili limeboresha na kuimarisha utendaji na uendeshaji wa shughuli katika Mahakama kwa namna ambayo haijawahi kuwepo huko nyuma.

Huduma ya Msaada wa Kisheria

Mheshimiwa Jaji Mkuu,
Nakubaliana nawe kuwa kukosekana kwa msaada wa kisheria kwa wale wasio na uwezo wa kulipia huduma ya uwakili ni kikwazo kwa watu hao kupata fursa ya kupata haki. Pia inakwaza utoaji wa haki. Nimefurahishwa na pendekezo lako la kuiomba Serikali kuona uwezekano wa kugharamia huduma za uwakili kwa watuhumiwa wasio na uwezo kifedha nje ya watuhumiwa wa makosa ya mauaji. Umeomba sasa tuangalie na wale wenye makosa yenye adhabu kubwa na vifungo virefu. Nakubaliana nawe kuwa wakati sasa umefika wa kuyaangalia mambo hayo kutokana na mabadiliko mbalimbali yaliyotokea nchini ikiwemo kuongezeka kwa aina ya makosa, adhabu na kuwepo kwa Wanasheria wa kutosha wa kuweza kutoa huduma hiyo ni jambo linalowezekana. Sisi katika Serikali tutalifanyia kazi pendekezo hilo na tutawashirikisha mtupe maoni yenu ya namna bora ya kutekeleza wazo hili. Naamini, tukifanya hivyo, tutakuwa tumepanua fursa kwa watu wengi kupata haki ya kisheria.

Wajibu wa Mahakama

Mheshimiwa Jaji Mkuu,
Kama nilivyosema awali, fursa ya kupata haki inategemea pia jinsi Mahakama inavyotelekeza ipasavyo wajibu wake. Nafurahishwa sana na hatua ambazo Jaji Mkuu umechukua ambazo zimewezesha kuboresha fursa ya kupata haki. Taarifa uliyoitoa hapa leo imeonesha wazi mafanikio yaliyopatikana. Kufuatia uamuzi wenu wa kujiwekea ukomo wa muda wa kuendesha kesi na idadi ya kesi kwa kila Jaji na Hakimu, mmeweza kupunguza mashauri ya siku nyingi kwa asilimia 50 kutoka mashauri 6,887 mwaka 2012 hadi 3,632 katika Mahakama Kuu mwaka 2014. Aidha, mmeweza kumaliza mashauri 52 kati ya 59 yanayohusu miradi mikubwa ya serikali iliyoko katika Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi.

Mheshimiwa Jaji Mkuu;
Natoa rai kwa wadau wengine wa sheria yaani waendesha mashtaka na vyombo vya upelelezi kwa upande wa mashauri ya jinai pamoja na Mawakili wa kujitegemea kuunga mkono juhudi zenu hizi. Bila shaka Mahakama itaendelea kuonyesha njia kwa kusimamia mwenendo wa mashauri ya jinai na madai pasipo kuchelewesha. Ni matumaini yangu kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka na vyombo vya upelelezi havitakuwa chanzo cha kuchelewesha mashauri pasipo sababu za msingi.

Kusogeza Huduma ya Mahakama karibu zaidi na Wananchi

Mheshimiwa Jaji Mkuu;
Natoa pongezi nyingi kwamba kwa sababu ya mambo mbalimbali mazuri yaliyofanyika ambayo yamesogeza huduma za Mahakama karibu na wananchi. Sehemu kubwa ya migogoro inayowagusa moja kwa moja wananchi imeshughulikiwa. Miongoni mwa hiyo ni ile ya ardhi ambapo Mabaraza ya Ardhi yameundwa katika Kata zote nchini chini ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Jambo hili limepunguza sana mzigo wa mashauri katika Mahakama zetu na kusaidia kuleta usuluhishi katika jamii zetu. Inawezekana utendaji wa vyombo hivi una upungufu mbalimbali kinyume cha matarajio ya wananchi. Dawa yake siyo kuvitelekeza bali kuyatambua matatizo yaliyopo na kuyapatia ufumbuzi.

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Halmashauri za Wilaya waendelee kusimamia kwa karibu vyombo hivi muhimu kwa kusogeza huduma ya upatanishi na kushughulikia migogoro midogo ya ardhi. Kuna malalamiko ya kutokuwepo kwa Mabaraza ya Ardhi ya Wilaya katika Wilaya nyingi nchini. Kwa sababu hiyo watu wamekuwa wanapata usumbufu katika kutafuta haki baada ya kutokuridhishwa na uamuzi wa Mabaraza ya Kata. Wizara iharakishe kuunda Mabaraza hayo na Halmashauri zisaidie upatikanaji wa majengo ya Mabaraza hayo.

Uhusiano wa Mabaraza ya Ardhi na Mahakama Kuu

Mheshimiwa Jaji Mkuu;
Naambiwa kuwa yapo malalamiko ya kukosekana mtiririko mzuri wa majalada kwenda Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi. Nia njema ya kuanzisha Mabaraza ya Ardhi imezaa adha. Kilio kilichopo ni kwamba Mabaraza hayo yamekuwa hayataki kutii amri ya Mahakama Kuu ya kupeleka kumbukumbu pindi kunapokuwa na rufaa dhidi ya maamuzi yake ni jambo ambalo sio tu halikutarajiwa bali halikubaliki. Linatia dosari katika utoaji wa haki ya ardhi. Wakati huo huo, Wizara ya Ardhi iwachukulie hatua zipasazo watendaji wa Mabaraza ya Ardhi wanaochelewesha kumbukumbu.

Ni matumaini yangu kuwa wadau wanaohusika yaani Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Katiba na Sheria na Mahakama mtakaa pamoja mapema iwezekanavyo kulitafutia ufumbuzi tatizo hili. Kama itahitaji kupitia upya sheria na taratibu ifanyike hivyo ili kuondoa kikwazo hiki na kuondoa malalamiko yanayoendelea kwa muda mrefu sasa kuhusu jambo hili. Ipo rai kwamba Sheria iwawajibishe watendaji wa Mabaraza ya Ardhi kwa Mahakama Kuu moja kwa moja. Busara na hekima ya kufanya hivyo itafakariwe kwa makini. Ni matarajio yangu kwamba hatua hizi zitachukuliwa mapema na pale kwenye mkwamo tuambiane tuone namna ya kusaidia kukwamua.

Mheshimiwa Jaji Mkuu;
Nimefarijika sana kusikia kwamba mkakati uliopo sasa ni kuongeza weledi kwenye Mahakama za Mwanzo kwa kuendelea kuajiri wahitimu wa Shahada ya Sheria kwenye Mahakama hizo. Hili ni jambo zuri ambalo litawawezesha Mawakili kusimamia na kuendesha kesi kwenye Mahakama za Mwanzo. Madhali sasa, hatuna uhaba wa Wanasheria na Mawakili, hili linawezekana. Uamuzi wetu wa kupanua huduma ya Mahakama Kuu kila Mkoa ni mwendelezo wa dhamira yetu ya kuwafanya wananchi waweze kuifikia huduma hiyo karibu na wanapoishi. Bado tunayo dhamira ya kukamilisha ujenzi wa Mahakama Kuu kila mkoa ifikapo mwaka 2016 kama tulivyoagiza. Utekelezaji wa dhamira hii unakwenda sambamba na uteuzi wa Majaji wengi wa Mahakama Kuu kama nilivyoeleza awali.

Mapendekezo yako, Mheshimiwa Jaji Mkuu, ya kupitia upya taratibu zilizopo ili kufanya utatuzi wa migogoro na utoji haki uwe rahisi na unaoeleweka kwa wananchi ni mzuri. Sehemu kubwa ya mashauri ya madai yanahusu usuluhishi. Kinachotakiwa ni kwa wanaosuluhishwa kuelewa na kuridhika na utaratibu uliotumika kusuluhisha migogoro yao. Nakuomba, Mheshimiwa Jaji Mkuu na wenzako myafanyie kazi mapendekezo hayo ili nchi yetu iwe na mfumo rahisi unaoeleweka wa kutatua migogoro kwa haki, wepesi na haraka. Tukiweza kufikia lengo hili, wananchi wataiona Mahakama ni chombo cha kutatua migogoro na siyo mahali pageni pasipofaa kufika hata kama mtu hana budi kufanya hivyo. Hii itaondoa kishawishi kwa wananchi kutafuta njia nyingine zisizofaa kupata haki zao. Tusikubali tufike huko.

Hitimisho
Mheshimiwa Jaji Mkuu;
Napenda kumalizia hotuba yangu kwa kurudia kukushukuru kwa kunialika kuja kujumuika nanyi siku hii adhimu. Katika kipindi hiki tumefanya mambo mengi yaliyoleta mabadiliko madogo na makubwa katika mifumo ya utoaji wa haki nchini na kuongeza ufanisi. Nawashukuru wale wote tulioshirikiana katika kuleta mabadiliko haya. Busara za Majaji Wakuu watatu walioiongoza Mahakama, Majaji wa Rufani, Majaji wa Mahakama Kuu, Wasajili, Mahakimu na watumishi wengine wa Mahakama ni hazina kubwa na ya kujivunia. Ushirikiano wa wadau mbalimbali umetusaidia kufikia hapa tulipo sasa. Naamini kama watu wataendelea kuitumikia nchi yetu na watu wake kwa moyo wa uzalendo na kujituma tutapiga hatua kubwa mbele.

Baada ya kusema hayo yote naomba sasa niwatakie siku njema ya Sheria nchini.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!








All the contents on this site are copyrighted ©.