Askofu mkuu Maurice Gardès wa Jimbo kuu la Auch, Ufaransa anasema, hata katika shida
na mahangaiko, magonjwa na taabu, mwanadamu anaweza kuonja furaha na amani ya ndani,
kinyume kabisa cha baadhi ya watu wanaodhani kwamba, mgonjwa hawezi kuwa na furaha
eti kwa sababu ya ugonjwa wake. Hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya furaha ya
mtu na udhaifu wake wa kimwili kutokana na ugonjwa.
Askofu mkuu Gardès anasema,
ulimwengu mamboleo unakumbana na changamoto nyingi ambazo zinamwondolea mwanadamu
ile furaha na amani ya ndani. Kati ya mambo haya kuna magonjwa: mateso, kuvunjika
kwa ndoa, vita, ukosefu wa fursa za ajira pamoja na vizingiti vya maisha ya kawaida
katika hija ya mwanadamu, kiasi cha kumwachia nafasi ndogo kabisa ya kuweza kufurahia
ndoto na matamanio ya moyo wake.
Askofu mkuu Gardès anayasema haya yote katika
barua yake ya kichungaji kwa Familia ya Mungu Jimbo kuu la Auch, Ufaransa, kama sehemu
ya maandalizi ya Jumapili ya Wagonjwa, ambayo inafanyika jimboni humo tarehe 8 Februari
2015, ili kutoa nafasi kwa waamini kuweza kushiriki kwa wingi, ingawa, Siku ya Wagonjwa
Duniani inaadhimishwa hapo tarehe 11 Februari 2015 sanjari na Kumbu kumbu ya Bikira
Maria wa Lourdes.
Askofu mkuu Gardès anasema kuna haja kwa watu kutofautisha
kati ya furaha na anasa, kwa kukubali na kuthamini hata udhaifu wa mwili wa mwanadamu.
Inasikitisha kuona kwamba, kuna baadhi ya watu wanadhani kwamba, furaha ya kweli inajikita
katika fedha na utajiri kwani waswahili wanasema, eti "fedha ni sabuni ya roho". Kuna
watu wanadhani kwamba, furaha inapatikana katika ulimbwende, huko watu watajikwatua
hadi kuchubuka, lakini wapi, bado utawakuta watu hawa hawana ile furaha ya kweli.
Na wengine wanadhani kwamba, furaha inapatikana kwa njia ya mafanikio katika taaluma,
hata huko nako, bado wanabaki wakiwa na midogo wazi! Wanashangaa na kupigwa na bumbuwazi!
Maajabu ya Mungu.
Askofu mkuu Gardès anasema, unaweza kumkuta maskini hata
katika umaskini wake anakicheko na furaha isiyokuwa na makunyanzi, kwani anaipokea
na kuikubali hali yake ya ubinadamu na hivyo kuwa na amani na utulivu wa ndani mambo
msingi katika maisha ya binadamu na wala si fedha, ulimbwende na mafanikio katika
taaluma. Mwanadamu kwa kukubali mapungufu na udhaifu wake, anaweza kuishi kwa amani
na utulivu, kwani mambo yote haya yanategemea jinsi ambavyo mtu mwenyewe anayakubali
na kuyapokea katika safari ya maisha yake ya kila siku!
Askofu mkuu Gardès
anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kufanya tafakari ya kina kuhusu
Heri za Mlimani; muhtasari wa mafundisho makuu ya Yesu, ambayo ni kinyume kabisa cha
utamaduni wa watu mamboleo wanaopenda anasa na starehe; watu wanaotaka "kula kuku
kwa mrija, huku wakiwa wameketi kwenye viti virefu". Katika shida na mahangaiko ya
ndani, mwanadamu anatafuta faraja na utulivu kwa wale wanaomzunguka; watu hawa wanakuwa
ni dawa inayoganga madonda na hivyo kumkirimia mtu furaha na utulivu wa ndani.
Kuna
haja ya kuendelea kufanya maboresho katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu,
ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi pamoja na kuhakikisha
kwamba, watu wanawaonesha upendo na mshikamano wagonjwa na wale wote wanaoteseka kutoka
na shida na magumu mbali mbali ya maisha. Wakristo wanahamasishwa na Mama Kanisa kuwasaidia
na kuwahudumia wagonjwa, kwa kukubali udhaifu na mateso ya mwanadamu. Udhaifu wa mwanadamu
na furaha ya kweli, vinapatikana kwa mwamini kuwa mfuasi mwaminifu na mkweli wa Yesu
Kristo.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio
Vatican.