Wananchi wa Riunione wanatarajiwa kufanya uchaguzi mkuu hapo tarehe 22 na tarehe 29
Machi 2015 ili kuwachagua viongozi watakaosaidia mchakato wa kukoleza maendeleo endelevu,
kwani hii ni haki msingi ya kikatiba na sehemu ya utekelezaji wa demokrasia. Uchaguzi
mkuu isiwe ni fursa ya kuwagawa watu, kuanzisha fujo na vurugu, kwani siasa inapaswa
kujikita katika mchakato wa kutafuta na kudumisha mafao ya wengi.
Hii ni sehemu
ya ujumbe ulioandikwa na Askofu Gilbert Aubry wa Jimbo Katoliki la Saint- Denis, kama
sehemu ya maandalizi ya uchaguzi mkuu nchini humo na kwamba, kuna haja ya kuwachagua
viongozi wanaonesha nia na ari ya kutaka kuwatumikia wananchi ili kuweza kukabiliana
barabara na changamoto za maisha badala ya kuwachagua viongozi wanaotaka madaraka
ili kujinufaisha wao wenyewe na ndugu zao.
Viongozi wa kisiasa waoneshe dira
na mikakati ya kupambana na ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana wa kizazi kipya na
kwamba, rasilimali na utajiri wa nchi usaidie kujenga na kuimarisha jamii; kwa kushirikiana
na kusaidiana, kwani kimsingi siasa inapaswa kukoleza mafao ya wengi katika medani
mbali mbali za maisha. Ni wajibu wa kila mwananchi kuhakikisha kwamba anashiriki kikamilifu
katika ustawi na maendeleo ya nchi yake kadiri ya nafasi na dhamana yake ndani ya
jamii. Kamwe nchi isigeuzwe kuwa ni msitu wa vita na machafuko; mahali ambapo binadamu
kwa binadamu wanawindana ili kumalizana!
Askofu Gilbert Aubry anawataka waamini
na wananchi kwa ujumla kuachana na falsafa ya kutaka kulipizana kisasi, kwa kujenga
na kudumisha amani na maridhiano kwa kuanzia ndani ya mtu binafsi, familia na jamii
katika ujumla wake. Mafao, utu na heshima ya binadamu vipewe kipaumbele cha kwanza
katika dira na mikakati ya maendeleo ya wengi. Kanisa na Jamii vinapaswa kushirikiana
ili kuhakikisha kwamba, kweli wananchi wanajipatia maendeleo ya kweli sanjari na kuendelea
kutunza amani na utulivu!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili
ya Radio Vatican.