Maaskofu 70 kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wanaojisadaka kwa ajili ya maskini
na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii ni kati ya Familia ya Mungu iliyohudhuria
Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko siku ya Jumatano, tarehe 4 Februari 2015, kwenye
Ukumbi wa Mikutano wa Paulo VI, ulioko mjini Vatican. Hawa ni Maaskofu wanaoshiriki
katika mkutano ambao umeandaliwa na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio yenye Makao yake Makuu
mjini Roma.
Akiwatambulisha Maaskofu hawa, Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Rais
wa Baraza la Kipapa la Familia, alimwambia Baba Mtakatifu kwamba, kundi hili la Maaskofu
liko mjini Roma, ili kufanya hija ya pamoja inayopania kujenga na kudumisha umoja
wa Kanisa katika huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Hii
ni huduma ya upendo inayomgusa na kuacha chapa ya kudumu katika maisha ya mwamini;
kwa kuvuka mipaka ya kudhaniana vibaya, tayari kuanza mchakato wa urafiki na udugu.
Maaskofu wanatambua kwamba, katika maisha na huduma yao, wanaliwakilisha Kanisa
katika huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Mama Kanisa
anawatuma watoto wake kuzingatia haki na kutenda mema, ili waweze kupata maisha ya
uzima wa milele.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili
ya Radio Vatican.