2015-02-04 07:39:24

Vipaumbele: Familia, Wakimbizi na Amani!


Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika ya Kati, ACEAC, linalounganisha Maaskofu kutoka DRC, Rwanda na Burundi, katika mkutano wao wa mwanzo wa mwaka wamejadili na kukazia kwa namna ya pekee, umuhimu wa Familia ya Mungu kusimama kidete kulinda na kutetea tunu msingi za maisha ya familia; ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji sanjari na ujenzi wa misingi ya haki na amani. Hizi ni kati ya changamoto zinazofanyiwa kazi na Kanisa huko Afrika ya Kati.

Ujumbe uliotolewa na Maaskofu baada ya mkutano huu, unawahimiza waamini kushuhudia Injili, kwa kumwilisha imani katika uhalisia wa maisha, huku wakiendelea kuwashirikisha jirani zao, tunu msingi za maisha ya Kikristo na utu wema; mambo ambayo kwa sasa hayana budi kupewa kipaumbele cha pekee. Kanisa katika maisha na utume wake, linapenda kuwa ni chumvi na mwanga wa dunia, hasa wakati huu ambapo kuna pilika pilika za mchakato wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu nchini Burundi.

Kuna baadhi ya wanasiasa wanataka kuhakikisha kwamba, wanaingia madarakani kwa nguvu zote, hata ikibidi, kumwaga damu! Jambo ambalo Maaskofu wanasema, haliwezi kukubalika, kumbe, kuna haja kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuendelea kujikita katika misingi ya haki, amani na demokrasia ya kweli, huku wakiombea amani na utulvu, ili demokrasia ya kweli iweze kushika mkondo wake.

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika ya Kati, linapenda kuwasindikiza wanasiasa katika utekelezaji wa mikakati na sera za maendeleo na uchumi kwa kujikita katika mchakato wa haki, amani na upatanisho katika eneo la Maziwa Makuu. Maaskofu bado wanaendesha kampeni ya amani katika eneo la Maziwa Makuu, kampeni ambayo ilizinduliwa kunako mwaka 2013, kwa lengo la kushuhudia imani kwa Yesu Kristo, Mfalme wa amani; sanjari na kuwajengea wananchi uwezo wa mfungamano wa kijamii, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mchakato wa amani, badala ya kutumia mtutu wa bunduki.

Ni wajibu wa Familia ya Mungu, kutoka katika eneo la Maziwa Makuu, kuhakikisha kwamba, inajielekeza katika ushuhuda wa maisha unaopania kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya chachu ya Injili inayofumbatwa katika utamaduni wa haki na amani.

Maaskofu wanasema kwamba, mchakato wa Uinjilishaji mpya sanjari na familia ni kati ya vipaumbele vya maisha na utume wa Kanisa katika eneo la Maziwa Makuu. Maaskofu wanaendelea kutafakari kuhusu matatizo, changamoto na fursa mbali mbali ambazo familia nyingi zinakabiliana nazo, ili kuweza kutoa majibu muafaka na kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia itakayofanyika mjini Vatican, mwezi Oktoba, 2015.

Maaskofu wanasema, kuna haja ya kuonesha ushirikiano na mshikamano wa dhati miongoni mwa nchi za Maziwa Makuu, katika harakati za kuwasaidia na kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji, dhamana inayoweza kuratibiwa kwa njia ya Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki, yaani Caritas katika nchi husika. Mwishoni, Maaskofu wametembelea kwenye eneo la Kumbu kumbu ya Kabgay, ili kutoa heshima zao kwa wale wote waliopoteza maisha yao wakati wa mauaji ya kimbari yaliyofanyika nchini Rwanda kunako mwaka 1994.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.