Serikali ya Tanzania imewataka wamiliki wa viwanda kuwapa ushirikiano wadadisi wa
Sensa ya Viwanda watakaopita katika maeneo yao kwa lengo la kukusanya takwimu sahihi
za viwanda vilivyopo nchini na mchango vinaotoa katika maendeleo ya taifa. Kauli hiyo
imetolewa Jijini Dar es salaam na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara
Maria Biliawakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku 14 ya wadadisi wa Sensa ya Viwanda
yanayoendelea katika Chuo cha Takwimu cha Mashariki mwa Afrika kilichopo eneo la Changanyikeni
jijini Dar es salaam.
Amesema kuwa mafanikio ya Sensa hiyo yatatokana na
wamiliki wa viwanda kuthamini na kutambua umuhimu za Sensa hiyo kwa kutoa ushirikiano
kwa wadadisi watakaopita katika maeneo yao kupata taarifa zinazohusu masuala mbalimbali
ikiwemo uzalishaji wa bidhaa na masuala ya ajira; Amesema upatikanaji wa takwimu sahihi
kuhusu Sekta ya Viwanda nchini Tanzania utaiwezesha Serikali kuweka Sera na mipango
endelevu ya maendeleo itakayoisaidia sekta hiyo kupiga hatua kimaendeleo.
“Sensa
hii ya viwanda ni muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu, na mafanikio yake yatatokana
na wenye viwanda kutupa ushirikiano maana bila wao kutoa takwimu sahihi mipango ya
maendeleo kuhusu viwanda haitatekelezeka kwa sababu ya kukosa takwimu sahihi” Amesema
Bilia.
Kuhusu sampuli ya viwanda vitakayoguswa na Sensa hiyo amesema ni
pamoja na maeneo ya viwanda yaliyoajiri watu wengi na yanayohusisha uzalishaji mkubwa
wa bidhaa za viwandani ,maeneo ya uzalishaji wa bidhaa za kokoto, bidhaa za vyakula
na maeneo yaliyoajiri mtu zaidi ya mmoja.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu
wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Dkt. Albina Chuwa akizungumza wakati wa ufunguzi wa
mafunzo hayo amesema kuwa Sensa hiyo ya viwanda itakayohusisha viwanda vyote nchini
inafanywa kwa ushirikiano wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu na Wizara ya Viwanda na Biashara.
Amesema
kukamilika kwa Sensa hiyo kutaliwezesha taifa kuwa na takwimu sahihi za viwanda na
kutambua mchango wa Sekta ya viwanda katika uchumi wa taifa na mchango wa ajira kwa
wananchi.
Kuhusu mafunzo hayo ya siku 14 kwa wadadisi 200 watakaoendesha
zoezi hilo amesema Ofisi ya Taifa ya Takwimu kupitia Chuo cha Takwimu cha Mashariki
mwa Afrika inaendesha mafunzo hayo kwa vitendo na nadharia ili kuwawezesha na kuwajengea
uwezo wadadisi hao kukusanya takwimu bora. “Lengo la kuendesha Sensa hii ni kuhakikisha
kuwa nchi yetu inapiga hatua na kuwa nchi yenye maendeleo ya kati kwa kuwa na matumizi
sahihi ya takwimu ztu”
Kaimu Mkurugenzi wa Shirikisho la wenye Viwanda
nchini Bw.Hussein Kamote akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo kwa niaba
ya wamiliki wa Viwanda nchini amesema kuwa Sensa ya viwanda itakayofanyika nchini
mwezi huu italiwezesha taifa kuwa na takwimu sahihi zinazohusu sekta ya viwanda. “Sensa
hii ya viwanda ni muhimu sana kwa maendeleo ya taifa nawaomba wenye viwanda watoe
ushirikiano wa kutosha maana bila wao zoezi hili litakuwa gumu”
Ameongeza
kuwa Sensa ya viwanda ni muhimu kutokana na mchango wake katika nchi nyingi za Asia
ambazo zimefanikiwa na kupiga hatua kimaendeleo kwa sababu ya kuwa Sensa endelevu
na takwimu sahihi za sekta ya viwanda na mchango wake katika pato la taifa.