Maaskofu kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaoshiriki katika mkutano maalum ulioandaliwa
na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio yenye Makao yake makuu mjini Roma, unaoongozwa na kauli
mbiu "Taifa la kinabii kwa ajili ya ubinadamu mpya", Alhamisi, tarehe 5 Februari 2015
kuanzia saa 12:30, kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Trastevere mjini Roma, wataadhimisha
Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuombea amani nchini Syria, Niger na Nigeria.
Baadhi
ya Maaskofu wanatoka katika maeneo ambayo yameguswa na kutikiswa na vitendo vya kigaidi
huko Syria ambako vita imepachikwa jina la kidini, ili kuendeleza nyanyaso na dhuluma
dhidi ya watu wasiokuwa na hatia. Kuna Maaskofu kutoka Niger ambao hivi karibuni walishuhudia
Makanisa yao yakichomwa moto kwa chuki za kidini, kama inavyojionesha hata Pakistan
na Nigeria ambako Kikundi cha Kigaidi cha Boko Haram kinaendelea kupandikiza mbegu
ya kifo, chuki na uhasama, madonda ambayo itachukua muda mrefu kabla ya kugangwa na
kuponyeka kabisa!
Maaskofu wanasali ili kumlilia Mwenyezi Mungu awapatie amani
na utulivu baada ya kipindi kirefu cha misiba na maombolezo. Maaskofu hawa wanasindikizwa
na sala pamoja sadaka ya waamini kutoka sehemu mbali mbali za dunia, kwa kuwaomba
wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa na wakuu wa nchi husika kuzivalia njuga changamoto hizi
ili kuweza kupata suluhu ya kudumu. Wadau mbali mbali waguswe na mahangaiko ya watu
wanaoendelea kuteseka kutokana na athari za vita pamoja na kulazimika kuyakimbia makazi
yao.
Maaskofu hawa watakuwepo mjini Roma hadi tarehe 7 Februari 2015, wakati
mkutano utakapofungwa na Maaskofu kuanza kurudi tena majimboni mwao, tayari kuendeleza
mchakato wa ujenzi wa amani kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa wengi.
Na Padre
Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.