Homa ni ugonjwa wa ajabu unaolegeza viungo vya mwili kutokana na kupanda na kushuka
kwa joto mwilini. Kadhalika homa inamnyima mgonjwa hamu ya kula. Mapato yake homa
inamdhoofisha na kumkosesha nguvu na kumlaza kitandani na mgonjwa hawezi kufanya shughuli
yoyote ile.
Kwa kiswahili cha mitaani, neno “homa” linatumika kumaanisha woga
wa kukabili maisha, mathalani hali ya kuogopa mitihani wanaita “homa ya mitihani”
au yamaanisha pia udhaifu au tabia mbaya inayoweza kumkumba mtu au hata kuikumba jamii
fulani wanaita “homa ya jiji, homa ya kijiji, homa ya vijana, homa ya Kanisa, homa
ya Wakristo, homa ya watawa, homa ya mapadre, homa ya mabunge wetu, nk, wakimaanisha
kasoro au tabia fulani mbovu inayoinasa na kuipagawaza jamii hadi jamii nzima ikajisikia
inaumwa nayo bila kujitambua.
Kwa mfano tunaweza pia kusema rushwa ni “homa
ya nchi,” au tabia ya kuiga mitindo ya maisha ya mataifa ya ulaya au Amerika, hiyo
ni “homa ya Waafrika.” Homa za mtindo huo zinaweza kuwadhoofisha watu wote hata viongozi
wa serikali na dini hadi wanalazwa kitandani na kushindwa kufanya kazi ya haki, upendo
na amani. Aidha ni ngumu sana kupona toka homa aina hizo.
Hebu leo tumfuatilie
kwa makini mwalimu, mwanamapinduzi anavyomnusuru mtu mwenye kunaswa na homa kali hadi
kumlaza kitandani, na baada ya kupona anaendelea na shughuli zake za kawaida. Kituko
cha leo ni kifupi sana ukikilinganisha na vituko vingine vilivyoelezwa katika injili.
Lakini kinavyoelezwa, hakimaanishi kutupatia taarifa au maarifa ya kiakili, bali kipo
kwa ajili ya kutupatia ujumbe mkuu wa maisha yaani ni kama katekisimu. Mwinjili anataka
kutuonesha mabadiliko, au mapinduzi yaliyoweza kupatikana ulimwenguni hapa baada ya
Yesu kuingia duniani.
Tulishasikia kwamba ilikuwa ni siku ya Jumamosi (Sabato)
Yesu alikwenda kwenye Sinagogi kufanya ibada. Kule Sinagogini tulikishuhudia kizungumkuti
cha mtu mwenye mapepo. Mara baada ya ibada hiyo ya Jumamosi Yesu akatoka na wanafuasi
wake Petro na Andrea wakitanguzana pia na Yakobo na Yohane waliokuwa wameitwa kumfuata
wakarudi kuelekea nyumbani kwa Petro palepale kijijini Kafarnaum.
Wanapofika
nyumbani kwa Petro na Andrea, wafuasi hawa wanamkuta mamamkwe yaani mama ya mke wa
Petro anayo homa na amelala hoi kitanda hajiwezi. Mara moja wafuasi hawa wanamtaarifu
Yesu. Kitendo hiki cha wafuasi kuchukua jukumu la kumtaarifu Yesu, kinatufundisha
kuwajibika tunapoona ndugu au jirani anaumwa.
Kwa hiyo yasemwa: “Mkwewe simoni
mamaye mkewe, alikuwa kitandani, hawezi homa,” maana yake amelala kitandani na hawezi
kufanya chochote, hawezi kuamka na kushughulika na kazi ya kujenga familia au taifa.
Amefungwa, amezuiliwa na hawezi kuwa mtu kamili na kufanya anachotakiwa mtu mwenye
afya kukifanya. Homa hii haijulikani imesababishwa na ugonjwa gani bali ni homa tu.
Hali ya homa ya mkwe wa Petro inawakilisha ulimwengu wa kale, ulimwengu ambao siyo
wa utu kamili. Sisi sote ni waana wa Mungu, na tunao uana wa kimungu ndani mwetu,
lakini uana huo ukipatwa na homa haukui bali unabaki umesinyaa tu kama “Kandunji”
yaani mtu aliyedumaa na asiyerefuka.
Hiyo ni homa ya maisha. Je, ni homa gani
inayotudumaza, inayotulaza kitandani tusiweze kuinuka, tusiweze kuwa watu na watoto
halisi wenye sura ya Mungu? Homa hii inayotupooza kabisa ndiyo ubinafsi, yaani kujifikiria
mwenyewe tu. Kutojali wala kuwathamini wengine. Homa inayotuzuia tusikue na kuendelea
kuwa na ule uwaana wa Mungu ulio ndani mwetu ambao ni kufanya kazi ya kutumikia wengine
kwa upendo.
Hebu tuone jinsi Yesu anavyoponya homa hii. Kwanza anamkaribia
mgonjwa, yaani hamwogopi mwenye homa bali anamkaribia. Katika tendo hilo la kukaribia
sisi tunapata ujumbe muhimu, yaani kule kumkaribia mgonjwa kwaonesha kuthamini na
kugundua hali inavyomnyima jirani na jamii utu stahiki. Hali halisi ya ulimwengu haijali
utu, yaani homa ya ulimwengu, kama vile umaskini, maradhi, vita, unyanyasaji, rushwa,
wongo, nk. Sisi hatuikabili homa hiyo kwa karibu. Tunatoroka tunapoona mambo hayaendi
inavyotakiwa.
Kumbe Yesu anapoikaribia na kuikabili homa, hapo hali inabadilika.
Katika homa kama hii inayomfanya mmoja asiweze kuamka kuwa mtu kamili na kuendelea
kufanya kazi haifai kujifanya hamnazo na kutoona au bila kusema kitu. Kama hakuna
anayekaribia basi unaalikwa wewe mkristu kukaribia na kuikabili. Hivi hatua ya kwanza
ni kuikabili hali halisi ya homa. Baada ya kumkaribia mgonjwa, Yesu anamshika mkono
na kumwinua. Kwa kigiriki kuinua ni “egeirein” lenye maana ya kumwinua
usingizini kama vile angekuwa mfu na kumpa tena uhai. Ama kweli mtu asiyeweza kupenda,
mtu mbinafsi huyo ni mfu ni msiba unaotembea. Yaonekana kuwa mama huyu alikuwa kama
mfu tu, hivi Yesu anamwinua, hapo homa inamwacha.
Mara tu baada ya kupona “anawatumikia.”
Hapo maisha mapya yanaonekana katika kutumikia, katika kuwapenda wengine, na kufanya
kitu kwa ajili ya jamii. Mtu amepona pale anapoanza kutumikia. Huyu sasa ni mtu mpya
aliyezaliwa katika mazingira fulani anayoshindwa kupenda na sasa anakuwa tayari kumtumikia
jirani hasa pale anapolitambua Neno la Mungu. Kwa hiyo mapinduzi aliyofanya Yesu hapa
ni kule kumwinua mgonjwa na kumfanya aweze kutumikia ndugu zake. Tunapotaka kutumikiwa
na wengine hapo tunakuwa na homa ya ubinafsi, tunakuwa wafu. Kumbe tunapotumikia wengine
tunakuwa huru.
Katika kuhitimisha sehemu hii inasemwa kwamba “kulipokuwa jioni,
na jua limekwisha kuchwa, walikuja wagonjwa wengi na wenye pepo. Wote walikuwa wamekusanyika
mlangoni.” Kusanyiko hilo linaeleweka kabisa kwa vile ilikuwa ni jumamosi jioni siku
ya mapumziko na asubuhi yake walikuwa kwenye ibada ya Sinagogi. Lakini kulikoni wakusanyike
mlangoni, tena basi ni mlangoni pa nyumba ya famili alimokuwa anaishi Yesu na Petro?
Hapo mlangoni, ndipo palijaa fundisho kwetu. Yaonekana mle ndani ya nyumba
kulikuwa na Neno la uhai, neno linalookoa na linaloponya aina ya homa za watu wote
waliokusanyika pale mlangoni. Kwa hiyo picha na fundisho unayoweza kuipata ni kwamba
ulimwengu mzima unasubiri katika mlango wa nyumba inamokaa familia na jumuia yenye
kutoa Neno la amani, Neno la utu, Neno la haki na Neno la upendo na heshima.
Hapa
unaachiwa mwenyewe kufanya tafakari juu ya nyumba yako na jumuia yako hata dini yako,
endapo watu wanakusanyika hapo na kwa lipi. Kama watu hawakusanyiki mlangoni pa nyumba
ya mtu ujue wakazi wake wamehama au wamelala kitandani hawawezi homa. “Palipo na upendo
na mapendo hapo Mungu yuko.”
“Alfariji na mapema sana Yesu akaondoka na kwenda
kuomba.” Lengo la kuomba ni kutaka kuunganisha matendo na maneno yake na mapenzi ya
Mungu Baba yake. Kwa hiyo, hata sisi tukitaka kujenga ulimwengu yabidi kulinganisha
shughuli zetu katika maisha na mapendo ya Mungu.
Petro na wafuasi hawakuelewa
kwa nini Yesu anaomba au anasali wakamwambia: “Watu wote wanakutafuta.” Yesu ikabidi
awaambie wazi kwamba ujumbe huu unaowanasua watu toka kwenye homa zako, tusiubinafsishe
na kuubana ubaki hapa Kafarnaumu, bali twendeni vijiji vingine, kwa jumuia zote za
Kiyahudi, na ulimwengu wote tukatangaze Neno hili litakalomwamsha mtu kutoka “homa
ya jiji” yaani ubinafsi.