Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 5 Februari 2015 amekutana na kuzungumza
na Rais Anote Tong wa Jamhuri ya Watu wa Kiribati; baadaye amekutana na Kardinali
Pietro Parolin, aliyekuwa ameandamana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu
mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.
Mazungumzo
kati ya viongozi hawa wawili yamejikita katika umuhimu wa kulinda na kutunza mazingira
pamoja na masuala mbali mbali yanayogusa mabadiliko ya tabianchi na athari zake nchini
humo, kama ilivyo pia kwa nchi ambazo ziko kwenye Bahari ya Pacific, ambazo mwara
kwa mara zinakabiliwa na majanga asilia. Mazungumzo haya yamelenga pia katika mkutano
wa kimataifa utakaojadili kuhusu mabadiliko ya tabia nchi utakaofanyika mjini Paris,
Ufaransa, Desemba 2015. Ni matumaini ya viongozi hawa wawili kwamba, Jumuiya ya Kimataifa
itafanya maamuzi mazito na yanayotekelezeka ili kukabiliana na changamoto za athari
za mabadiliko ya tabianchi.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya
Kiswahili ya Radio Vatican.