Baba Mtakatifu Francisko Mapema Alhamisi amekutana na kundi la Maaskofu Katoliki kutoka
Ugriki, waliomtembelea kama sehemu ya hija yao ya kitume katika Ofisi za Kiti Kitakatifu
na Idara za Vatican kwa ujumla. Hotuba ya Papa kwa Maaskofu hao imeanza na salaam
za upendo wa kibaba akisema, hija yao katika makaburi ya Mitume, daima ni tukio maalum
lenye kuimarisha uhusiano wa ushirika na Halifa wa Mtume Petro na dekania nzima ya
Maaskofu, waliotawanyika kote duniani.
Umoja huu wenye kukuza ushirika wa kidugu
kati yao, ni muhimu kwa ajili ya ukuaji wa Kanisa nchini Ugiriki, kama ilivyo pia
kwa ajili ya maendeleo ya jamii. Na kwa nchi yao ni hitaji muhimu zaidi, kwa ajili
ya ufanikishaji mazungumzo, kati ya vyama na taasisi mbalimbali na hasa vya kisiasa,
itikadi na utamaduni, kwa ajili ya ulinzi na udumishaji wa maendeleo kwa manufaa
ya wote. Papa amewataka Maaskofu wasisahau kuwaombea watu waliokabidhiwa katika
huduma yao ya kiaskofu, na kuwa shahidi jasiri wa udugu, mahali popote walipo.
Papa
aliendelea kuuzungumzia udugu katika dekania ya Maaskofu akisema, kwa upande mmoja
inadai ulinzi na uimarishaji wa mila za kijadi na mizizi ya Kikristo ya jamii ya Kigiriki,
na kwa upande mwingine inadai kujifunua kwa uwazi zaidi katika maadili ya kitamaduni
na kiroho, yanayoletwa na wahamiaji wengi, katika roho ya kweli ya kuwakaribisha
ndugu hawa, wake kwa waume bila ya ubaguzi wa rangi, lugha au dini. Papa amesihi,
jamii yao ya Kikristo, ionyeshe kweli umoja kati yao na wakati huo huo kufungua njia
za kukutana na kuwapokea, hasa wahamiaji walio katika hali ngumu zaidi, ambao wanaweza
kutoa mchango wao katika kuleta mabadiliko chanya katika jamii, sambamba mafundisho
ya Injili.
Papa alionyesha kufurahia kwamba, tayari Maaskofu wanashiriki katika
shughuli hii kupitia kazi zao za kichungaji na hisani, hasa kwa ajili ya wahamiaji,
ambao wengi wao ni Wakatoliki. Kwa moyo wake wote Papa amewahimiza Maaskofu waendelee
na jitihada mpya za kimisionari, na hasa kwa kuwashirikisha zaidi vijana: ambao ni
mustakabali wa taifa.
Papa aliendelea kuzungumzia changamoto za uchumi na
fedha zinazowakabiliwa, kama ilivyo sehemu nyingine za dunia, na kuwataka wasichoke
wala kukata tamaa katika kujenga tumaini kwa ajili ya siku zijazo. Na wawe na ujasiri
wa kupambana kile kinachojulikana kama utamaduni rajua, kuona kwamba mambo yote ni
mabaya. Papa amehimiza moyo wa mshikamano ambao Wakristo wote wanatakiwa kuuishi na
kuushuhudia katika hali halisi ya maisha ya kila siku, kama chachu ya mshikamano na
matumaini.
Amesema, Ni muhimu kwamba, kila Askofu anadumisha uhusiano wake
wa karibu na utawala wa nchi, ikiwa ni pamoja na taasisi na vyama mbalimbali vya
jamii, ili kueneza moyo wa umoja na mshikamano, kupitia njia ya majadiliano na kushirikiana
na nchi nyingine za Ulaya. Katika roho hiyo, Papa pia amewahimiza waendelee na
mazungumzo ya ana kwa ana na Waotodosi, katika kuilisha safari muhimu ya kiekumeni
na matarajio mazuri katika utulivu na mafanikio ya kiroho kwa manufaa yao wote.
Papa
pia hakuchelea kuzungumzia utekelezaji wa utume wa Uinjilishaji na kukuza ubinadamu
kama wito wa Kanisa nchini Ugiriki, na huduma isiyokwepeka katika ukarimu na motisha
ya viongozi wa dini. Kwa hiyo, aliwasihi, Maaskofu waongeze zana sahihi, huduma nzuri
kitaaluma, na kushughulikia upungufu wa watumishi. Katika suala hili, aliwaomba wafikishe
kwa mapadre wa majimbo yao, ambao wengi wao ni wazee, upendo wake kwa wote na shukrani
zake za dhati kwa bidii yao ya kitume, licha ya ufinyu wa njia.
Papa ametaja
umuhimu na thamani ya mchango wa kutangaza Injili kwa Taasisi za Maisha wakfu, na
akatoa mwaliko wa kutoa angalisho makini sahihi, kwa sababu, licha ya matatizo mengi,
lengo la Unjilishaji liweze kuendelezwa Ugirki. Papa alieleza huku akipeleka mawazo
yake hasa katika uwanja wa elimu. Na pia katika uimarishaji wa jamii ya Kikristo,
akisema wameitwa kuongeza nafasi ya waamini walei katika utendaji wa shughuli nyingi
za Kanisa. Na kwamba, Ushirikiano wao na huduma ya maaskofu na makasisi inahitajika
kushughulikia changamoto za leo na pia katika mtazamo wa siku zijazo.
Na hii
ina maana ya kuwa na malezi mazuri ya kutosha kupitia mipango ya elimu, na pia katika
lengo la kuongeza uwepo wa walei katika harakati na vyama Kanisa. Na haya yote yanahitaji
maongozi mazuri ya Kichungaji, popote kuwawezesha walei kuthamini dhamira yao ya
kimisionari na furaha ya kuwa Mkristo, katika kueneza na kutenda daima kwa maelewano
ya pamoja na miongozo ya kichungaji kwa Makanisa maalum iliyowekwa kijimbo na katika
Parokia.
Papa pia amezungumzia hoja ya kudhoofika kwa familia, ambako pia
kunasababishwa na changamoto za malimwengu, na hivyo inahitaji dhamira ya Kanisa ya
kudumu katika mipango ya utoaji mafunzo kwa wale wanaolenga kufunga ndoa, na hasa
juu ya malezi ya vizazi mpya, kama sehemu ya malezi ya Kikristo.
Amewataka
Maaskofu wasisahau kundi la wazee katika huduma yao , wazee ambao wengi wao sasa
wanajikuta wameachwa katika upweke au kutelekezwa, kwa sababu kuzuka kwa utamaduni
wa taka, unaozidi kupanda chati siku hadi siku kila mahali. Maaskofu wasichoke kusisitiza
kwa maneno na vitendo kwamba uwepo na ushiriki wa wazee katika jamii ni muhimu kwa
jamii kutembea katika njia sahihi.
Papa alikamilisha hotuba yake na shukurani
za dhati kwa Maaskofu, kwa ajili ya kazi ya uinjilishaji ambayo, licha ya matatizo
mengi, wanaendelea kuifanya nchini mwao Ugriki. Na akashukuru kwamba, kutambuliwa
kisheria Kanisa Katoliki na serikali , ni tukio kubwa muhimu, la kuwapa nguvu na
ujasiri wa kutenda kwa kujiamini zaidi kwa ajili ya ufanikishaji utendaji wa leo na
pia kwa ajili ya manufaa ya siku zijazo, kwa shauku zaidi katika kuwa mashahidi
wa Bwana, aliyekufa na kufufuka.
Papa amewaomba Maaskofu wajenge moyo wa
kuvumilia kwa furaha ya Kiinjili. Na aliwakabidhi Mapadre, watawa na waamini wote
wa kawaida wa Majimbo yao, chini ya maombezi ya Bikira Maria na, pia akaomba maombi
yao kwa ajili yake mwenyewe na kwa ajili ya huduma yake kama Khalifa wa Mtume Petro,
na kuwapa Baraka zake za Kitume.