2015-02-04 08:26:08

Fumbo la Kifo!


Nalikuwa macho kwa kipofu, nalikuwa mguu kwa aliyechechemea, ndiyo kauli mbiu inayoongoza maadhimisho ya Siku ya 23 ya Wagonjwa Duniani, inayoadhmishwa tarehe 11 Februari 2015 sanjari na Kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Lourdes. Ni siku iliyoanzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II, ili kuonesha mshikamano wa upendo na watu wanaoteseka kutokana na magonjwa mbali mbali pamoja na kuwatia shime, wale wanaowahudumia ili kutekeleza dhamana hii kwa unyofu na uadilifu mkubwa, kwa kutambua utu na heshima yao kama binadamu!

Baraza la Maaskofu Katoliki Uswiss, linaadhimisha Jumapili ya Wagonjwa nchini humo hapo tarehe 1 Machi 2015, kwa kuwataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuondokana na unafiki unaojificha katika sera na mikakati inayopania kukoleza maboresho ya afya ya jamii, kwa kudhani kwamba, watu wenye magonjwa yasiyokuwa na tiba au magonjwa ya muda mrefu hawastahili kuishi na matokeo yake watu wengi wanaanza kukumbatia utamaduni wa kifo unaojikita katika kifo laini au Eutanasia au hata kwa wagonjwa wenyewe kutema zawadi ya maisha kwa kutoona tena thamani na maana ya maisha.

Baraza la Maaskofu Katoliki Uswiss linawataka waamini na watu wenye mapenzi mema, kuhakikisha kwamba, wanawaonesha wagonjwa na ndugu zao upendo na mshikamano wa dhati, kama kielelezo makini cha kushuhudia Injili ya Uhai, Upendo na Mshikamano, unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. NI wajibu wa wanafamilia na wahudumu katika sekta ya afya kuwasaidia wagonjwa kukabiliana kikamilifu na Fumbo la Kifo, kwa amani, imani na matumaini.

Maaskofu wanatambua kwamba, tangu mwanadamu anapozaliwa anaanza safari ya kukabiliana na kifo, kumbe, wagonjwa waonjeshwe upendo, huruma na utu, ili waweze kulipokea Fumbo la Kifo kwa imani. Wakati mwingine, ugonjwa ni hija inayomsaidia mgonjwa kuanzisha mchakato wa upatanisho kati ya nafsi ya mtu pamoja na Mungu wake; kumbe hakuna sababu ya mtu kutema zawadi ya maisha, akitambua kwamba, anapendwa na kuthaminiwa na Mwenyezi Mungu, huku akiwaachia ndugu na jamaa kuamua hatima ya maisha yake.

Jamaa wawasaidie wagonjwa, lakini si kwa kuwasindikiza katika kitanda cha mauti kwa njia ya kifo laini; kwani hata katika mateso na magonjwa, mwanadamu bado anaweza kuonja upendo na huruma ya Mungu katika maisha yake. Baraza la Maaskofu Katoliki Uswiss, linahitimisha ujumbe kwa Jumapili ya Wagonjwa, kwa kumwomba Bikira Maria, ili aweze kuwaombea wagonjwa na wale wote wanaoteseka, bila ya kuwasahau watu wote wanaowahudumia wagonjwa: kiroho na kimwili, ili huduma hii kwa wagonjwa, iwasaidie watu kuonja hekima ya kweli ya maisha ya kiroho.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.